Deni la Tanroads kitendawili kingine Serikali ya Rais Samia

February 7, 2024 5:14 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Deni hilo la Sh6.37 trilioni ni mara mbili ya bajeti ya iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
  • Kwa bajeti ya Wizara ya ujenzi huenda ikachukua miaka mitano kulipa deni hilo kama bajeti yote itatumika kulipa deni tu.

Dar es Salaam. Hapana shaka kuwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) utakuwa na kibarua kigumu cha kulipa madeni ya zaidi ya Sh6 trilioni yanayohusisha fidia za watu wanaopisha barabara na wakandarasi iwapo itataka kumalizana nao ndani ya muda mfupi kutokana na kiwango hicho kuwa kikubwa kuliko ‘kibubu’ chake.

Kwa mujibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu hadi kufikia Desemba mwaka 2023, Tanroads ilikuwa inadaiwa jumla ya Sh6.37 trilioni na watu mbalimbali ikiwa ni madeni ya fidia na malipo ya makandarasi na wahandisi washauri wa ndani na nje ya nchi.

Kamati hiyo ililieleza Bunge jana (Februari 5, 2024) kuwa kati ya fedha hizo, Sh778 bilioni ni fedha zinazodaiwa na wakandarasi na wahandisi washauri, huku Sh5.59 trilioni zikiwa ni fidia inayohitajika kulipwa kwa wamiliki wa maeneo yote nchini yanayotakiwa kupitiwa na barabara kuu na za mikoa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Selemani Kakoso alitahadharisha Serikali kulipa deni hilo kwa wakati ili kuepuka kuongezeka kwa gharama za deni kama taratibu za miradi zinavyosema.


Soma zaidi:Watoto wadogo katikati ya kuisaka elimu madarasa ya awali Tanzania-2


Licha ya Kakoso kuonya ucheleweshaji huo, uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa huenda ulipaji wa madeni hayo ukachukua muda mrefu kwa kuwa kiwango kinachodaiwa ni takriban mara mbili ya jumla ya bajeti za wizara za ujenzi na uchukuzi kwa mwaka 2023/24.

Juni mwaka jana Bunge liliidhinisha bajeti ya Sh3.5 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2023/24. Kati ya fedha hizo, Sh1.4 trilioni ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi na Shilingi 2.08 trilioni kwa ajili ya sekta ya uchukuzi.

Ni deni pasua kichwa

Hii ina maana kuwa iwapo Tanroads itatekeleza ulipaji wa madeni hayo ndani ya miaka miwili ijayo, basi Serikali italazimika kuhamishia matumizi ya bajeti zote za ujenzi na uchukuzi kumalizana na makandarasi, washauri elekezi na watu wanaodai fidia kupisha miradi ya barabara. 

Kwa kuwa kwa sasa Tanroads ipo chini ya Wizara ya Ujenzi, na ikiwa Sh1.4 trilioni iliyotengwa kwa ajili ya sekta ya ujenzi ndio bajeti ya wizara mpya ya ujenzi maana yake Serikali itatumia miaka mitano kulipa deni hilo ikiwa bajeti nzima ya wizara itaelekezwa kwenye deni tu.


Read more: From sunlight to harvest: Solar energy brings hopes to farmers in Iringa


Aidha uchambuzi zaidi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa deni la Tanroads ni sawa na asilimia 14.3 ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambapo Bunge liliidhinisha kukusanya na kutumia Sh44.36 trilioni hadi ifikapo Juni mwaka huu.

Jana Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliliambia Bunge kuwa Serikali imejiwekea utaratibu wa kupunguza madeni hayo na mwezi huu wa pili wameendelea kulipa Sh50 bilioni na Sh115 bilioni zitalipwa hadi kufikia Aprili mwaka huu.

Itakumbukwa kuwa Novemba 21, 2023, Waziri Bashungwa na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba walikutana na Umoja wa Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi (Tucasa) na kuahidi kuwalipa wale wanaozidai Tanroads na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura).

Kwa kuwa zaidi ya asilimia 90 ya deni la Tanroads ni kwa ajili ya fidia, wananchi wengi huenda wakaathirika kwa kucheleweshewa stahiki zao au kutolipwa kwa wakati iwapo watatoa maeneo yao kwa ajili ya miradi inayoendelea.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya uchumi wameishauri Serikali kutupia macho kwanza deni la wakandarasi pamoja na washauri ili kuepukana na riba inayoongezeka siku hadi siku huku ikifanyia kazi upatikanaji wa fedha kwa ajili ya fidia za wanaopisha barabara.

‘Bora walipwe wakandarasi kwanza’

Dk. Isaack Safari, Mchambuzi wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) ameiambia Nukta Habari kuwa ni vyema Serikali ikatoa kipaumbele ulipaji wa deni la wakandarasi kwa kuwa hukua kwa kiwango fulani cha riba kwa mujibu wa makubaliano.

“Kwenye hii mikataba huwa kuna masharti ya malipo, ambayo huhusisha riba pale muda uliowekwa wakati wa makubaliano unapopitiliza, suala kubwa hapa ni wapi Serikali itatoa hizo fedha na athari zitakazotokea zitakapoingizwa kwenye mzunguko, lakini ni muhimu ikatizama deni hilo klwa kipaumbele kuepuka riba kuongezeka zaidi,” amebainisha Dk Safari.

Safari ameongeza kuwa kwa sababu barabara ni kiungo muhimu kwa shughuli za kiuchumi hususan katika mataifa yanayoendelea kama Tanzania, ni vyema Serikali ikaingia makubaliano maalumu na watu wanaopaswa kupisha miradi ya barabara ili shughuli za ujenzi ziendelee wakati wao wakilipwa taratibu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa muongozo wa uthamini wa fidia uliotolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mwaka 2016, fidia ni malipo yanayotolewa kwa mtu au taasisi kama mbadala wa mali yake kutokana na kuondolewa kwenye eneo lake lililotwaliwa kwa manufaa ya umma na kupangiwa matumizi mengine tofauti na yale yaliyopo kwa sasa.


Soma zaidi : Tanzania na mtihani wa kuongeza matumizi ya nishati jadidifu ifikapo 2025


Malipo ya fidia yawe ya haki

Muongozo huo unafafanua kuwa pale ambapo ardhi inayohitajika imetwaliwa kwa ajili ya miradi au shughuli za maendeleo ya taifa zinazofanywa na Serikali, taasisi au mamlaka yeyote ya Serikali au binafsi, kijiji au mtu basi mmiliki wa asili wa ardhi hiyo, stahili yake ni kulipwa fidia.

Pamoja na Sheria ya Utwaaji kuelekeza Serikali kuwajibika kulipa fidia pale ardhi inapotwaliwa kwa ajili ya miradi yake, Sheria ya Ardhi (Sura 113) inapigilia msumari zaidi kuwa fidia hiyo ni lazima iwe kamilifu, ya haki na ilipwe kwa wakati.

Madeni hayo ya Tanroads yanazidi kuongeza mzigo kwa Serikali ambayo tayari hadi kufikia April 2023 deni lake lilifikia Sh79.1 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 13.9 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati wa uwasilishaji wa Hali ya Uchumi kwa mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2023/24 kati ya deni hilo la Serikali, la nje ni Sh51.16 trilioni huku lile la ndani ni Sh27.93 trilioni.

/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
5 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
5 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV