COP27: Afya iwe kitovu majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi

November 7, 2022 6:21 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Mwanamke akijarivu kuvuka maji ya mafuriko mjini Jakusko jimbo la Yobe Nigeria. WFP/Arete/Ozavogu Abdul


  • Ni baada ya kubainika kuwa ni chanzo kikubwa cha magonjwa kwa watu.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk Tedros Ghebreyesus amesema mabadiliko ya tabianchi yanafanya mamilioni ya watu kuwa wagonjwa au katika hatari zaidi ya magonjwa duniani kote.

Bosi huyo wa WHO ametoa kauli hiyo wakati mkutano wa mabadiliko ya tabianchi (COP27) ukiwa unaendelea nchini Misri ambapo wadau mbalimbali wamekusanyika kujadili suluhu zitakazosaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi duniani ikiwemo mafuriko, ukame na ongezeko la joto.

“Ni muhimu kwamba viongozi na watoa maamuzi wanaokutana katika COP27  kuweka afya katika kiini cha mazungumzo,” amesema Dk Tedros Novemba 6 wakati wa ufunguzi wa mkutano huo. 

“Afya yetu inategemea afya ya mifumo ya ikolojia inayotuzunguka, na mifumo ya ikolojia hii sasa iko chini ya tishio la ukataji miti, kilimo na mabadiliko mengine katika matumizi ya ardhi na maendeleo ya haraka ya ukuaji wa mijini,” amesema.

Uvamizi unaoendelea zaidi katika makazi ya wanyama unaongeza fursa kwa virusi hatari kwa wanadamu kufanya mabadiliko kutoka kwa wanyama wao. 

Kati ya mwaka 2030 na 2050, mabadiliko ya tabianchi yanatarajiwa kusababisha takriban vifo 250,000 vya ziada kwa mwaka kutokana na utapiamlo, malaria, kuhara na shinikizo la joto kali.

Amesema gharama za uharibifu wa moja kwa moja kwa afya bila kujumuisha gharama katika sekta zinazoamua mustakbali wa afya kama vile kilimo, maji na usafi wa mazingira, inakadiriwa kuwa kati ya Dola za Marekani bilioni 2 hadi 4 (Sh4.6 trilioni hadi Sh9.3) kwa mwaka ifikapo 2030.


Zinazohusiana:


Afya ziko hatarini 

Kwa mujibu wa WHO, ongezeko la halijoto duniani ambalo tayari limetokea linasababisha hali mbaya ya hewa ambayo huleta joto kali na ukame, mafuriko makubwa na vimbunga vinavyozidi kuwa na nguvu na pia dhoruba za kitropiki. 

Mchanganyiko wa mambo haya inamaanisha athari kwa afya ya binadamu inaongezeka na kuna uwezekano wa kuharakisha athari hizo.

“Lakini kuna nafasi ya matumaini, haswa ikiwa serikali zitachukua hatua sasa kuheshimu ahadi zilizotolewa huko Glasgow mwezi Novemba 2021 na kwenda mbali zaidi katika kutatua mzozo wa mabadiliko ya tabianchi”.

Shirika hilo linasema COP27 itakuwa fursa muhimu kwa ulimwengu kuja pamoja na kujitolea tena kuhuisha lengo la makubaliano ya Paris  la kuhakikisha kiwango cha joto kinasalia kuwa nyuzijoto 1.5.

WHO inatoa wito kwa serikali kuongoza awamu ya haki, ya usawa na ya haraka kutoka kwa nishati ya mafuta kisukuku na kuingia kwenye mpito kwa siku zijazo kuhamia kwenye nishati safi. 

“Uboreshaji wa afya ya binadamu ni jambo ambalo raia wote wanaweza kuchangia, iwe kupitia kukuza maeneo ya kijani kibichi zaidi ya mijini, ambayo huwezesha kukabiliana na hali ya hewa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” imeeleza WHO. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW