Fedha zaidi zinahitajika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi
- Michango iliyowasilishwa mwaka huu ni pungufu kwa asilimia moja ya lengo la mwaka 2030.
- Ripoti ya UNEP imetaka hatua zaidi kuchukuliwa kukabiliana na hewa chafuzi angani.
Dar es Salaam. Kufuatia mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha kuongezeka kwa joto duniani linaloathiri maisha ya watu na viumbe, fedha zaidi zinahitajika kukabiliana na mabadiliko hayo.
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) inayoangazia viwango vya utoaji hewa chafu kwa mwaka 2030 na viwango vya sasa iliyotolewa Oktoba 27, 2022 inasema kiwango cha fedha kilichowekwa na nchi wanachama kupunguza janga hilo ulimwenguni hakitoshi.
Mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa tabianchi (COP26) uliofanyika huko Glasgow nchini Uingereza uliafiki kuwa nchi wanachama kuongeza viwango vya michango ya kitaifa (NDCs) kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo, viwango hivyo vilivyowekwa havitoshi kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yaliyopo na yanayoendelea.
“Michango iliyowasilishwa mwaka huu itapunguza tani milioni 500 pekee za ujazo za hewa ya ukaa, kiwango ambacho ni pungufu kwa asilimia moja ya lengo la mwaka 2030,” imesema ripoti ya UNEP.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa kukosekana kwa kiasi hicho kunamaanisha kuwa dunia inaelekea kwenye ongezeko la kiwango cha joto na kushindwa kudhibiti kuvuka nyuzijoto 2 au 1.5 katika kipimo cha selsiyasi.
“Ripoti hii inatueleza kisayansi kile ambacho mazingira yamekuwa yanatueleza mwaka mzima, kupitia mafuriko, vimbunga na mioto ya nyika isiyozimika,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen aliyekuwa akizungumzia ripoti hiyo.
Soma zaidi:
Uviko-19 wafichua dharura kuboresha mifumo ya udhibiti wa taka duniani
Hatua za kuchukua
Ripoti inasema ingawa hatua zinachukuliwa kuelekea kuhakikisha hewa chafuzi inayozalishwa inaondolewa angani (net zero emmission) kwenye sekta za usambazaji umeme, viwanda, usafirishaji na kwenye majengo, bado kasi inahitajika zaidi.
“Usambazaji umeme umesonga mbele kiteknolojia, kwa kuwa gharama za umeme unaozalishwa kwa nishati rejelezi imepungua. Hata hivyo, kasi ya kipindi cha mpito kuelekea nishati rejelezi iongezwe,” imesema ripoti hiyo.
Kwa upande wa mifumo ya uzalishaji chakula ambayo inachangia theluthi moja ya hewa chafuzi, ripoti inapendekeza uhifadhi wa mifumo anuai asilia, kubadilisha vyakula ambavyo watu wanakula na kuhakikisha uzalishaji wa vyakula mashambani hauzalishi hewa ya ukaa.
Kiuchumi, ripoti inasema harakati za uchumi zitoazo kiwango kidogo cha hewa chafuzi zitahitaji uwekezaji wa angalau Sh920 trilioni na zaidi kwa mwaka.
Latest