Hapana: Taa za mionzi hazizuii maambukizi ya corona

August 29, 2022 12:43 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalamu waonya mionzi hii kusababisha kansa ya ngozi na upofu.
  • Licha ya kuwa chanzo cha vitamin D, ni hatari kuutumia majumbani
  • Chanjo ni njia pekee ya kuzuia maambukizi.

Dar es Salaam. Kumekuwa na uzushi unaoendelea kuhusu njia mbalimbali za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Uviko-19 ikiwemo kutumia taa zenye mionzi (Ultraviolet (UV)) inayotumika katika matibabu na maabara.

Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mionzi hiyo haitibu wala kuzuia ugonjwa wa Uviko-19 kumpata mtu. 

Mionzi ya Ultraviolet (UV)  ni mionzi ya sumaku umeme inayotumika viwandani kwa ajili ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali. Hutumika pia maabara kwa ajili ya kuua bakteria, virusi na vijidudu vingine vinavyoeneza magonjwa.

Mionzi hii pia inapatikana kwenye jua ambapo husaidia uzalishaji wa Vitamini D, kuboresha ngozi na kuupa mwili nguvu.

Hata hivyo, matumizi ya mwanga huu hayazuii maambukizi ya Corona na  yanaweza kusababisha madhara mengi kwenye mwili wa binadamu.

Wataalam wa afya wanaonya kuwa matumizi ya mionzi hii kama njia ya kuua virusi vya Uviko-19 majumbani, kwani ni vigumu kujua kiwango sahihi cha mionzi inayohitajika.

WHO katika  ripoti yao ya  mionzi ya ultraviolet iliyotolewa June 21, 2022, imeeleza kuwa sehemu ndogo tu ya mwanga UV inasaidia kuzalisha vitamin D, lakini umekuwa chanzo kikubwa cha saratani na upofu.

“Matumizi makubwa ya mionzi ya  UV yanahusishwa na matokeo mabaya ya kiafya kwani inaweza kusababisha saratani kwa wanadamu” imesema ripoti ya shirika hilo.

Kwa mujibu wa jarida la Healthline,  taa za mionzi ya UV  inaweza kutumika kuua vijidudu sehemu mbalimbali, lakini siyo sahihi kutumika moja kwa moja kwa ngozi ya mtu kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu  kuwa ni suluhu ya Uviko-19.

“Kumbuka, mwanga wa UV unaweza kuwa na madhara kwa watu mfano  mzio, kuwasha kwa ngozi, au uharibifu  wa ngozi,” limesema jarida hilo. 

Fanya haya kujikinga na Uviko-19

Mpaka sasa njia pekee ya kujikinga na Uviko-19 ni kuchanja chanjo za ugonjwa huo ambazo zinapatikana kwenye vituo vya afya nchi nzima.

Wizara ya Afya nchini imeendelea kusisitiza wananchi kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu ikiwemo kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono, kupunguza mikusanyiko isiyo ya lazima na kunawa mikono kwa maji tiririka mara kwa mara.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW