Wabunge wacharuka utekelezaji bajeti Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
Maendeleo ya ujenzi wa daraja jipya la Wami unavyoendelea ambapo ujenzi wa daraja hili unatarajiwa kugharimu Sh72 bilioni ambapo linatarajia kukamilika na kutumika Novemba Mwaka 2022. Picha| Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
- Ni kutokana na kutotekelezwa kwa baadhi ya miradi ya miundombinu majimboni kwao
- Baadhi wahoji uhalali wa kampuni moja kupewa tenda nyingi zisizokamilika.
Dar es Salaam. Licha ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2022/23 kuongezeka kwa Sh119.3 bilioni, hotuba ya bajeti hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na Wabunge huku baadhi wakilalamikia kutokamilika kwa miradi iliyopangwa kutekelezwa katika bajeti iliyopita.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa aliyewasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao amesema wanapanga kutumia Sh3.8 trilioni ikiwa imeongezeka kutoka Sh 3.7 trilioni ya mwaka fedha 2021/22.
Ongezeko la bajeti hiyo inayoendelea kujadiliwa na wabunge imeongezeka kwa Sh119.3 bilioni
Kati hiyo fedha, Prof Mbarawa amesema sh 1.4 trilioni zitaelekezwa katika sekta ya ujenzi huku kiasi kilichobaki kitaenda katika sekta ya uchukuzi ikiwemo kukamilisha miradi ya ujenzi wa bandari,ujenzi wa reli na viwanja vya ndege.
Hata wakati Prof Mbarawa akipendekeza bajeti ya 2022/23, mpaka kufikia Aprili mwaka huu, wizara yake ilikuwa imepokea Sh1.5 Trilioni sawa na asilimia 96.5 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge la Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Wabunge wacharuka
Mara ya baada ya Waziri kumaliza kusoma hotuba, wabunge wamepata fursa ya kuchangia bajeti hiyo huku wengi wao wakilia kutokukamilika kwa miradi ya miundombinu katika majimbo yao.
Miradi wanayoilalamikia wabunge hao ni ile iliyopangwa kutekelezwa katika bajeti ya mwaka huu unaoisha Juni 30, 2022 zikiwemo baadhi ya barabara ambazo zimechukua muda mrefu kukamilika.
Soma zaidi:
Mbunge wa jimbo la Ukonga, Jerry Slaa ameikosoa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kutoa miradi mingi ya ujenzi ya miundombinu kwa kampuni moja ambayo baadhi ya miradi yake haikujengwa kwa ubora na mingine kutokamilika, ukiwemo mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya pili ambao ubora wa barabara ulilalamikiwa na wadau jijini Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Spika Bunge lako hili na wewe ukiwa spika ndilo litakuwa Bunge ambalo limesimamia bajeti hii ambayo inakwenda kututengenezea kero ambayo iko Mbagala, iko Temeke inakwenda kurejeshwa tena Gongo la Mboto na maeneo mengine tutakuwa ni bunge la namna gani?,” amehoji Slaa.
Katika maeneo hayo, amesema kuna changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara kutokana na ongezeko la watu.
Bona Kamoli, Mbunge wa Segerea amehoji uhalali wa baaadhi ya watumishi wa Serikali kuhamisha matumizi ya fedha zilizopitishwa na Bunge bila kuwashirikisha akisema jambo hilo si sawa kwa sababu wao ndiyo wanawasilisha kero za wananchi bungeni.
Hoja hiyo imetokana na kuwepo kwa taarifa za kuhamishwa kwa fedha zilizoongezwa na Rais katika bajeti ya Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) mwaka 2021/22 kwenda kutumika katika zoezi la uwekaji wa anwani za makazi.
“Mimi nilipata taarifa kutoka kwa watendaji wangu wa Tarura kwamba pesa tulizokuwa tunazitegemea kwenye jimbo letu Sh800 milioni sasa zinaelekezwa kwenye Postikodi…” amebainisha Kamoli.
Tangazo:

Naye Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatey Massay amelalamikia kutotekelezwa kwa ujenzi wa barabara ya Karatu-Haidom yenye umbali wa kilomita 25 ambayo ilitengewa bajeti mwaka 2021/22 na imekuwa katika ilani nne za uchaguzi za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“…tumepeleka kwenye ilani ipo kwenye ilani, ilani zote nimewaeleza, sauti zao umewasikia ninazo hapa, hansard kule maneno yao yapo hapa ukitaka Mhe Spika nakuletea, wamezungumza hawa wakubwa zangu, maswali nimeuliza kwa mwaka jana mara saba, mwaka huu mara nne, Mhe Spika nafanyaje hapa nisaidie,” amehoji Massay kwa uchungu.
Kutokana na hoja mbalimbali za Wabunge kuhusu miundombinu hasa ya ujenzi, Prof Mbarawa anatarajia kuzitolea ufafanuzi atakapokuwa anahitimisha mjadala wa bajeti hiyo.
Huenda, majibu ya waziri huyo yakaleta ahueni katika maeneo yenye changamoto za miundmbinu nchini Tanzania.
Latest