Ilemela waimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia

June 2, 2022 2:19 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Waandaa kampeni maalum ya kutoa elimu.
  • Jamii yatakiwa kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo hivyo.

Mwanza. Serikali wilayani Ilemela imesema haitafumbia macho vitendo ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto unaoendelea wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala ametoa kauli hiyo leo Juni 2, 2022 wakati akifungua kikao cha wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia kilichowakutanisha watendaji kata, walimu wa shule ya msingi na maofisa maendeleo ya jamii, polisi kata na wadau wengine kilichoandaliwa na  shirika lisilo la kiserikali la Wadada Solution.

Mkuu huyo wa Wilaya amekiri kushamiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia wilayani humo ikiwemo ukatili kwa wanawake, ulawiti kwa wanafunzi wa shule za msingi, mimba za utotoni na wanafunzi kuacha shule.

Bila kutaja takwimu mkuu huyo wa wilaya amesema vitendo hivyo vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara ofisini kwake na ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo na kuwataka wadau hao kuhakikisha wanakuja na njia za kutokomeza vitendo hivyo.

“Sote kwa pamoja tushiriki kuibua na kutatua changamoto zinazotokea mitaani zikiwemo hizo za ulawiti kwa watoto wadogo, tuvunje ukimya na tusiache mambo yanayoendelea kwenye maeneo yetu na sisi tukakaa kimya, tunaamini mkiwa mabalozi wa kusema haya tutakuwa na jamii iliyo salama na tunatamani kuona vitendo vya kikatili vinavyoendelea hivi sasa vikimalizika,” amesema Masala.

Awali Afisa Mradi wa Kijana Paza Sauti Chukua Hatua kutoka Wadada Solution , Elihaika Mgenyi amesema utafiti mdogo uliofanywa na shirika hilo ulibaini kuwa maeneo ambayo uvuvi unafanyika unaongoza kwa matukio ya kikatili ambapo wavuvi huwalaghai wanafunzi wanaotumia muda mrefu kwenda shule.

“Kutokana na changamoto hizo kama shirika tuliona ipo haja ya kufika kwenye maeneo hayo ya vijijini na pembezoni mwa ziwa ambako matukio mengi ya ukatili wa kijinsia yanafanyika lengo ni kupaza sauti kuwalinda vijana dhidi ya vitendo hivyo vya kikatili,” amesema Mgenyi.

Mradi huo ambao umefadhiliwa na taasisi ya Terredes Hommes Schweiz unatekelezwa katika kata tano zilizoko pembezoni mwa Ziwa Victoria ambazo ni Kitangiri, Sangabuye, Shibula, Bugogwa na Kayenze lengo kuu ni kupunguza matukio ya ukatili.

“Sisi kama jamii tuna wajibu na  kwamba tunapaswa kutoa taarifa sahihi kuhusiana na matukio ya ukatili ili kuhakikisha tunalinda ulinzi na usalama wa mtoto kuanzia awapo nyumbani na si kuwaachia jukumu hilo walimu pekee,” amesema Mgenyi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wadada Solution, Lucy John amesema mkakati uliopo ni kuanza kukutana na wazazi na jamii kwa ujumla kuwapa elimu ya ulinzi wa mtoto ili kupunguza matukio ya ukatili.

Amesema hivi sasa wanatoa elimu hiyo kupitia midahalo mbalimbali shuleni na kuishauri jamii ambayo ndiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuwanyanyasa watoto wanaoishi nao nyumbani.

“Kitendo cha mzazi kumlawiti mtoto wake au kuchukua bastora na kumuua mwenzake ni vitendo ambavyo vinatakiwa kukemewa kwenye jamii, hivyo elimu inahitajika dhidi ya mapambano hayo,” amesema John.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW