HESLB yawapangia mkopo wanafunzi 2,177 waliokata rufaa 2023-24
- Jumla ya wanufaika wa mwaka wa kwanza yafikia 76,261
- Sh221 bilioni zagawanywa kwa wanufaika.
Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imewapangia mikopo wanafunzi 2,177 waliokata rufaa kwa mwaka wa masomo 2023/2024.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na HESLB (jana) Disemba 4, 2023 wanafunzi hao waliopangiwa mikopo yenye thamani ya Sh7.2 bilioni ni wale waliokata rufaa kwa kujaza na kuwasilisha taarifa zao katika bodi hiyo.
“HESLB imewapangia mikopo wanafunzi…baada ya kuwasilisha maombi ya rufaa kwa mwaka wa masomo 2023/2024 kwa kujaza taarifa na kuwasilisha nyaraka za kuthibitisha uhitaji wao,” inasomeka sehemu ya taarifa ya HESLB.
Soma zaidi:Idadi ya waliofariki Katesh yafika 63
Itakumbukwa HESLB ilitangaza kufungua dirisha la maombi ya rufaa kwa wale ambao hawakupangiwa kabisa mikopo au ambao hawakuridhishwa na viwango walivyopangiwa Novemba 8 – 17, 2023.
Wanafunzi 2,177 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 7.26 bilioni baada ya kuwasilisha maombi ya rufaa kwa mwaka wa masomo 2023/2024 kwa kujaza taarifa na kuwasilisha nyaraka za kuthibitisha uhitaji wao.
Tembelea SIPA kupara taarifa zaidi.#WeweNdoFuture
#TimizaWajibu
pic.twitter.com/vIm8KXIzIT— HESLB Tanzania (@HESLBTanzania) December 4, 2023
Idadi ya wanafunzi waliopata mikopo kutokana na rufaa inafanya HESLB kuwa na wanufaika 76,261 wa mwaka wa kwanza waliodahiliwa katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizopo nchini ambapo wametumia jumla ya Sh221.2 bilioni.
“Kati ya wanafunzi 76,261 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo, wanafunzi wa kiume ni 43,468 (asilimia 57) na wa kike ni 32,794 (asilimia 43),” Imeongeza HESLB.
Katika awamu hizo za mikopo kabla ya rufaa wanafunzi 74,084 wa shahada ya kwanza walipangiwa mikopo yenye thamani ya Sh214 bilioni katika awamu tatu zilizotangazwa Oktoba 20, 27 na Novemba 2, mwaka huu.
Latest