Emanuel Feruz: Mtaalam wa Tehama aliyegeukia ujasirimali wa upigaji picha

November 20, 2018 8:38 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link

Safari ya upigaji picha inahitaji uvumilivu na ubunifu ili kufikia viwango vitakavyowavuta wateja wengi zaidi. Picha| K15Photos.


  • Aliacha kazi yenye maslahi mazuri ikiwemo kufundisha vyuo mbalimbali na kujikita katika upigaji picha akiamini ni shughuli inayomfaa na kumuendeleza kimaisha.
  • Anatamani siku moja aweze kuhifadhi tamaduni mbalimbali za nchi katika mfumo wa picha kwa ajili ya vizazi vijavyo.
  • Ndoto yake ni kuanzisha kampuni itakayotoa ajira kwa vijana wenye malengo ya kuingia katika sekta ya upigaji picha.

Dar es Salaam. Wasomi wengi wamekuwa na kasumba ya kuchagua kazi za kufanya kwasababu tu ya kufikiria watu watawaonaje ikiwa watafanya kazi ambazo hawakusomea au zisizo na hadhi katika jamii.

Lakini kwa Emmanuel Feruzi (37), mtaalam wa masuala ya teknolojia na mawasiliano (Tehama) ameachana na fikra hizo na kuamua kufanya shughuli ya kupiga picha ambayo anaamini ni sahihi kwasababu inaendana na ndoto na matamanio aliyokuwa nayo tangu akiwa mdogo. 

Alipata shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika ya Kusini na baadaye akajiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ikichukua shahada ya umahiri lakini aliishia njiani na kuamua kufanya shughuli nyingine za ujasiriamali.  

Katika safari ya kuyatafuta mafanikio ya kweli kupitia ujasiriamali wa kupiga picha, haikuwa rahisi kwa Feruzi kusimama kwasababu ilimchukua muda mrefu kukubalika katika jamii ikizingatiwa alikuwa amesoma vizuri  na kutegemewa na ndugu zake, lakini ajira haikuwa kipaumbele chake.

Nukta imekuletea mahojiano iliyofanya na Feruzi ambaye kwasasa anafanya shughuli zake katika Jiji la Dar es Salaam. Mazungumzo haya yanaweza kuwasaidia vijana wasomi wenye vipaji au ubunifu ambao wangependa kuutumia kuboresha maisha  kupitia shughuli mbalimbali za kujiajiri.

Nukta: Safari yako ilianzia wapi?

Emanuel: Nilipomaliza masomo yangu ya IT nikafanya kazi kwenye kampuni mbili baada ya hapo nikaenda kufanya kazi kampuni ya mawasiliano ya Tigo kwa mwaka mmoja, baada ya hapo nikapata kazi nchini Norway ila sikukaa sana nikarudi nyumbani.

Nukta: Ulivyorudi nini kilitokea?

Emanuel: Nikaanza kufundisha vyuo mbalimbali kama Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Takwimu (EASTC) na UDOM (Chuo Kikuu cha Dodoma) kidogo halafu nikaacha na kujiunga na rafiki zangu wanne kufungua kampuni ya masuala ya teknolojia lakini baadae nilijitoa.

Nukta: Mmh! safari ilikuwa ndefu ila tunakujua kwa kupiga picha, hii imetoka wapi?

Emanuel: Nilipokuwa sikukuta picha zangu nyingi za utoto, hivyo nilipobahatika kupata mtoto wangu wa kwanza nikasema nitatumia nafasi hii kumtengenezea kumbukumbu nyingi za utotoni. Hivyo nikaanza kumpiga mtoto picha na kuwatumia ndugu, jamaa na marafiki.

“Wakaanza kuzipenda na wakawa wananikaribisha katika sherehe za ‘birthday’ ili niwe nachukua picha za matukio hayo. Hapo ndipo nikaona naweza kufanya hivi kujipatia kipato na kufanya ninachokipenda kwa wakati mmoja.”

Nukta: Familia ilichukuliaje ulipoamua kuacha kila kitu na kuanza kuwa mpiga picha?

