Bodi ya mikopo yafungua dirisha kukata rufaa wanafunzi waliokosa mikopo

November 14, 2022 5:14 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Litakuwa wazi kwa siku saba.
  • Wengine wanaoweza kukata rufaa ni wasioridhishwa na viwango walivyopangiwa.
  • Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 68,422 wamepangiwa mikopo.

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imefungua dirisha la rufaa ili kutoa fursa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ambao hawakuridhika na viwango vya mikopo walivyopangiwa kuwasilisha taarifa za uthibitisho ili kuongezewa viwango vya mikopo kulingana na uhitaji wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema dirisha hilo la rufaa litakuwa wazi kwa siku saba kuanzia Novemba 13 hadi 20 mwaka huu na kuwa rufaa kutoka kwa wanafunzi zinapaswa kuwasilishwa kwa njia ya mtandao.

“Hadi leo (Novemba 13, 2022), tumeshawapangia mikopo wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 68,422 na tunafahamu kuwa kuna wanafunzi ambao kwa sababu mbalimbali, hawakukamilisha nyaraka muhimu kuthibitisha uhitaji wao, dirisha la rufaa ni fursa kwao,” amesema Badru katika yake iliyotolewa Novemba 13, 2022.

Kwa mujibu wa Badru, lengo ni kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya 71,000 katika mwaka wa masomo 2022/23 na kuwasihi wanafunzi wanaowasilisha rufaa kusoma na kuzingatia maelekezo yaliyopo kwenye mfumo wa kuwasilisha rufaa.

Tangua bodi ya mikopo ianze kutoa mikopo mwezi uliopita kumekuwa na mjadala wa wanafunzi wenye sifa kupangiwa viwango vidogo vya mikopo na wengine kukosa kabisa. 

Malipo ya fedha kwa waliopangiwa

Kuhusu malipo, Badru amesema fedha zilianza kutumwa vyuoni hata kabla ya wanafunzi kufika vyuoni na kuwa kazi hiyo ni endelevu na kuwashauri wanafunzi waliopangiwa mikopo kufika kwa maafisa mikopo wa vyuo vyao ili kukamilisha taratibu za kupokea fedha.

“Pale mwanafunzi anapoona amepangiwa mkopo kupitia akaunti yake ya SIPA (Student’s Individual Permanent Account), basi afike kwa afisa mikopo wa chuo chake ambaye yupo palepale chuoni ili awasilishe taarifa zake za benki na kupokea fedha,” amesema Badru.

Badru amezishukuru taasisi za elimu ya juu na serikali za wanafunzi kwa ushirikiano wanaoipatia HESLB ambao umeendelea kuimarisha ufanisi katika kuwahudumia wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali. 

“Kwenye huu mnyororo wa kuwahudumia wanafunzi, uongozi wa vyuo, serikali za wanafunzi na jumuiya yao ya TAHLISO ni wadau muhimu na wamekuwa wakitupatia ushirikiano mkubwa, tunawashukuru sana,” amesema Badru.

HESLB ilipanga  kutoa mikopo yenye thamani ya kiasi cha Sh570 bilioni kwa mwaka wa masomo 2022/23.

Kutokana na malalamiko juu ya ufanisi wa HESLB, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda aliunda tume ya wataalamu ambao watachunguza ufanisi wa bodi hiyo katika ugharamiaji wa elimu ya juu kwa wahitaji.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW