Rais Samia ajitwisha deni fursa za zabuni kwa kampuni za vijana, wanawake Tanzania

September 12, 2022 1:52 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mwendelezo wa ahadi za Rais Samia kuboresha mazingira ya biashara kwa kampuni changa za vijana na wanawake maarufu kama startups.
  • Ayashauri mataifa mengine Afrika kuwa na utaratibu huo wa kutoa upendeleo kwa kampuni za vijana, wanawake.
  • Wachambuzi wa uchumi wasema ni jambo jema iwapo Serikali itatekeleza ipasavyo. 

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa atasimamia utoaji fursa za upendeleo kwa kampuni za vijana na wanawake katika manunuzi ya umma ili kuimarisha ushiriki wao katika biashara na ukuzaji uchumi. 

Rais Samia amewaambia washiriki wa Kongamano la Wanawake na Vijana la Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) leo (Septemba 12, 2022)  jijini Dar es Salaam kuwa katika uongozi wake atalisimamia ipasavyo jambo hilo nchini Tanzania ambalo huusisha utengaji wa angalau 30 ya bajeti za taasisi za umma kwa ajili kuyapa fursa makundi maalum.

Kauli hiyo ya mkuu wa nchi inakuja katika kipindi ambacho kumekuwa na malalamiko lukuki miongoni mwa kampuni zinazochipukia (startups) za vijana na wanawake kuwa si rahisi kupata fursa ya kuwa mzabuni wa Serikali. 

Hata wale ambao hubahatika kupata zabuni hizo za Serikali,  baadhi wamekuwa wakilalamikia kucheleweshewa malipo kiasi cha kuathiri mwenendo wa ukuaji wa kampuni hizo changa ambazo hutegemea malipo hayo kama mtaji mkuu wa kuendesha biashara. 

Baadhi ya Washiriki wa kongamano la (AfCFTA) wakisikiliza jambo katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere unapofanyika mkutano huo. Picha|Ikulu.

Katika hotuba yake, Rais Samia amesema utoaji wa upendeleo katika kufanya baadhi ya manunuzi makubwa ya umma kwa kampuni za vijana na wanawake ni miongoni mwa njia zitakazosaidia kuimarisha ushiriki wao katika biashara barani Afrika.

“Sheria yetu inasema asilimia 30 ya manunuzi ya umma wapewe wanawake, sheria zipo lakini utekelezaji wake unalegalega, ninaendelea kuwasimamia kutimiza hilo, ”amesema Rais Samia ikiwa ni muendelezo wa ahadi zake za kuendelea kuimarisha upatikanaji wa fursa kwa vijana. 

Licha ya kuahidi kusimamia sheria hiyo, taasisi nyingi za Serikali ya Rais Samia zimekuwa hazitengi kiwango hicho cha bajeti kinachotakiwa kiasi cha kuzinyima fursa kampuni hizo changa ambazo kwa kawaida huwa ni ngumu kupata zabuni kubwa kutoka katika sekta binafsi. 

Sheria ya Ununuzi wa Umma  iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 inaitaka kila taasisi ya umma kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalumu kama vile wanawake na vijana kuzipatia fursa sawa za kibiashara na kiuchumi kama kampuni kubwa. 


Soma Zaidi 


Hata hivyo, utekelezaji wa sheria hiyo umekuwa wa kusuasua baada ya Ripoti ya Hali  ya Ununuzi Serikalini ya mwaka 2020/21 kuonyesha kuwa ni taasisi mbili tu kati ya 86 zilizofanyiwa tathmini zilifuata matakwa hayo ya sheria. 

“Taasisi tatu zilikuwa zimetenga pungufu ya asilimia 30, wakati taasisi 81 hazikuwa zimetenga chochote,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi ya Umma (PPRA) 

Itakumbukwa Tanzania ni miongoni mwa nchi barani Afrika zinazokabiliwa na wimbi kubwa la vijana wasio na ajira hivyo baadhi yao huanzisha biashara kujiajiri ili kukabiliana na makali ya maisha. 

Wachambuzi wa masuala ya biashara na uchumi wanaeleza kuwa uamuzi wa Rais Samia kusimamia sheria ya kutenga asilimia 30 ya bajeti za taasisi kuzipatia kampuni za vijana na wanawake fursa za zabuni za umma iwapo utatekelezwa ipasavyo utasaidia kuboresha maisha ya Watanzania kwa kiwango kikubwa. 

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Ndahani Mwenda ameiambia Nukta Habari kuwa hatua hiyo itasaidia kiwango kikubwa cha fedha kubaki kwenye mzunguko nchini kwa kuwa asilimia kubwa ya kampuni za kigeni hunufaisha mataifa yao wanapolipwa.

“Kumekuwa na ukiritimba vijana wanapohitaji hizo pesa na kusababisha vijana kukata tamaa, Serikali inahitaji kutazama upande wa pili kama fedha wanazozitenga zinawafikia walengwa kwa kiasi gani,” amesema Mwenda.

Mtaalamu huyo ameshauri uwepo wa utaratibu wa kutoa elimu kwa vijana na wanwake kutambua fursa za fedha na biashara zilizotengwa kwa ajili yao ili waweze kuzitumia kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuimarisha maisha yao.

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jul, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
15 Jul, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
15 Jul, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Kutana na ‘Poultry Plucker’, mashine inayonyonyoa kuku watatu kwa dakika moja

Kutana na ‘Poultry Plucker’, mashine inayonyonyoa kuku watatu kwa dakika moja

Nukta TV

Rais Samia: Kalamu yangu ina hatari, sijawahi kusaini mtu kunyongwa

Rais Samia: Kalamu yangu ina hatari, sijawahi kusaini mtu kunyongwa

Nukta TV

Rais Samia: Matumizi jina Samia, likiwa kila mahali inachosha, tafuteni wengine

Rais Samia: Matumizi jina Samia, likiwa kila mahali inachosha, tafuteni wengine

Nukta TV