IFC kuipiga jeki sekta binafsi Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan akutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji  wa International Finance Cooperation (IFC) Makhtar Sop Diop Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo Februari 3, 2022. Picha| Ikulu.
- Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) laahidi kushirikiana na sekta binafsi
- Wamachinga kufaidika na usaidizi wa shirika hilo.
- Rais Samia aishukuru IFC kwa kuchangia kuinua uchumi.Â
Dar es Salaam. Huenda sekta binafsi Tanzania ikapata msukumo mpya baada ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) kuonyesha nia ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga kuinuka kiuchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa IFC, Makhtar Sop Diop amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na sekta binafsi nchini Tanzania, pamoja na kuangalia namna ambayo wanaweza kuwasaidia wamachinga na kuwawezesha kiuchumi wanawake wanaofanya kazi katika sekta binafsi.
Diop amesema eneo jingine ambalo IFC ingependa kushirikiana na Tanzania ni kuimarisha sekta ya usafiri nchini hususan usafiri wa majini, kuwajengea uwezo wawekezaji katika miradi mikubwa ya ujenzi wa makazi pamoja na uwekezaji zaidi katika elimu na afya.
Dipo ametoa ahadi hizo leo Februari 3, 2022 alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Diop amempongeza Rais Samia kwa mafanikio aliyoyapata kutokana na utendaji mzuri wa kazi katika kuwaletea maendeleo Watanzania, ikiwa ni pamoja na kukua kwa uchumi na kusimamia mfumuko wa bei nchini.
IFC NI mwanachama wa Benki ya Dunia. Ndiyo taasisi kubwa zaidi ya maendeleo ya kimataifa inayolenga sekta ya binafsi katika masoko yanayoibukia.
Inafanya kazi katika zaidi ya nchi 100, kwa kutumia mitaji, utaalamu na ushawishi kuunda masoko na fursa katika nchi zinazoendelea.Â
Soma zaidi:
- BOT: Marufuku kurusha hovyo noti
- BOT yashusha tena riba kwa benki za biashara Tanzania
- Tabasamu: Mikopo kwa sekta binafsi yaongezeka Tanzania
Katika mwaka wa fedha wa 2021, IFC iliwekeza Dola za Marekani bilioni 31.5 (Sh72.8 trilioni) kwa makampuni binafsi na taasisi za kifedha katika nchi zinazoendelea, ikitumia uwezo wa sekta ya binafsi kumaliza umaskini uliokithiri na kuimarisha ustawi wa pamoja wa wananchi na uchumi.
Rais Samia amemshukuru Diop na ujumbe wake kwa kumtembelea na amewapongeza kwa kuendelea kuunga mkono sekta binafsi na anatarajia kuwa wataendelea kuiunga mkono zaidi sekta hiyo.
Aidha, ameipongeza IFC kwa ushirikiano mkubwa inayoutoa kwa Tanzania katika kuunga mkono jitihada zake za maendeleo na kuihakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na shirika hilo katika kutekeleza majukumu yake hapa nchini.
Pamoja na mambo mengine amemueleza Diop hatua mbalimbali zilizofikiwa na Serikali katika kuimarisha miundombinu ya elimu, afya, barabara vijijini, usimamizi wa reli ya kisasa (SGR) pamoja na kutumia fursa za uchumi wa bluu.
Latest
