Jinsi ya kutaja kiwango sahihi cha mshahara wakati wa ‘interview’ ya kazi

April 22, 2021 9:17 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kawaida kwenye usaili wa kazi kuulizwa kiwango cha mshahara cha kulipwa.
  • Wakati wa kutaja kiasi ukitakacho, zingatia ujuzi wako, hali ya kampuni na uhalisia wa fani yako.
  • Inashauriwa kufanya utafiti ili ufahamu waliopo katika fani yako wanalipwa kiasi gani.

Dar es Salaam. Kwa watafuta ajira wengi wanaofikia ngazi ya usaili wa kupata ajira, swali linalouliza kiasi cha mshahara ambacho mtu anahitaji kulipwa baada ya kuajiriwa ni mtego ambao ukilijibu vizuri umepata kazi na ukikosea, kazi hauna tena.

Hali hiyo huwaacha vijana wengi katika sintofahamu ya jinsi ya kulijibu ili waipate kazi ambayo ipo mbele yao. 

Hata hivyo, baadhi yao hukosea kujibu na wengine wanaobahatika, wanalijibu vizuri na kupokea simu ya wito wa kuanza ajira hizo.

Mkurugenzi wa kampuni ya kidijitali inayojihusisha na ufundi pamoja na ujenzi ya Toolboksi, Julius Mbungo amesema lengo la waajiri kuuliza swali hilo ni kufahamu kama bajeti ya kampuni inaweza kumlipa kiasi alichotaja.

Mbungo amesema wakati mwingine waajiri wanafanya hivyo kujua malipo ya nafasi hiyo kwa sehemu zingine ili wafanye maamuzi.

“Mkimuuliza hivyo mnataka kujua anaendana na bajeti  ya mshahara uliopangwa au yuko chini au juu ya matarajio. Kama yupo juu, juu yake ni kubwa sana kiasi cha kuzungumza akashuka chini katika sehemu mnayotaka au kama yuko chini sana na ana sifa mnazozihitaji basi kampuni mnufaike,” amesema Mbungo.

Haupaswi kutaja fedha ya juu sana kuliko uhalisia wala pesa ya chini sana ili upate ajira. Picha| Freepik.com

Jibu sahihi la swali hilo ni lipi? Kabla haujajibu swali hilo hakikisha umetafiti na kuwa na uhakika wa masuala yafuatayo:

Miaka ya uzoefu wako

Kuna kipindi nilimsikia mwajiri mmoja akisema, “yaani hajawahi kufanya kazi popote, huna uzoefu wowote tangu amalize chuo lakini anataka milioni na nusu?” na hapo ilikuwa wazi kuwa yeyote aliyekuwa akizungumziwa hapo, ajira hiyo haikuwa yake tena.

Baaadhi hushindwa kuelewa kuwa mshahara wao unatakiwa kuendana na miaka yao ya uzoefu na ujuzi wa kazi ambao wanaenda nao kwenye kampuni husika.

Afisa Mwajiri kutoka kampuni ya CV People, Noemi Mseven ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz)  kuwa kwa mtu ambaye ndio kwanza anaanza kazi, kulingana na kazi anayoomba mara nyingi mshahara unaweza kuanzia Sh600,000 hadi Sh800,000.

“Kwa ambaye ana uzoefu wa miaka miwili na zaidi, anaweza kuanzia Sh1.5 milioni na kuendelea hata hivyo inategemeana na hiyo kazi anayofanyiwa usahili,” amesema afisa huyo ambaye pia hutoa mafunzo kwa vijana wanaosaka fursa za ajira. 


Soma zaidi:


Uhalisia wa fani hiyo na kampuni

Mtafuta ajira unatakiwa kufahamu kwa undani kampuni ambayo unaenda kufanyiwa usaili. Mfano kwa kampuni ambazo zinaanza, mshahara huwa wa wastani hivyo kutaja pesa kubwa kwa kampuni ambayo ndiyo inaanza kujitambulisha sokoni inaweza isiwe kitu kizuri.

Inakuhitaji ufanye uchunguzi kufahamu soko la nafasi hiyo na kiwango cha makadirio ya malipo. Pia unahitaji kufahamu mshahara huo unaambatana na manufaa gani mengine mfano bima ya afya, usafiri, nyumba ya kuishi na kadhalika. 

Hivyo haupaswi kutaja fedha ya juu sana kuliko uhalisia wala pesa ya chini sana ili upate ajira. Unatakiwa kusema fedha ambayo itakimu mahitaji yako na kukuruhusu kufanya kazi pasi na changamoto zingine za kimaisha.

Ni kawaida kwenye usaili wa kazi kuulizwa kiwango cha mshahara cha kulipwa lakini unatakiwa kuwa makini. Picha| Mtandao.

Ujuzi, malengo na ukubwa wa kazi

Kujibu swali hilo pia unahitaji kufahamu ujuzi ulionao, malengo yako ya kuomba kazi hiyo na pia ukubwa wa kazi ambayo ipo mbele yako.

Mfano kwa kazi ambayo itakuhitaji kuifanya kwa uzito ikiwemo kutumia muda mwingi, nguvu nyingi na utashi, mshahara wake haupaswi kuwa lele mama kulingana na uwezo wako kiujuzi na manufaa utakayoongeza katika kampuni husika.

Mtaalamu wa mawasiliano na Mkurugenzi Mtendaji wa Crimson Communications Ltd, Myoma Kapya amesema kujibu swali hilo inahitaji uweke ujuzi wako, na ukubwa wa kazi katika mizani huku ukijua thamani ya taaluma hiyo.

“Inategemeana na kampuni unayoenda na thamani yako. Kama unaanza kazi, Sh400,000 au Sh 500,000 inatosha kuanzia lakini kama una ujuzi wa miaka miwili, milioni moja sio haba. Unaenda kidogo kidogo,” amesema Myoma aliye na miaka 11 katika fani ya mawasiliano. 

Wadau mbalimbali wameimbia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa ni kweli swali hilo huweza kukupatia kazi au kukukosesha fursa hiyo. 

Hata hivyo, inashauriwa kuwapatia waajiri nafasi ya kusema kiwango ambacho wanaweza kulipa na kisha mkaanza kujadiliana kuona kama kinawezekana miongoni mwenu wote.

Mara zote, weka wazi kuwa hiyo pesa unayoitaja ni baada au kabla ya makato ya kodi na mambo mengine kama bima. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW