Zimamoto yatangaza nafasi za ajira kwa vijana
- Ajira hizo ni kwa ajili ya waombaji wenye elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita wenye ujuzi maalum, na wahitimu wa shahada katika taaluma mbalimbali.
Arusha. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limetangaza nafasi za ajira kwa vijana wa Kitanzania wenye sifa stahiki, likiwataka kutuma maombi yao kupitia mfumo wa ajira wa jeshi hilo kabla ya tarehe 28 Februari, 2025.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, John Masunga Februari 13, 2025 nafasi hizo ni kwa ngazi ya Konstebo na zinahusisha waombaji wenye elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita wenye ujuzi maalum, na wahitimu wa shahada katika taaluma mbalimbali.
Miongoni mwa vigezo vilivyotajwa kwa waombaji ni kuwa na uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa, afya njema kimwili na kiakili, kutokuwa na kumbukumbu za uhalifu, kutokuwa na alama za kuchorwa mwilini (tatoo), na kutowahi kutumia madawa ya kulevya.
Aidha, waombaji wanapaswa kuwa tayari kuhudhuria mafunzo ya taaluma ya Zimamoto na Uokoaji.
Kwa waombaji wa nafasi za madereva wa magari makubwa, wanapaswa kuwa na leseni ya daraja E huku marubani wa helikopta wakihitajika kuwa na umri wa miaka 18 hadi 35. Kwa upande wa wahitimu wa shahada, nafasi za ajira zinazopatokana ni kwa taaluma kama uhandisi bahari, TEHAMA, sheria, uchumi, na uhandisi wa Ndege.
Maombi yote yanapaswa kufanywa kupitia mfumo wa ajira wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa njia ya mtandao kupitia ajira.zimamoto.go.tz, huku nyaraka muhimu kama barua ya maombi, nakala za vyeti vilivyothibitishwa, cheti cha kuzaliwa, na kitambulisho cha utaifa (NIDA) zikiambatanishwa.
Jeshi hilo limeonya kuwa maombi yatakayowasilishwa kwa barua pepe, posta au kwa mkono hayatapokelewa, huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa kwa wale watakaowasilisha nyaraka za kughushi au taarifa za uongo.
Hata hivyo, jeshi hilo halijabainisha idadi ya nafasi za ajira zizlizotolewa kwa ajili ya vijana wakitanzania.
Latest
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/download-3-1024x696-1.jpeg?fit=300%2C204&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/VFLt5vHV7aCoLrLGjP9Qwm.jpg?fit=300%2C169&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/71f29364436954e34871d65ac6f43839-scaled.jpg?fit=300%2C200&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Gi21YlZXgAAxQ2l.jpg?fit=300%2C200&ssl=1)