BOT yafuta vibali vya ‘Apps’ 69 zinazotoa mikopo mtandaoni

November 21, 2024 2:30 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Mkopo fasta,KOPAHAPA, Nikopeshe App, Kwanza loan.
  • BOT imeutahadharisha umma kutojihusisha na “Applications” hizo.

Arusha. Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imefuta vibali vya uendeshaji vya programu tumizi (application) 69 zinazotoa mikopo mtandaoni kwa kukiuka masharti ya leseni za utoaji wa huduma hizo ikiwemo kutolinda faragha za wateja.

Taarifa ya Emmanuel Tutuba, Gavana Mkuu wa BOT iliyotolewa leo Novemba 21, 2024 inaeleza kuwa Apps hizo zimefungiwa kutokana na kushindwa kukidhi matakwa ya Mwongozo kwa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili wanaotoa huduma za mikopo kwa njia ya kidijitali wa mwaka 2024 uliotolewa na Agosti 27 mwaka huu.

“Mwongozo huo unalenga kuimarisha usimamizi wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha Daraja la Pili nchini na kuhakikisha uzingatiwaji wa Kanuni za kumlinda mlaji wa duduma za fedha, ikijumuisha uwazi, uwekaji wa tozo na riba, njia za ukusanyaji wa madeni, na utunzaji wa taarifa binafsi za wateja na kulinda faragha zao…

…Kupitia taarifa hii, Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuarifu Umma kwamba Majukwaa na Programu Tumizi “Applications” zifuatazo hazina kibali na haziruhusiwi kuendelea na shughuli za utoaji mikopo kidijitali,” imesema taarifa ya Tutuba.

Miongoni mwa application zilizofungiwa ni pamoja na Mkopo fasta,KOPAHAPA, Nikopeshe App, Kwanza loan. Nufaika Loans, BoBa Cash, Bolla Kash – Bolla Kash Financial Credit na Hi Cash.

Taarifa ya BOT inakuja wakati kukiwa na ongezeko la application hizo zinazotoa mikopo mtandaoni huku baadhi zikilalamikiwa kutolinda faragha za wateja wao pamoja na kuweka viwango vikubwa vya riba vilivyoifanya mikopo hiyo kupewa majina mbalimbali ikiwemo kausha damu.

Aina hiyo ya mikopo iliibua hoja mseto katika Bunge la Tanzania hali iliyofanya Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba, Mei 2 mwaka huu kuahidi kulifanyia kazi jambohilo kwa kina.

“Ili tuweze kuboresha zaidi, nitafanya semina ya wawakilishi wa wanachi na taasisi za kifedha ili tukubaliane kuhusu jambo hili…. Tukubaliane ili wabunge waziambie taasisi zangu zote namna gani wanataka sheria zisimamie maslahi ya wananchi wanaowawakilisha,” alisema Nchemba.

Aidha, BOT imeutahadharisha umma kutojihusisha na majukwaa na “Applications” hizo huku ikiahidi kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzifungia programu hizi ili kuepusha umma kutumia huduma za fedha zisizokuwa na vibali vya mamlaka husika.

Enable Notifications OK No thanks