MSD yasambaza vitakasa mikono lita 350,000, mahitaji yakizidi kuongezeka Tanzania

Nuzulack Dausen 1129Hrs   Machi 18, 2020 NuktaFakti
  • Bosi wa MSD asema kwa sasa hawana mpango wa kuingiza vitakasa hivyo kutoka nje
  • MSD yasema kuwa mahitaji yameongezeka mara tatu

Dar es Salaam. Bohari ya Dawa (MSD) imesema hadi sasa imeshasambaza vitakasa mikono (sanitisers) lita 350,000 kwa mashirika ya umma na taasisi mbalimbali nchini huku kukiwa na mahitaji zaidi ya  vimiminika hivyo muhimu katika kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa Corona.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD Laurean Bwanakunu ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa licha ya kusambaza vitakasa mikono hivyo bado kuna oda nyingi walizozipokea kutoka kwa wateja wao kutokana na mahitaji makubwa.

“Awali hatukuwa tumetarajia mahitaji yangefikia kiwango hiki. Mahitaji yametriple (yameongezeka mara tatu) kwa sababu ya hofu. Tunaendelea kutoa huduma kuhakikisha tunatimiza mahitaji hayo,” amesema Bwanakunu.

Amesema hadi sasa wana oda nyingi kutoka kwa wateja na wataweka vitakasa vyenye ujazo wa kawaida vikiwemo vya mililita 60 katika maduka yao yote nchi nzima ili vipatikane hadi kwa wananchi wa kawaida badala ya taasisi pekee.

Bosi huyo amesema miongoni mwa oda walizonazo kwa sasa ni vitakasa vilivyopo kwenye vifungashio vya lita 5 vipatavyo 50,000 sawa na lita 250,000, sanitisers za mililita 250 uniti 130,000; na sanitisers dispensers (vitoa vitakasa mikono) 100,000.  


Soma zaidi:


Amesema MSD kwa kawaida husambaza vitakasa mikono hivyo kwa taasisi za afya lakini mahitaji ya sasa yamepaa kwa kuwa kila mtu anahitaji kwa ajili ya kujikinga na virusi vya corona.

Tanzania ina visa vitatu vya virusi vya corona hadi leo hii (Machi 18, 2020). 

Alipoulizwa iwapo wana mpango wa kuingiza vitakasa hivyo kutoka nje ya nchi, Bwanakunu amesema kwa sasa viwanda vya ndani bado vina uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko.

“Kwa sasa tutaendelea kununua vitakasa vya ndani kwa kuwa viwanda vya ndani bado vina uwezo wa kuzalisha vitakasa hivyo na kukidhi mahitaji. Hapo baadaye ikitokea vimeshindwa kabisa kukidhi mahitaji ndipo tutaangalia uwezekano wa kuagiza nje lakini siyo kwa sasa,” amesema.

Mapema leo baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam waliiambia Nukta kuwa vitakasa hivyo vimekuwa adimu katika maduka ya kawaida na vinapopatikana vinauzwa bei ya juu.

“Hizo sanitisers (vitakasa) na masks (barakoa) zimekuwa mtaji huko mtaani havipatikani kila na ni bei ghali kwa sisi wa hali ya chini. Serikali itusaidie tuweze kuvipata kwa bei nafuu,” amesema Idrissa Rajabu, dereva wa bodaboda Victoria jijini Dar es Salaam.

Vitakasa vimekuwa moja ya bidhaa adimu katika maduka mbalimbali ya dawa na maduka makubwa (supermarkets) jijini hapa kutokana na watu kununua kwa wingi ndani ya juma hili.

Related Post