Emanuel: Wengi waliona nimepotea lakini nashukuru wazazi wangu walikuwa wanajali kipato zaidi kuliko kazi ninayofanya, hivyo hawakuwa na shida na mimi kuacha kazi.

Nukta: Vipi lakini hukupata changamoto zozote ulipoingia rasmi katika upigaji picha.

Emanuel: Kwa kweli mtaji ilikuwa ‘issue’ (changamoto) kwasababu vifaa vya kamera ni bei, niliuza kila kitu ili ninunue vifaa vya kamera.

Feruzi amevutiwa zaidi katika kazi ya kupiga picha kwasababu ya kuwa na kumbukumbu nyingi za watoto wake. Picha| K15 photos.

Nukta: Vipi lakini soko lipoje?

Emanuel: Soko sio baya ila wapiga picha ni wengi sana, ambapo wengine wanaweza kuona ni changamoto ila kwangu ni fursa maana wakichaji cha juu na mimi inanisaidia kuongeza.

Nukta: Hongera kwa kufikiria kibiashara zaidi vipi lakini watu gani maarufu ambao ulishawahi kuwapiga picha?

Emanuel: Nimempiga mwigizaji  Lulu (Elizabeth Michael), Mhe Jokate  Mwegelo (Mkuu wa Wilaya ya KIsarawe), Angel Benard (Mwimbaji wa nyimbo za injili) na Nasreem Kareem (Mwanamitindo).

Nukta: Kwanini uliamua kuwatumia watu picha zao kwa kutumia kiunganishi inayompeleka mtu kwenye sehemu ulipomhifadhia picha?

Emanuel: Niliamua kufanya hivyo kama mtaalam wa Tehama lazima nionyeshe utofauti kidogo pia ni njia ya kutunza picha kwasababu flash inaweza potea na mtu akapoteza kumbukumbu zake, ila link unahifadhi tu.

Nukta: Ni mafanikio gani umeyapata mpaka sasa?

Emanuel: Mafanikio ya kwanza ni kujuana na watu wengi, vingine nimeweza kuajiri vijana wawili ambao tunashirikiana katika kazi na kikubwa zaidi ni kufanya kitu ninachokipenda.

Nukta: Changamoto gani unayokumbana nayo katika kazi yako ya sasa?

Emanuel: Changamoto kubwa ni vifaa vingi havipatikani nchini kirahisi, wateja wanadharau sana kazi yetu, huwa hawaoni umuhimu wetu bila kujua sisi ndio tunaoweka kumbukumbu kwa muda mrefu. Nyingine ni vijana ukiwafundisha tu wakishajua wanaondoka.


Zinazohusiana: 


Nukta: Kwanini wasiwaze mipango ya biashara na waanze kufanya biashara?

Emanuel: Mfumo wa elimu ya biashara unawachelewesha wajasiriamali wengi kwasababu watu wanaogopa kuanza na walichonacho, vilevile mifumo ya kodi kwa wafanyabiashara ni changamoto, serikali ingewapa nafasi wajasiriamali na kuwaandalia mfumo mzuri wa ulipaji kodi.

Nukta: Unajiona wapi miaka kumi ijayo?

Emanuel: Najiona nitakuwa mzee (anacheka), nitakuwa nimekuwa mimi na kampuni pia itakuwa inajitegemea yenyewe.

Nukta: Unatamani kuona nini kitokee kwenye fani uliyochukua.

Emanuel: Natamani siku moja nifanye kazi na wizara mbalimbali katika kuhifadhi tamaduni zetu kupitia video, ili vizazi vijavyo waweze kujua tulipotoka. Na ningependa kuona serikali inafanya kazi na wapiga picha mbalimbali ili kuweza kuhifadhi vitu vingi vilivyopo nchini. 

Nukta: Una ushauri gani kwa vijana wanaopenda kuwa wajasiriamali?

Emanuel: Kama wanapenda ujasiriamali waanze leo, kama unataka kupiga picha nunua kamera anza, usiwaze kwanza mambo ya mipango ya biashara.

Enable Notifications OK No thanks