Simbachawene: Zaidi ya asilimia 40 ya watumishi wa umma Tanzania hawafanyi kazi

February 14, 2025 11:53 am · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni na Tume ya Utumishi wa Umma Tanzania.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  George Simbachawene amesema zaidi ya asilimia 40 ya watumishi wa umma nchini hawafanyi kazi licha ya kulipwa mshahara kila mwezi.

Simbachawene amesema hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni na Tume ya Utumishi wa Umma Tanzania.

Waziri Simbachawene aliyekuwa akifunga Kikao kazi cha tano cha Serikali Mtandao  leo Februali 14, 2025  jijini Arusha amesema watendaji wakuu wa taasisi za umma wana wajibu wa kuhakikisha  kila mtumishi anatekeleza majukumu yake ipasavyo.

‘’Watumishi ni lazima wafanye kazi kwani wasipofanya kazi wanakuangusha wewe mkuu wa taasisi, lazima tuwe na jamii inayoandaliwa kufanya kazi’’ amesisitiza Simbachawene.

Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha tano cha Serikali Mtandao kilichofanyika kwa muda wa siku tatu jijini Arusha ambacho kimefungwa  leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene. Picha l Lusungu Helela

Simbachawene ameongeza kuwa, kwa mujibu wa tafiti hiyo, wavivu, wazembe, wagonjwa pamoja na waliosusiwa kutokana na vipaji na uwezo wao ni  asilimia 40 ya watumishi wanaolipwa pasipo kufanya kazi

Hata hivyo, amewataka wakuu hao wa taasisi  kuwatumia watumishi wa umma wenye vipaji na uwezo badala ya kuwafanyia fitina na hujuma hali inayosababisha kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

“Kumeibuka tabia ya baadhi ya watendaji wakuu pindi mtumishi  mwenye sifa za ziada anapohamia kwenye taasisi anayoiongoza hupata hofu na kutompangia majukumu kwa hisia kuwa ametumwa kumchunguza  au kuchukua nafasi yake,

Tabia hiyo kwenye utumishi wa umma haikubaliki na wale wenye tabia hiyo wajirekebishe haraka ,Taasisi hizo ni za umma na sio mali yao binafsi,” amesema Simbachawene.

Katika hatua nyingine, kutokana na ongezeko la matumizi ya simu kwa wananchi, Simbachawene amezitaka taasisi za umma kutoa huduma za kidijitali kutokana na fursa hiyo huku akitoa onyo kwa taasisi ambazo hazijaanza kutumia mfumo wa kidijitali wa e-Mrejesho kuanza kuutumia mfumo huo mara moja kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks