Sababu za wabunifu wa nguo kutumia malighafi za nje

November 25, 2020 6:20 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Viwanda vingi vilivyopo nchini vinazalisha kanga na vitenge. 
  • Kutofautiana kwa mahitaji na watu kutaka kuwa na muonekano tofauti. 
  • Serikali yasema tayari imeanza mchakato wa kujenga viwanda vya nguo kukidhi mahitaji ya soko la ndani. 

Dar es Salaam. Nikiwa mdogo, nilifurahia nilipomuona mama akipokea zawadi za vitenge kutoka kwa rafiki zake na hata akijinunulia mwenyewe.

Furaha ilizidi zaidi pale mama yangu alipoamua kukata kipande cha kitenge na kunishonea shati liililoendana na suruali zangu na kisha kunivalisha na taratibu siku za jumapili tukitembea pamoja kuelekea kanisani na hata kwenye mitoko mingine.

Nilikuwa na furaha hiyo kwa sababu nilijua ninavaa kitu kilichotengenezwa na mtu kutoka Tanzania.

Vitenge ni kati ya bidhaa za nguo ambazo viwanda vya Tanzania vinajivunia kutengeneza. Siyo vitenge tu zipo kanga pia ambazo ni vazi maarufu kwa wanawake na wasichana japo wanaume pia hawajakubali kupitwa nalo.

Licha ya kuwa wapo wabunifu mbalimbali ambao wanatumia vitenge na kanga kama malighafi za kubuni mavazi mbalimbali, baadhi ya wabunifu wanalazimika kuagiza malighafi za vitambaa vya aina mbalimbali kutoka nje ya nchi vikiwemo vya hariri, satini na silika.

Hata kwa baadhi ya malighafi zinazopatikana nchini, bado wabunifu hao wamekuwa wakipendelea kutumia zinazotoka nje ya nchi. 

Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) umebaini kuwepo na sababu nyingi zinazofanya wabunifu kutotumia malighafi zinazozalishwa nchini katika ubunifu wa mavazi yao. Je sababu hizo ni zipi?

Ukosefu wa malighafi zinazoendana na kazi zao

Mbunifu wa magauni ya matukio mbalimbali yakiwemo harusi na mitoko, Juma Wilson amesema kwa shughuli zake, hawezi kutumia kanga na vitenge kutengeneza mavazi anayobuni.

Wilson ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz)  kuwa, vitambaa ambavyo anatumia kushona magauni vikiwemo vya “lace” (vitambaa chenye asili neti) havizalishwi nchini hivyo kutumia malighafi zinazotoka nchi za nje ikiwemo Marekani, China, Uturuki na Thailand.

“Vitambaa unavyoweza kupata hapa ni vile vya nguo za wazawa kama kanga na vitenge. Sitengenezi magauni ya aina hiyo,” amesema Wilson maarufu kama fundi Juma anayefanyia shughuli zake jijini Dar es Salaam.

Wilson ambaye hutengeneza magauni ya harusi amesema hawezi kufanya kazi hiyo kwa vitenge na kanga pekee. Picha| Juma Wilson.

Kutafuta utofauti miongoni mwa wabunifu

Kazi za wabunifu haziwezi kuwa sawa kwa sababu ni kazi za sanaa zinazozalishwa kwa matokeo ya utashi wa mbunifu.

Wilson amesema kwa kuwa kila mbunifu ana utashi wake, analazimika kutumia malighafi ambazo zitamtofautisha na wabunifu wengine. Hivyo, wengine huamua kuagiza kutoka nje ya nchi ili kufikia viwango vya kimataifa. 

Kutokuwepo kwa viwanda vinavyojitosheleza

Rahma Baijun ambaye ni mbunifu wa mavazi kutoka MnM Clothing Line ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa licha ya kuwa Tanzania ina viwanda vya kutengeneza malighafi za nguo lakini bado havitengenezi malighafi za kutosha zinakidhi mahitaji ya wabunifu wa mavazi.

