Joto kali linavyowatesa watoto zaidi ya milioni 500 duniani
- Mtoto 1 kati ya 3 anaishi katika nchi zenye joto kali duniani.
- Joto kali husababisha magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji na moyo.
- Mpaka kufikia mwaka 2050 takriban watoto bilioni 2 watakuwa wameathiriwa na joto kali.
- Serikali zatakiwa kuchukua hatua za mapema kukabili ongezeko la joto.
Dar es Salaam. Watoto milioni 559 duniani kote wanakabiliwa na joto kali hali inayosababisha matatizo ya afya ikiwemo magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji na moyo.
Ripoti ya Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) iliyotolewa Oktoba 25, 2022 inasema mpaka kufikia mwaka 2050 takriban watoto bilioni 2 watakuwa wameathiriwa na mawimbi tofauti ya joto kali bila kujali ukanda waliopo.
Ripoti hiyo iiyopewa jina la “Mwaka wa baridi zaidi katika maisha yao yote” inaonyesha kuwa waathirka wakubwa wa mawimbi ya joto ni watoto ukilinganisha na watu wazima.
“Hii ni kwa sababu hawana uwezo wa kudhibiti joto la mwili wao ikilinganishwa na watu wazima. Kadiri watoto wanavyokabiliwa na mawimbi ya joto, ndivyo uwezekano wa kupata matatizo ya kiafya unaongezeka,” imesema ripoti hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell aliyekuwa akizungumza kuhusu ripoti hiyo amesema watoto wengi zaidi wataathiriwa na misimu ya joto kwa muda mrefu, “joto litakuwa kali zaidi na litatokea mara kwa mara katika miaka 30 ijayo hali inayotishia afya na ustawi wao.”
“Tayari, mtoto 1 kati ya 3 anaishi katika nchi ambazo zinakabiliwa na hali ya joto kali na karibu mtoto 1 kati ya 4 wanakabiliwa na misimu mikubwa ya joto, na hali itazidi kuwa mbaya zaidi,” amesema Russell.
Bosi huyo wa UNICEF amesema Serikali lazima ziweke kikomo cha joto duniani kwa haraka hadi kufikia nyuzi joto 1.5 na kupatikane ufadhili wa kukabiliana na hali hii ifikapo mwaka 2025 ili kupunguza athari za joto duniani.
Zinazohusiana:
- Namna wenye magari ya gesi asilia wanavyookoa maelfu ya fedha Tanzania
- Statoil yaja kivingine uchimbaji gesi Tanzania
- Mengi kuwekeza Sh68 bilioni uchimbaji wa mafuta, gesi Tanzania
Nini kifanyike kupunguza athari hizo?
Ripoti hiyo ya UNICEF imependekeza mambo makuu manne yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa haraka na Serikali zote duniani ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko kwenye huduma za kijamii.
“Kila Serikali lazima ibadilishe huduma muhimu za kijamii ambazo ni maji, usafi wa mazingira na usafi, afya, elimu, lishe, ulinzi wa kijamii na ulinzi wa mtoto ili kulinda watoto na vijana,” imesema ripoti hiyo.
Pia ziandae namna ya watoto kuishi katika ulimwengu unaobadilika badilika ikiwemo kutoa elimu kwa vijana na watoto kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Jambo lingine lililopendekezwa na ripoti hiyo ni Serikali kuweka kipaumbele kwa watoto na vijana katika utoaji wa fedha na rasilimali za mabadiliko ya tabianchi.
Nchi zilizoendelea lazima zitekeleze ahadi zao walizoweka kwenye mkataba wa mabadiliko ya tabia ya nchi (COP26) ya kuwa watafadhili Sh 92 trilioni kwa mwaka ifikapo 2025 kwa kiwango cha chini.
Sambamba na jitihada hizo pia Serikali zimetakiwa kupunguza utoaji wa gesi chafuzi zinazoharibu mazingira kwa kuangalia upya mipango na sera zao za mabadiliko ya tabianchi za kitaifa ili kuongeza matamanio na hatua zaidi za kukabiliana na janga hili.
Hata hivyo, ili kutimiza azma hiyo, nchi ziwe tayari kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwa angalau asilimia 45 ifikapo mwaka 2030 ili joto lisizidi nyuzi joto 1.5.
Latest