Zaidi ya nusu ya bajeti Wizara ya Fedha kulipa deni la Serikali

June 7, 2022 2:48 pm · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni bajeti ya mwaka 2022/23 ambayo itakuwa Sh14.9 trilioni.
  • Sh9.09 trilioni kulipa deni la Serikali.
  • Kamati yashuari liundwe fungu maalum la deni la Serikali.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/23 inakadiria kutumia bajeti ya Sh14.9 trilioni huku zaidi ya nusu ya fedha hizo zitatumika kulipa deni la Serikali. 

Bajeti ya wizara hiyo ndiyo bajeti ya kiwango cha juu kuliko bajeti zote zilizowasilishwa katika Bunge la bajeti la mwaka huu. 

Dk Nchemba katika hotuba yake ya bajeti iliyowasilishwa leo (Juni 7, 2022) Bungeni jijini Dodoma amesema bajeti hiyo itagawanywa katika mafungu nane kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. 

Dk. Mwigulu ameliambia Bunge kuwa kati ya kiasi hicho cha fedha, Sh13.6 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh1.32 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.  

Hata hivyo, sehemu kubwa ya fedha hizo zitatumika kulipa deni la Serikali ambalo linaongezeka kila mwaka.

Kwa mujibu wa waziri huyo amesema Sh9.09 trilioni sawa na asilimia 60.8 zitatumika kulipa deni la Serikali. 

Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa 2022/23 imeongezeka kwa Sh2.55 trilioni kutoka Sh12.9 trilioni ya mwaka huu unaoisha mwezi Juni.


Soma zaidi:


“Fungu jipya la deni liundwe”                                  

Kamati ya Bunge ya Bajeti imependekeza kuundwa kwa fungu jipya la deni la serikali ili kusiwepo na mkanganyiko kwa sehemu kubwa ya wizara hiyo kutumika kulipa deni kila mwaka. 

“Hatua hiyo itaondoa mkakanyiko uliokuwepo wa kujumuisha madeni ya serikali na huduma za mfuko wa serikali,” amesema Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Omari Kigua.

Enable Notifications OK No thanks