Rais Samia kushiriki mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi wa AU nchini Ethiopia

February 14, 2025 11:05 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Mkutano huu unatarajiwa kujadili ajenda mbali mbali ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia.
  • Kabla ya mkutano huo Rais Samia pia anatarajia kuhudhuria Mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika leo.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajia kufanya ziara ya kikazi jijini Addis Ababa, Ethiopia, kuanzia  leo hadi Februari 16, 2025 kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).

Taarifa ya Sharifa Nyanga, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu  iliyotolewa Februari 13, 2025 inabainisha kuwa mkutano huo utahusisha uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa umoja huo kwa mwaka 2025.

Uchaguzi huo unafanyika ili kumpata mrithi wa Rais wa umoja huo Mohamed Ould Cheikh El Ghazouani kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania anayemaliza muda wake.

Kwa mujibu wa Katiba ya AU, kila mwaka wakuu hao wa nchi wanatakiwa kufanya uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti wa wa umoja huo ambaye huchaguliwa kutoka miongoni mwa viongozi wa nchi wanachama, kwa msingi wa mzunguko wa kanda za Afrika.

https://twitter.com/ikulumawasliano/status/1890273534452400608

Aidha, viongozi wapya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika watachaguliwa, wakiwemo Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, na Makamishna sita.

Mbali na uchaguzi, viongozi hao wwatajadili taarifa ya ushiriki wa Umoja wa Afrika kwenye mkutano wa Nchi Tajiri Duniani (G20), Utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na taarifa kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi. 

Mkutano huo pia utajadili ajenda kuhusu Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia iliyopendekezwa na nchi ya Tanzania. 

Hata hivyo, kabla ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa AU, Rais Samia pia atahudhuria Mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika utakaofanyika leo Februari 2025.

Sanjari na hayo mkutano huo unatarajiwa kujadili masuala muhimu yanayolenga kuimarisha juhudi za AU katika kudumisha amani na usalama, pamoja na kujadili mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazokabili bara hili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks