Jamii iwajibike kulinda watoto dhidi ya ukatili

August 9, 2022 1:17 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Stella Mbura akimkabidhi sare za shule zilizotolewa na shirika la MOCSO mwanafunzi wa Shule ya Msingi Gedeli iliyopo Kata ya Nyakato wilayani Ilemela mkoani Mwanza. Picha | Mariam John.


  • Hiyo itasaidia kujenga jamii yenye amani na maadili.

Mwanza. Jamii imetakiwa kuwa mstari wa mbele katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto ili kuwa na jamii yenye amani.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri  ya Wilaya ya Ilemela, Stella Mbura amesema kila mmoja awe balozi wa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo viovu.

Amesema jamii salama inawezekana iwapo vitendo vya ukatili wa kijinsia vitapigwa vita na kila mmoja atasimama kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili.

“Serikali inawajali na itaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuwalinda na kuzuia vitendo vya ukatili kwa watoto, na hili litawezeka iwapo kila mmojawetu atakuwa balozi wa kupiga vita vitendo hivyo,” amesema Mbura.

Mbura alikuwa akizungumza leo Agosti 8, 2022 kwenye hafla fupi ya kukabidhi sare za shule kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, msada uliotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Mosco. 

Mosco imekabidhi sare za shule ikiwemo  mabegi, daftari na kalamu kwa watoto 315 ambapo lengo ni kuwasaidia watoto waweze kupenda  shule na kupunguza utoro.

Afisa Msimamizi Mshauri wa watoto wa shirika hilo, Amos Jackson amesema vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi.

“Lengo  ni kuwafikia watoto hao pamoja na  kuisaidia jamii hasa watoto waliopo katika mazingira hatarishi na makundi maalum  kwa kupunguza kero na changamoto zinazokwamisha kufikia ndoto zao hasa za kielimu,” ameeleza Amos.

Amos ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa  taasisi na mashirika mengine kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na changamoto zinazokabili jamii hasa watoto.

Mratibu wa afya shuleni kutoka Halmashauri ya  Manispaa ya Ilemela, Finias Nyaganyi  amesema kitendo kilichofanywa na shirika hilo kitasaidia kupunguza kero kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Nyakato ‘A’ Lucia Bugama amesema sare hizo zimepunguza mzigo kwa wazazi wao kwa sababu mara nyingi walikuwa wanakosa kuhudhuria masomo kutokana na kukosa sare.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW