Hapana: Wapinga pendekezo ada ya ving’amuzi Tanzania

June 15, 2022 2:34 pm · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Ada ni kuanzia Sh1,000 hadi Sh3,000 kulingana na matumizi yako
  • Hadi Desemba 2021 Tanzania ilikuwa na ving’amuzi hai milioni 3.19 huku takriban nusu vikitumia mfumo wa satelaiti.
  • Serikali imetaja sababu kuu ni kuongeza mapato nchini
  • Baadhi ya wananchi wamesema itakuwa mzigo kwao na wapo hatarini kuvitelekeza ving’amuzi vyao.

Dar es Salaam. Baadhi ya Watanzania wamewaomba wabunge kutopitisha ada ya ving’amuzi iliyopendekezwa katika bajeti kuu ya Serikali mwaka wa fedha 2022/23 wakieleza kuwa itazidi kuongeza gharama za maisha na kuwanyima haki ya kupata habari.

Katika hotuba ya  makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka ujao wa fedha iliyosomwa jana (Juni 14, 2022), Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alibainisha kuwa Serikali inapendekeza  kuanzisha utaratibu wa kutoza ada ya Sh1,000 hadi Sh3,000 kwenye ada ya matumizi ya king’amuzi kulingana na kiwango cha matumizi ya mtumiaji.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wameaimbia Nukta Habari kuwa hawaridhishwi na pendekezo hilo la kutoza ada kwenye ving’amuzi huku wakitaja sababu kuu ni kuongezeka kwa ugumu wa maisha nchini na kuwa watapata shida kupata habari.

Daniel Mdeka, mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam amesema Serikali inaonekana kukosa ubunifu wa kukusanya mapato kwa kuwa kwa sasa inaweza kutafuta vyanzo vingine vya pesa kuliko kuongeza tozo ambazo zinazidi kumwongezea mwananchi makali ya maisha.

“Tuna madini, gesi na  bandari hivyo vyote ni vyanzo vinavyoweza kutupatia kipato kikubwa (nchini) kuliko kuwaumiza wananchi,” amesema Mdeka ambaye hujishughulisha na kutengeneza vifaa vya umeme.


Zinazohusiana:


Mbali na kuongeza gharama za maisha, baadhi wamesema uamuzi huo utaongeza gharama za sasa za vifurushi kiasi cha kuwafanya wasivitumie kabisa katika kupata habari na burudani.

Saida Rilo anayeishi Kijitonyama jijini hapa amesmea anaona kama Serikali ina lengo la kuwakandamiza na kutokana na mapendekezo hayo hataweza kumudu gharama zaidi ya kifurushi kidogo cha Azam TV anachotumia kwa sasa.

“Kwa kuwa mini, ni mjasiriamali nikirudi nyumbani jioni nataka kuangalia taarifa ya habari ya yale yaliyojiri siku zima kama itakuwa hivyo basi nitakuwa nafungulia redio na si ving’amuzi,” amesema Saida anayeuza genge la mboga mboga.

Wakati Saida akijipanga kugeukia redio kupata habari, wengine wanapanga kususa kwa kuwa hata vifurushi walivyokuwa wanatumia ni vya ngazi ya chini zaidi kutokana na kipato chao kuwa kidogo.

“Mimi kwangu sitamudu, itabidi nizime televisheni nikae pembeni, wataangalia wenye hela….nashauri wabunge waangalie hiyo bajeti, lakini kwa sisi wananchi wanatuumiza,” amesema Witness Kitime kutoka Mwananyamala.

Katika kutatua adha hiyo, mkazi wa Kigamboni, Abdulrahman Mwamaka amesema Serikali inapaswa kuangalia kuwa ving’amuzi si starehe bali ni chanzo cha habari na kuongeza ada hiyo itafanya watoboe zaidi mifuko yao kupata huduma hiyo inayozidi kukua nchini.

“Itakuwa ngumu sana, hata kama tutamudu (ada ya ving’amuzi) itakuwa mara moja moja sana, kwa sababu kwa sasa tu unaweza ukakaa mwezi huu usilipe, hivyo utakuwa unapata ‘local channel’  (chaneli za ndani) nyingine huzipati,” amesema Mwamaka.

Bajeti kwa mwaka 2022/23 inaonesha kuwa Sh 41.48 trilioni zinatarajiwa kukusanywa na kutumika huku jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh28.02 trilioni, sawa na asilimia 67.5 ya bajeti yote.

Ada ya ving’amuzi ni moja ya vyanzo vya mapato vitakavyonehemesha mfuko wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kugharamia bajeti hiyo itakayoanza Julai mosi mwaka huu. Hata hivyo, Serikali haijaweka bayana kiasi ambacho inatarajia kukusanya kutoka katika ada za ving’amuzi hivyo.

Hadi mwaka 2021, takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinabainisha kuwa kulikuwa na ving’amuzi hai milioni 3.19 ambavyo kati yake milioni 1.58 vinatumia satelaiti.

Iwapo Serikali itatoza ada angalau Sh1,000 kwa kila king’amuzi kwa mwezi huenda ikavuna Sh3.19 bilioni kutoka vifaa hivyo hai sawa na Sh38.28 bilioni kwa mwaka.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...