Rais Samia azitolea uvivu nchi tajiri kuhusu mabadiliko ya tabianchi

November 2, 2021 5:31 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezungumza katika mjadala wa wazi wa viongozi kwenye mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, CO26 huko Glasgow, Scotland na kusema mshikamano na juhudi zao kama viongozi katika kukabili mabadiliko ya tabianchi vitapimwa si kwa ahadi kubwa wanazotoa kwenye mkutano huo bali kwa jinsi wanatekeleza vipengele vyote vya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi. Picha| UN.


  • Azitaka zitoe fedha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
  • Ahimiza mshikamano, utashi kukabiliana na suala hilo.
  • Kuhutubia leo mkutano wa mabadiliko ya tabianchi huko Glasgow, Scotland.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amezihimiza nchi zilizoendelea duniani kutekeleza kwa vitendo ahadi zao za kutoa fedha kwa nchi maskini zitakazosaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu suala hilo ni la kimataifa na linahitaji mshikamano.

Rais Samia alikuwa akizungumza jana Novemba Mosi katika mjadala wa wazi wa viongozi kwenye mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi (CO26) huko Glasgow, Scotland.

Amesisitiza kuwa fedha za kutosha hususan kupitia misaada ya fedha itakuwa ni msingi katika mikakati ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika nchi za kipato cha chini.

Amesema nchi yake ya Tanzania na nyingine za kipato cha chini zimeandaa mipango ya kina ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (NDCs) lakini zinahitajika fedha kuitekeleza.  

“Mipango yetu ni mtambuka katika sekta zote muhimu lakini hatuwezi kufanikisha bila usaidizi wa kutosha na teknolojia inayotakiwa ili kujenga uwezo wetu,” amesema Rais.

Amezitaka nchi tajiri duniani kutekeleza kwa vitendo ahadi zao kwa nchi za kipato cha chini kwa kuzipatia fedha ili kuzinusuru na mabadiliko ya tabianchi yanayoitesa dunia kwa sasa.

“Mabadiliko ya tabianchi ni suala la dunia nzima na hivyo majawabu yake ni lazima yawe ya kimataifa na hivyo tunatoa wito kwa nchi zilizoendelea ambazo ndio zinaongoza kwa uchafuzi zitekeleze kwa vitendo ahadi zao za kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa fedha za kutosha kutuwezesha sisi nchi za kipato cha chini kufanikisha malengo yetu kwenye michango ya kitaifa ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa uendelevu,” amesisitiza Rais Samia.

Amesema mshikamano na juhudi zao kama viongozi katika kukabili mabadiliko ya tabianchi zitapimwa si kwa ahadi kubwa wanazotoa kwenye mkutano huo bali kwa jinsi wanatekeleza vipengele vyote vya mkataba wa Paris wa mwaka 2015 wa mabadiliko ya tabianchi.

“Waheshimiwa kama hatutachukua hatua sasa tena kwa mshikamano, lengo la kuwa na kiwango cha joto katika nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi litatoweka punde na hatutalifikia,” amesema kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Mkutano huo wa COP26 unafanyika kati ya Oktoba 31 hadi Novemba 12, 2021 jijini ambapo unawakutanisha wataalam wa mazingira, viongozi wa serikali, mashirika na taasisi binafsi kujadili namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

COP26 ni muendelezo wa mijadala ya kimataifa ambayo inaziunganisha nchi mbalimbali ulimwenguni kutafuta suluhu ya kudumu ya mabadiliko ya tabianchi ambayo ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha bahari, joto la dunia, ukame, mafuriko na vimbunga.

Mabadiliko hayo husababishwa na shughuli za asili na kibinadamu ikiwemo ongezeko la viwanda na watu, ukataji wa miti na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira.

Leo Rais Samia anatarajia kuhutubia mkutano huo ambapo atazungumzia mambo mbalimbali ikiwemo Tanzania inavyokabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuboresha maisha ya raia wake. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW