Filamu ya “Honest Thief”: Utarajie nini unapoanza uhalifu?
- Ni filamu inayomhusu mwizi ambaye anaamua kujisalimisha baada ya kupata mpenzi.
- Wapelelezi wanaohusika na kesi yake, wanamzunguka na kutaka kuiba fedha ambazo anataka kuzirudisha.
- Safari ya kuwawinda maafisa hao inakolea baada ya mpenzi wake kuuumizwa.
Dar es Salaam. Riiin riiiing! Ni simu ya mezani ya FBI inaita na Carter anaongea “nataka nijisalimishe lakini nataka kuweka makubaliano.”
“Makubaliano gani?,” wanauliza FBI.
“Ninawapatia pesa zote nilizowahi kuiba na mimi nahitaji kupunguziwa hukumu. Ni muhimu,” anasema Carter.
Kuweka mambo sawa, Tom Carter (Liam Neeson) ni mwizi mwenye ueledi wake. Na baada ya kudondoka kimahaba kwa mwanadada Annie (Kate Walsh) anatamani kuanza maisha yake upya huku akisafisha dhambi yake aliyoifanya zamani.
Kati ya dhambi hizo, ni wizi alioufanya hapo mwanzoni ambapo amefanikiwa kujikusanyia kitita cha Sh20.9 bilioni kwenye benki zaidi ya tano.
Hata baada ya kuiba, Carter alifanikiwa kuukwepa mkono wa dola kwani hawakuweza kufahamu kama ni yeye ndiye anayehusika.
Soma Zaidi
- Vunja mbavu zako na filamu ya “Hubie Halloween”
- Sababu za wabunifu wa nguo kutumia malighafi za nje
- Tanzania yaanza kutumia helikopta kuzima moto Mlima Kilimanjaro
Imekuwaje ghafla catrer anahitaji kubadilika na kujisalimisha kwenye vyombo vya dola? Jibu ndiyo hilo, amepata mwanamke ambaye yupo tayari kubadilisha maisha yake na kumfanya mtu mwema.
Mwizi huyo baada ya kumpenda Annie, anahitaji mwanzo mpya na hivyo anataka kurudisha fedha ambazo aliziiba ili awe na amani bila haja ya kudanganya kuhusu mambo aliyoyafanya kale.
Jembe huyo anapoamua hayo, maafisa wawili wa FBI wanakabidhiwa kesi hiyo lakini hapo ndipo mambo yanapoenda kombo baada ya maafisa hao kukiona kilima hicho cha fedha.
“Njemba inasema ukweli lakini tunaweza kubaki na hizi fedha sisi wenyewe,” mmoja kati ya maafisa hao anamwambia mwenzake huku wakipanga njama za kumzunguka Carter ambapo wanaanza kwa kumuua mkuu wa kesi hiyo.
Pale wanapojichanganya na kumjeruhi Annie, Carter anapiga simu na kusema…
“Mpenzi wangu hakuhusika na lolote kwenye hili. Agent Evans, ninakuja kwa ajili yako,” anasema Carter.
Hapo ndipo Evans anapofahamu kuwa amekalia kuti kavu baada ya kutaka kumdhulumu mwizi ambaye anatafuta nafasi ya kujisafisha.
Annie atapona, Je, Evans atakimbia na fedha za Carter?, dhamira ya Carter itafanikiwa? Yafahamu yote haya kupitia filamu ya “Honest Thief” inayoonyeshwa kwenye kumbi za filamu za Century Cinemax jijini Dar es Salaam zikiwemo Mlimani City, Aura Mall na Mkuki House.
Kama filamu siyo fungu lako? Una mambo mengi ya kufanya wikiendi hii ikiwemo kutazama video YouTube au kuwatembelea marafiki na ndugu.