Idadi ya ‘startups’ yapaa Tanzania zikikabiliwa na changamoto ya mitaji
- Zimeongezeka kwa asilimia 15 ndani ya mwaka mmoja.
- Mitaji yasalia kuwa changamoto kubwa ya kukua kwa kampuni hizo.
Dar es Salaam. Idadi ya kampuni za teknolojia zinazochipukia (startups) nchini imeongezeka kwa asilimia 15 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita huku zikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mitaji ya kuendesha shughuli zao.
Startups zimekuwa zikitumia teknolojia kutoa suluhu ya changamoto katika sekta mbalimbali ikiwemo afya na elimu ili kurahisisha na kuboresha maisha ya watu.
Ripoti ya hali ya startups Tanzania ya mwaka 2022 iliyotolewa hivi karibuni na Chama Cha Kampuni zinazochipukia Tanzania (TSA) imeeleza kuwa mwaka 2022 kulikuwa na startups 673 zikiongezeka kutoka 587 za mwaka juzi.
Ukuaji huu umechochewa na mambo kadhaa ikiwemo vijana wenye ujuzi wa teknolojia, muamko wa ujasiriamali, kuboreshwa hali ya biashara, na kuongezeka kwa upatikanaji wa mtandao wa intaneti.
Mwaka 2022, Dar es Salaam ndiyo ilikuwa kinara wa kuwa na startups nyingi nchini. Startups zilizopo jijini humo ni asilimia 66.5 ya startups zote za Tanzania.
Dar es Salaam imefuatiwa na Arusha kwa asilimia 8.1, Mbeya (asilimia 4.2) na asilimia 21.9 iliyobaki ni startups zilizopo katika mikoa iliyobaki nchini.
“Utafiti unaonyesha kuwa asilimia 76.6 ya startups zinamilikiwa na wanaume, asilimia 17.2 na wanawake. Pengo la kijinsia linadhihirisha haja ya kuwa na mtawanyiko na ujumuishi katika tasnia ya startups ili kuchochea uvumbuzi na mitazamo mipya,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Soma zaidi:
- Mambo muhimu yatakayozisaidia kampuni zinazochipukia Tanzania kukua
- Startups za Tanzania zilizotamba mwaka 2018
- Starups nne Zanzibar zapenya shindano la Seedstars.
Safari bado ndefu
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukosefu wa mitaji ni moja ya changamoto kubwa inayowakabili waanzilishi wa startups, huku wengi wakihangaika kuvutia uwekezaji kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi.
Matokeo ya ripoti hiyo yanaonyesha kuwa kampuni chipukizi hutegemea zaidi akiba ya mtu binafsi kwa asilimia 36.21 na msaada wa fedha kutoka kwenye familia na marafiki kwa asilimia 32.76.
Washirika wa maendeleo wanafadhili mitaji kwa asilimia 24.39 na fedha za uwezeshaji za Serikali zimechangia asilimia 15.8 ya ufadhili, lakini data zimeonyesha kuwa ni asilimia 6.2 pekee ya walengwa kupata mitaji hiyo.
Pengo kubwa zaidi limeonekana kwenye taasisi za fedha ndani, kama vile benki za biashara, kutoa asilimia 4.88 pekee ya ufadhili, huku kukiwa na uhaba mkubwa wa uwekezaji wa mitaji, hivyo ni asilimia 2.44 tu ya ufadhili imetoka kwa wabia.
Mojawapo ya sababu kuu za pengo hili la ufadhili ni hatari kubwa inayohusishwa na kuwekeza katika kampuni changa hasa zile zilizo katika hatua za mwanzo za maendeleo.
Wawekezaji mara nyingi wanasita kuweka fedha zao kwenye makampuni ambayo bado hayajathibitisha uwezo na faida yao, na matokeo yake, waanzishaji wengi wa Kitanzania wanajikuta wakishindwa kupata mitaji wanayohitaji ili kukuza nakampuni zao.
Sababu nyingine inayochangia uhaba wa fedha unaowakabili wafanyabiashara wa Tanzania ni ukosefu wa tasnia ya mitaji yenye maendeleo nchini.
Ingawa kuna makampuni machache ya mitaji ya ndani yanayofanya kazi nchini Tanzania, tasnia bado ni ndogo na haijaendelea ikilinganishwa na sehemu nyingine za dunia.
Mbali na changamoto hizo, kampuni chipukizi pia zinakabiliwa na vikwazo kadhaa vya udhibiti ambavyo vinaweza kufanya iwe vigumu kupata mitaji imeeleza ripoti hiyo.
Mojawapo ya vikwazo hivyo ni hitaji la wawekezaji wa kigeni kupata kibali kutoka kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kabla ya kuwekeza kwenye biashara za ndani.
Mchakato huu huwa mrefu, na unaweza kuwakatisha tamaa wawekezaji wa kimataifa kuzingatia kampuni chipukizi kama fursa za uwekezaji.

Washiriki wa Kongamano la ujasirimali wa teknolojia la Seedstars Africa Summit 2018 walikuwa na bashasha la aina yake baada ya kujumika pamoja. Picha| K15.
Licha ya vikwazo hivi, kampuni chipukizi zina matumaini makubwa kwa siku zijazo, zikifanya kazi kwa bidii ili kushinda changamoto hizi, huku zikitafuta njia bunifu za kuongeza mitaji na kukuza biashara zao.
Mojawapo ya kampuni chipukizi ni KopaGas, kampuni ya Kitanzania ambayo imeunda huduma ya gesi ya kupikia ya kulipa kadri unavyotumia ambayo inaruhusu wateja kununua gesi kwa mkopo kwa kutumia malipo ya simu.
Hivi karibuni ilichangisha Sh23.5 bilioni katika raundi ya ufadhili iliyoongozwa na Energy Access Ventures, kampuni ya mtaji ya ubia ambayo inajishughulisha na kuwekeza katika makampuni ambayo hutoa ufikiaji wa nishati kwa jamii ambazo hazijafikiwa.
Pia startup ya Jibu inayotoa huduma ya maji safi ya kunywa kwa bei nafuu imechangisha zaidi ya Sh23.5 bilioni kwa ufadhili hadi sasa, na ina mipango ya kupanua shughuli zake kanda zote miaka ijayo.
Mafanikio ya baadhi ya kampuni chipukizi yanaonyesha kuwa licha ya vikwazo vya ufadhili vilivyopo, bado kuna uwezekano mkubwa wa ukuaji na ubunifu.
Kwa usaidizi sahihi na uwekezaji, kampuni chipukizi zina uwezo wa kuwa washiriki wakuu katika nyanja ya ujasiriamali wa kimataifa, kukuza ukuaji wa uchumi na kuunda fursa mpya kwa vijana na wafanyakazi wenye vipaji nchini.
Latest