Vitu vinavyoongeza nafasi yako ya kupata ajira
- Ni ujuzi ambao utakuongezea nafasi ya kubaki kwenye orodha baada ya usahili wako.
- Waajiri waweka wazi kuwa siku hizi wanaenda mbali ya uwezo wako wa darasani.
- Vijana wasisitizwa kuendelea kujisasisha kwa teknolojia na ujuzi wa vitu.
Dar es Salaam. Swali kubwa ambalo waajiri hujiuliza pale wanapopata maombi ya kazi kutoka kwa vijana, ni kitu gani ambacho utaongeza kwenye biashara au kampuni.
Ni katika hatua hiyo ambayo waajiri huanza kuangalia sifa za nyongeza walizonazo watu walioomba kazi hiyo.
Mbali na mambo mengine ambayo huangaliwa ikiwemo sehemu ulizowahi kufanya kazi, taaluma yako, kuna mambo mengine ya ujuzi ambayo huangaliwa ili kumtofautisha mtu mmoja na mwingine.
Mfano, endapo waombaji wote wamefanya vyema kitaaluma, wamefikia sifa zinazohitajika ikiwemo uzoefu na mengineyo, waajiri huanza kuangalia mambo mengine kulingana na ajira inayotolewa.
Baadhi ya vitu ambavyo vinaweza kuongezea nafasi yako ya kupata ajira endapo vyeti vyako, uzoefu na uwezo wako wa kujipambanua kwenye usaili vimepata vema ni hivi.
Unahitaji ujuzi wa kujiongeza. Picha| Medium.
Ufahamu wa takwimu
Kupitia takwimu sahihi, Makampuni yanaweza kutabiri namna hali ya biashara itakavyokuwa katika majira yajayo na kujiandaa kikamilifu kuikabili.
Afisa miradi ya biashara (B2B Project Manager) kutoka kampuni ya ITM Tanzania, Michael Mwangoka amesema makampuni mbalimbali yanahitaji watu walio na ufahamu wa masuala ya takwimu ili kutatua changamoto.
Baadhi ya makampuni yanayoelewa hali za biashara (business trends) na mabadiliko ya mahitaji kwa wateja, yana nafasi kubwa ya kukabili janga lolote linaloweza kukumba biashara zao kuliko mengine na hivyo uelewa wa takwimu kwa vijana ni nyongeza ya ujuzi.
“Watu wenye ujuzi wa uchambuzi wa takwimu na kuzitolea maamuzi sahihi, watakuwa na mafanikio katika soko la ajira,” amesema Mwangoka.
Fikra tunduizi (Critical thinking)
Unahitaji zaidi ya cheti chako cha akademia kuwa na mchango kwenye kampuni yoyote. Unahitaji nguvu ya kazi na uwezo wa kufikiria nje ya boksi ili kuibua ufumbuzi wa changamoto na masuala yanayoendelea kwenye kampuni.
Mwangoka amesema watu wenye uwezo wa kuchambua taarifa kwa kina kutoka vyanzo mbalimbali ili kutambua ipi ni sahihi, watakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa kwenye soko la ajira.
“Sio kila taarifa inaweza kufanyiwa kazi katika biashara, kwa hiyo, makampuni yataangalia ni nani anayeweza kuchambua taarifa kwa kina ili kujua ipi ihusike kwenye kufanya maamuzi na ipi ipuuzwe bila kuathiri utendaji wa kampuni kibiashara,” amesema Mwangoka.
Ujuzi wa kimtandao na ubunifu wa programu (CODING)
Masuala kama masoko ya kimtandao (Digital marketing), ujuzi wa kutengeneza na kusimamia tovuti (web development), yana maana na masoko zaidi kwa sasa.
Karibu makampuni yote hivi sasa yako mtandaoni na yanatafuta watu sahihi wa kuleta matokeo chanya na faida kwenye mitandao hiyo ikiwemo ya kijamii na tovuti rasmi hivyo ni wewe tu kujiweka vizuri.
Kwakuwa kampuni zinahamishia huduma mtandaoni, unahitaji kufahamu kutumia mitandao hiyo kiueledi. Picha| Alternative Africa.
Ujuzi wa akili ya hisia (Emotional Intelligence)
Huu ni uwezo wa kufahamu, kuonesha na kusimamia hisia binafsi na kuzitambua za wengine. Kwenye mazingira ambayo watu hawaoni usalama juu ya kazi zao na baadaye ya biashara zao, ni muhimu kujiunganisha nao kupitia akili ya hisia.
Endapo hilo halitozingatiwa, watu wanaweza kuzalisha kinyume na matarajio kwa sababu tu, wanajihisi kutosikilizwa, kuheshimiwa wala kuangaliwa.
“Watu wenye ujuzi wa akili ya hisia (Emotional Intelligence) wana nafasi kubwa ya kupata mafaniko wanapoomba kazi, amesema Mwangoka.
Sifa zingine ni pamoja na ujuzi wa uongozi, ubunifu na uwezo wa kufanya kazi kutokana na mazingira utakayopangiwa (flexibility).
“Makampuni mengi kwa sasa yameondokana na utamaduni wa kuajiri tu kwa kuzingatia vyeti na mafanikio mengine ya kitaaluma. Ni muhimu kuendelea kujiandaa na mazingira yoyote kupitia mitandao na intaneti katika kujielimisha,” ameshauri Mwangoka.
Ujuzi wa kimawasiliano na kufanya kazi na watu
Katika ofisi utakayoenda, lazima ukute watu ambao wanaendelea na shughuli zao. Utaweza kufanya nao kazi? Kuvumilia au kurekebisha kwa upole madhaifu yao huku ukifuata haki zao? Hilo ni jambo ambalo linaangaliwa pia kwani tabia yako ni uwakilishai wa kampuni uwapo nje ya ofisi.
Afisa mwajiri kutoka kampuni ya CV People, inayounganisha wajiri na wafanyakazi, Noemi Museveni amesema waajiri huangalia uwezo wa mtu kuwasiliana ili ikawe rahisi kwa yeye kutambua wapi atapata msaada pale akianza kazi yake.
Mawasiliano hayo ni ya kuongea na kuandika pamoja na kusikiliza.
Unapoajiliwa, hauendi kufanya kazi peke yako hivyo unahitaji ujuzi wa kimawasiliano. Picha| NASPA.
Kujituma
Hakuna mwajiri anayetafuta mtu ambaye atahitaji kuambiwa kila kitu anachopaswa kufanya. Waajiri wanaangalia mtu ambaye ana uwezo wa kujiongeza kujua kuwa hili ni jukumu langu, nitalifanyia kazi kwa muda huu na litaisha siku hii.
Museveni amesema unahitaji kuwa na ujuzi wa kufanya kazi hata katika mazingira magumu ikiwepo presha ya mwajiri na kazi kubwa zinazotakiwa kutatuliwa kwa muda mfupi.
Mbali na hayo yote, Museveni amesema utanashati wako pia utaamua kama kazi hiyo utaipata au hautoipata. Kwa baadhi ya waajiri, muonekano wako wa mara ya kwanza ni kitu kikubwa sana kwani zipo kazi ambazo atakuhitaji ukamwakilishe na endapo muonekano wako hauwezi kuonyesha kuwa unafaa kwa kazi hiyo, huenda kazi hiyo isiwe yako.
Museveni amesema muonekano ni kuanzia jinsi unaongea na kujipambanua kwa mavazi, unadhifu wako na unavyoweza kujibishana na watu na kubaki na uhalisia wako.
Latest