Baijun amesema kuna malighafi mbalimbali za nguo ikiwemo hariri na satini ambazo hazizalishwi Tanzania kwa sababu viwanda vingi vimejikita kutengeneza kanga na vitenge. 

“Siyo wote wanavaa vitenge na khanga,” amesema Baijun.

Mbunifu huyo ambaye anamiliki duka la mtandaoni la kuuza nguo anasema hali hiyo ndiyo inafanya Tanzania iagize vitambaa nje ya nchi kuliko inavyouza. 

Ripoti ya takwimu muhimu Tanzania (Tanzania in Figures 2019) ya mwaka 2019 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kwa mwaka 2019, viwanda vya nguo vilizalisha bidhaa za nguo mita za mraba milioni 45 ikiwa imeshuka kwa asilimia 15.1 kutoka mita za mraba milioni 53 za mwaka 2018.

Changamoto hizo za viwanda vya nguo zinachangiwa na tija ndogo katika uzalishaji wa pamba nchini, na teknolojia hafifu katika utengenezaji wa bidhaa mwambata zinazoweza kuzalishwa kutokana na uchambuaji wa pamba mbegu. 

Utofauti wa bei wa bidhaa hizo

Wakati mwingine wanunuzi hupendelea malighafi za nje kwa sababu huzipata kwa bei ya chini ikilinganishwa na za ndani ambazo bei zake huathiriwa na gharama za uzalishaji. 

“Mita moja (ya kitambaa) hapa nchini unaweza kununua kwa Sh10,000 hadi 15,000, mita hiyo hiyo nchi za nje inanunuliwa hata kwa Sh800,” amesema Baijun.

Ikizingatiwa kuwa wabunifu wengi wanapenedelea kutumia vitambaa vya nje, hali hiyo huongeza ushindani na kupunguza soko la malighafi za ndani.

Nini kifanyike?

Wilson ambaye pia ni mdau wa vitambaa vya nje ya nchi amesema viwanda vya ndani vipunguze bei za malighafi zake na pia viongeze wigo wa uzalishaji ili kukidhi matakwa ya soko la ndani linakua kila siku. 

Amebainisha kuwa ni wakati muafaka kwa mamlaka zilizopo kuangalia namna ya kuunga mkono juhudi za wabunifu kwa kuwawekea kodi rafiki za vifaa na hata za bidhaa zao.

“Ni wakati wa mamlaka kuangalia namna wanaweza kutusaidia. Badala ya kila mwisho wa mwezi kuwa nawaza malipo ya kodi, nianze kuwaza ubunifu na kujiendeleza kama mbunifu. Hapo nitatengeneza bidhaa bora na zinazoweza hata kuwanufaisha Watanzania wenye hali ya kawaida kiuchumi,” amesema mbunifu huyo.


Soma zaidi:


Naye Baijun amesema ni wakati wa Serikali kuja na sera rafiki za uwekezaji zitakazochochea uanzishwaji wa viwanda vingi vya nguo nchini ili kutengeneza ajira na kuongeza mapato ya umma.

Waziri wa Viwanda na  Biashara, Innocent Bashungwa katika hutuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2020/21 amesema wamekamilisha  upimaji wa eneo la viwanda la TAMCO mkaoni Pwani ambapo Ekari 94 zimetengwa kwa ajili ya viwanda vya nguo na mavazi.

“Jumla ya ekari 201.04 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na miundombinu (katika eneo hilo la TAMCO),” amesema Bashungwa katika hutuba hiyo.

Huenda ujenzi wa viwanda hivyo, utachochea kilimo cha pamba, uzalishaji wa malighafi za nguo na soko la nguo zinazotengenezwa nchini Tanzania, jambo litakalosaidia wabunifu kutumia bidhaa za ndani. 

Enable Notifications OK No thanks