BoT yashusha tena riba kwa benki za biashara Tanzania

Nuzulack Dausen 0355Hrs   Agosti 25, 2018 Biashara
  • Waraka wa BoT unaeleza kuwa riba hiyo ambayo hutumika kuzikopesha benki za biashara imeshuka hadi asilimia saba kutoka asilimia tisa ya awali.
  • Benki hiyo yasema riba hiyo mpya itaanza kutumika Agosti 27, 2018.
  • Wataalamu waeleza kuwa hatua hiyo italeta ahueni kwa benki za biashara nchini ambazo zinazidi kujiimarisha baada ya misukosuko ya kifedha iliyotokea ndani ya miaka miwili iliyopita.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kutoa ahueni kwa sekta ya benki baada ya kushusha tena riba ambayo huitumia kuzikopesha benki za biashara nchini (discount rate) kutoka asilimia tisa iliyokuwepo awali hadi asilimia saba.

Ahueni hiyo inakuja ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu BoT ipunguze riba hiyo kutoka asilimia 12 iliyokuwepo hapo awali. Kiwango hicho kipya cha riba ya asilimia saba ni cha chini kuwahi kurekodiwa nchini wakati kiwango cha juu kuwahi kutokea ni asilimia 16. 

 Waraka wa BoT kwa benki uliyotolewa Agosti 23 mwaka huu unaeleza kuwa viwango hivyo vipya vitaanza kutumika kuanzia Jumatatu ijayo (Agosti 27, 2018) na vitabaki hadi itakapotangazwa tena. Viwango hivyo, kwa mujibu wa BoT, pia vitatumika kushusha riba inayotozwa na benki za biashara kwa Serikali kupitia ununuzi wa hati fungani,

“Mabadiliko hayo yanasadifu muendelezo wa jitihada za kukuza ukopeshaji kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini,” inaeleza sehemu ya waraka huo wa BoT kwa benki nchini.

“Mapitio hayo ya riba ya ukopeshaji wa benki za biashara pia yamezingatia sera iliyopo ya kifedha na maendeleo ya hivi karibuni katika mapato yatokanayo na ununuzi wa hatifungani za muda wa siku 91 na siku 182.”

Baadhi ya wataalamu wa benki wanaeleza kuwa hatua hiyo ya BoT ni nzuri ikizingatiwa kuwa mazingira ya uendeshaji wa biashara yamebadilika kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Mtaalamu wa masuala ya kibenki Kassim Bwinjo amesema kuwa uamuzi huo wa BoT utatoa ahueni kwa benki za biashara nchini kwa kuongeza ukwasi utakaochochea uendeshaji wa taasisi hizo.


Inayohusiana: NMB yaingiza sokoni huduma tatu za kidijitali kwa mpigo


Miaka miwili iliyopita Sekta ya benki ilikumbwa msukosuko baada ya kuongezeka kwa mikopo chechefu iliyochochea pia kushuka kwa faida kwa baadhi ya benki.

Hali hiyo ilifanya BoT kwa nyakati tofauti kuchukua hatua za kiudhibiti dhidi ya benki ambazo zimeshindwa kujiendesha kutokana matatizo yao ya kifedha kwa ama kuzifunga au kuchukua usimamizi wake.

Hivi karibuni BoT ilitangaza kuchukua usimamizi wa Bank M kuanzia Agosti 2 mwaka huu baada ya kubaini upungufu mkubwa wa ukwasi na kwamba kuendelea kuendesha biashara kwa hali hiyo kuhatarisha usalama

Related Post