WHO: Njia ya kumaliza Corona ni kuvunja mnyororo wa maambukizi

Mwandishi Wetu 0202Hrs   Machi 17, 2020 Habari
  • Yasema hilo linawezekana ikiwa nchi zitaongeza nguvu ya upimaji watu kudhibiti visa vipya.
  • Pia watakaobainika kupata maambukizi watenge na watu wengine mpaka wapone.
  • Tanzania nayo yathibitisha kuwa na mgonjwa wa kwanza wa virusi vya Corona.

Dar es Salaam. Wakati virusi vya corona (COID-19) vikiendelea kusambaa sehemu mbalimbali duniani na kuongeza idadi ya vifo, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema huu ni wakati wa kuongeza kasi ya upimaji ili kudhibiti visa vipya.

Takwimu za WHO za jana zinaeleza kuwa watu 167,511 wameambukizwa ugonjwa huo huku waliofariki wakifikia 6,606.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kuhusu COVID-19, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedross Ghebreyesus amesema hatua mbalimbali za kuridhisha zinaendelea kuchukuliwa lakini upimaji bado haujawekewa msisitizo.

”Tumeshuhudia hatua mbalimbali zikichukuliwa ikiwemo kujitenga, kufunga shule, kufuta matukio ya michezo na hata mikusanyiko.

”Lakini hatujashuhudia hatua za kutosha za katika upimaji, kuwaweka watu sehemu maalum na kufuatia waliokutana na wagonjwa kitu ambacho ni cha muhimu sana katika kukabiliana na maambukizi,” amesema bosi huyo.

Ameongeza kuwa hatua za kunawa mikono, kujitenga na matukio ya mikusanyiko ya kijamii kutasaidia kupunguza maambukizi na kuiwezesha mifumo ya afya kukabiliana na hali hiyo.


Zinazohusiana


Hata hivyo, amesisitiza kuwa hatua hizo pekee hazitoshi kumaliza mlipuko huo kwa sababu ni mchanganyiko wa hatua ndiYo unaoleta mabadiliko.

“Kama ninavyoendelea kusisitiza kwamba nchi zote zinapaswa kuchukua mtazamo wa kina wa hatua, lakini njia bora zaidi ya kuzuia maambukizi na kuokoa maisha ni kuvunja mnyororo wa maambukizi  na ili kufanikisha hilo ni lazima upime na kutenga watu.

”Huwezi kupambana na ugonjwa huu kama hujui nani ameambukizwa,” amesema Dk Tedross.

Dk Tedross amesema nchi zote duniani kuhakikisha zina  “pima, pima, pima , pima kila kisa kinachoshukiwa” na kuongeza kuwa endapo watabainika wana virusi hivyo , basi watenganishwe na wengine.

Hadi kufikia sasa, WHO imeshasafirisha vifaa vya upimaji milioni 1.5 kwa nchi 120.

Tanzania imekuwa nchi ya tatu Afrika Mashari baada ya Kenya na Rwanda kuthibitisha kuwepo kwa mgonjwa wa virusi vya Corona huku wananchi wakitakiwa kuchukua tahadhari kujikinga na maambukizi mapya.

Related Post