Mbio za usiku kutikisa jiji la Mwanza kwa mara ya kwanza
- Zitafanyika usiku wa Julai 23, 2022.
- Lengo ni kuhamasisha jamii kushiriki Sensa ya Watu na Makazi.
- Pia kupinga ukatili wa kijinsia.
Mwanza. Wakimbiaji zaidi ya 600 wanatarajia kushiriki mbio maalum za riadha zitakazofanyika usiku wa Julai 23 jijini Mwanza kwa lengo la kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia na kuhamasisha jamii kushiriki Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti mwaka huu.
Mratibu wa mbio hizo (Rock City Runners) Magreth Mushi, akizungumza kwenye uzinduzi wa dirisha la usajili wa watu wanaotaka kukimbia mbio hizo Juni 24, 2022 amesema mbio hizo zitasaidia katika kupunguza matukio ya ukatili ambayo hivi sasa yameshamiri.
“Lengo ni kuisaidia jamii kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia lakini pia kuihamasiha jamii kujitokeza kuhesababiwa,” amesema Mushi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MWAA), Julius Kambarage amesema kumekuwepo na matukio mengi ya ukatili akiwemo ndugu wa karibu kuwafanyia watoto wao ukatili.
Amesema umefika wakati ambapo ndugu hawezi kumwamini ndugu yake mwingine kulala na watoto wake akihofia kulawitiwa.
“Binadamu tumebadilika ndugu haoni aibu kumlawiti mtoto wa ndugu yake wa miaka minne, niombe pamoja na dhima kuu ya mbio hizi kupunguza matukio hayo lakini pia iwepo mikakati maalum itakayosaidia kupunguza matukio hayo,” amesema Kambarage.
Mwenyekiti huyo pia ameiomba jamii kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pale wanaposhuhudia vitendo hivyo wakifanyiwa watoto ili kupunguza matukio hayo.
Mbio hizo zilizoandaliwa na Club ya wakimbiaji ya Rock City Runners ni za kwanza kukimbiwa usiku na zitajumuisha mbio za kilomita saba na 15 kwa watu wote.
Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kali amesema zitasaidia kuutangaza Mkoa wa Mwanza kiutalii na kukuza uchumi.
“Hizi ni mbio za kwanza kufanyika usiku, tumezea mbio za alfajiri saa 12 lakini hizi zitakimbiwa usiku wakati ambapo hakuna vurugu ya magari, hakuna jua kali hivyo nina imani idadi kubwa ya watu watajitokeza kumbia,” amesema Kali.
Ameitaka jamii kubadilika kuacha matukio ya kikatili.