Begi la umemejua: Mkombozi wa elimu Tanzania

February 17, 2023 5:33 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Lina taa ya umemejua inayowasaidia wanafunzi kusoma usiku.
  • Huwaepusha wanafunzi na madhara ya kiafya.

Dar es Salaam. Huenda ufaulu wa msomo ukaongezeka kwa wanafunzi waishio vijijini nchini Tanzania baada ya wabunifu kubuni begi maalum la umemejua linalowawezesha watoto kujisomea nyakati za usiku.

Wabunifu hao waliopo mkoani Mwanza wamebuni mradi uliopewa jina la ‘Soma Bag. ambao unalenga kukata kiu ya wanafunzi ambao wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya kujisomea nyakati za usiku hatua ambayo huwalazimu kutumia kibatari ama taa za chemli ili kupata mwanga.

Kusoma kwa kwa kutumia kibatari ama taa za chemli hutajwa kuwa ni kikwazo katika ufaulu wa wanafunzi kutokana na kuhitaji kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kununulia mafuta ya taa ambayo hutumika kuwashia nishati hiyo.

Innocent James ambaye ni muasisi wa mradi huo akihojiwa na mwandishi Evarist Mapesa wa redio SAUT FM iliyoko mkoani Mwanza Tanzania,, anasema wazo lilianza pale walipokuwa wakijaribu kutatua changamoto ya wanafunzi kujifunza wenyewe kwa kuwajengea tabia ya kujisomea.

Yeye na wenzake walianzisha maktaba tembezi ambayo ilikuwa ikiwafuata watoto mahali walipo kama mashuleni au uwanjani.

Huduma hiyo ilianza kukuwa, huku wakijiuliza maswali, wanafunzi wangapi wanaitumia huduma hiyo? na inawafaa vipi katika masomo na ufaulu wao?. Walipofanya utafiti wakagundua watoto waliokuwa wakichukua vitabu katika maabara tembezi hawakuvisoma ipasavyo.

Begi la sola lililotengenezwa kwa kutumia taka mali. Kipande cha sola kimeunganishwa na waya inayopokea nishati ya jua na kuingiza katika taa maalumu ambayo usiku hutumika kwa ajili ya kujisomea. Picha | UN News/Evarist Mapesa.

Na miongoni mwa sababu walizozigundua kwa watoto hao kutosoma vitabu walivyokuwa wakivichukua ni kutokuwa na nishati rafiki ya kuwasaidia kujisomea nyakati za usiku.

“Tuligundua kwamba watoto wanapokuwa nyumbani nyakati za usiku wanawasha kibatari ambacho kinatumia mafuta ya taa, na kwa kawaida hakitoi mwanga wa kutosha wa kumvutia kusoma, pili unazalisha moshi ambao kimsingi unaleta kero kwa mtumiaji, na tatu ni gharama kununua mafuta hayo. 

“Hapo ndipo tuliweza kubuni mabegi haya ili kuwasaidia wanafunzi kujisomea nyakati za usiku”, anasema James.

Kwa sasa James na wenzake wana kiwanda cha kutengeneza bidhaa hiyo, kwa siku huzalisha zaidi ya mabegi 100 ambayo huyauza na kuyasambaza katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania.

Jinsi yanavyotengenezwa

Begi hili ambalo hutengenezwa kwa taka mali ikiwemo mifuko ya saluji ambayo hukusanywa kutoka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kisha husafishwa na kuunganisha kipande cha kifaa kinachonasa nishati ya jua (Sola).

Nishati hiyo hukusanywa kwa siku nzima kwani kipande hicho cha umemejua kinakuwa kimeshonwa nyuma ya begi la mwanafunzi, ndani ya begi kunakuwa na taa ya kutoa nishati ya mwanga (bulb) ambayo inakuwa imeunganishwa na waya unaotoka kwenye sola.


Soma zaidi:


Hivyo nyakati za usiku mwanafunzi anapokuwa anataka kusoma, huchomoa taa hiyo na kuiweka sehemu yeyote anayohisi akiiweka taa hiyo itampa mwanga mzuri wa kumuwezesha yeye kusoma vizuri bila usumbufu wowote.

Ujio wa mabegi hayo, yameanza kuleta matokeo chanya katika ufaulu wa darasani.

Janeth Andrea ni mwanafunzi wa darasa la sita katika moja ya shule mkoani Mwanza, anakiri kuwa uwepo wa mabegi hayo umemsaidia katika usomaji hasa nyakati za usiku.

Mwanafunzi mwingine Jackline Andrea anasema “taa hunisaidia usiku, zamani nilikuwa nasoma na taa ya nyumbani, ilikuwa na mwanga mdogo lakini taa hii ya begi ina mwanga mkali.”

Andrea Busabusa ni mzazi wa Watoto wawili ambao wanatumia mabegi hayo yanayokusanya mwanga wa jua, anasema yamewasaidia watoto wake hasa katika maendeleo ya ufaulu shuleni.

“Maendeleo ni mazuri, kwa watoto wangu wawili mmoja anakuwa wa nne mwingine wa tano, ni kiwango kizuri kabisa kwa sababu akiwa shuleni anaona kwa macho kwa kutumia mwanga wa jua, akirudi nyumbani anasoma kwa kutumia mwanga wa sola muda wowote anaoutaka,” anasema Busanusa.

Taa hizi iwapo zitasambazwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania zitawasaidia wanafunzi hususani wale waishio maeneo ya vijijini kujisomea vizuri nyakati za usiku na hatimaye kutimiza malengo yao.

Enable Notifications OK No thanks