Bosi Nukta Africa atoa mbinu matumizi ya AI kukabiliana na habari feki 

February 14, 2025 5:50 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kwa kutumia zana za kidijitali kama Google Reverse Image, TinEye pamoja na InVid.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Habari na Teknolojia ya Nukta Africa Nuzulack Dausen amesema ni muhimu vyombo vya habari vikajifunza mbinu mpya za kukabiliana na habari za uongo ili kulinda uaminifu wa vyombo vya habari. 

Kwa mujibu wa Dausen hivi sasa kuna ongezeko kubwa la maudhui yanayozalishwa kwa kutumia akili unde ambapo baadhi ya maudhui hayo huwa ya kupotosha na baadhi ya vyombo vya habari huyatumia pasi na uhakiki.

Dausen aliyekuwa akizungumza katika siku ya pili ya Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji (ABC 2025) unaoendelea jijini Dodoma ameeleza kuwa maudhui ya uzushi yanayosambazwa  na vyombo vya habari si tu huwa ni kinyume cha sheria, bali pia yanahatarisha biashara kuu ya vyombo vya habari ambayo ni imani kwa hadhira yake.

“Mara nyingine bila kujua tunachapisha maudhui mtandaoni ambayo ni ya uzushi. kufanya hivyo ni kinyume cha sheria, lakini pia tunaathiri biashara yetu… Biashara yetu kuu tunayouza ni uaminifu,” amesema Dausen.

Kwa mujibu wa Dausen hivi sasa kuna ongezeko kubwa la maudhui yanayozalishwa kwa kutumia akili unde ambapo baadhi ya maudhui hayo huwa ya kupotosha, Picha | Kozica.

Njia za kuhakiki maudhui

Dausen ameleeza kuwa ni muhimu kujiuliza maswali kama vile ni lini picha au video hiyo ilichukuliwa?, Ilikuwa wapi? Na jambo gani lilitokea siku hiyo kabla ya kusambaza au kupakia maudhui hayo katika chombo chako cha habari.

Aidha, Dausen ameongeza kuwa mara nyingi picha na video hutumiwa nje ya muktadha wake jambo linaloweza kupotosha ukweli wa tukio ambapo mara nyingi watu hutumia picha au video zisizohusiana na habari husika kujaribu kuuaminisha umma kile walichokiandika.

Ili kuthibitisha maudhui hayo Dausen amewaambia wahudhuriaji kuwa wanaweza lkutumia zana mbalimbali za kidijitali ikiwemo Google Reverse Image Search, TinEye ambazo hufanya kazi ya kutoa taarifa za picha husika huku InVid yenyewe ikitumika kuhakiki video.

Kwa kutumia dhana mbalimbali za kidijitali ikiwemo Google Reverse Image unaweza kutambua ikiwa picha imetengenezwa kupitia AI, Picha Pcmag.com

Kwa kutumia programu hizo, watumiaji wanaweza kubaini mahali picha au video ilipopigwa, kuona tukio lililotokea wakati huo, pamoja na kutambua ni nani alikuwa wa kwanza kuipakia mtandaoni.

Hata hivyo, Dausen ameongeza kuwa picha au video zilizotengenezwa kwa akili unde mara nyingi haziwezi kuthibitishwa kupitia mifumo hii kwa sababu ni za kufikirika na hazina uhalisia wowote.

“Kuna wakati unaweza usipate matokeo kama hiyo picha imetengenezwa na AI, kwa sababu huwezi kuhakiki kitu ambacho hakipo. AI ni kitu cha kufikirika tu, si kitu halisi,” ameeleza kwa msisitizo.

AI, msaidizi au tishio?

Katika wasilisho lake la nne kuhusu matumizi ya akili unde katika kubaini maudhui ghushi Dausen alibainisha kuwa akili unde inaweza kuwa fursa au kitisho katika tasnia ya habari kutegemeana na namna itakavyotumika.

Kwa mujibu wa Dausen kusudio la kuanzishwa kwa akili unde ni kuleta suluhu ya changamoto mbalimbali ambapo katika tasnia ya habari inaweza kutumika katika uchakataji maudhui, uhariri, pamoja na usambazaji wa maudhui.

Akili unde inaweza kuwa fursa au kitisho katika tasnia ya habari kutegemeana na namna itakavyotumika,Picha | Digiexam.

Hata hivyo, Dausen ameonya kuwa AI inaweza kuwa changamoto ikiwa haitatumiwa vyema kwa sababu mpaka sasa baadhi ya watu wanatumia kutengenezea maudhui potofu kwa kutumia AI zenye uwezo wa kuiga sauti za watu wengine, kutengeneza simu feki, pamoja na kunakili sura za watu na kuzitumia kuzalisha maudhui potofu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks