DCEA yataifisha mali za Sh 3.3 bilioni za watuhumiwa biashara dawa za kulevya 

December 3, 2025 3:45 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Mali zilizotaifishwa ni pamoja na apartment, nyumba na magari.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetaifisha mali zenye thamani ya Sh3.3 bilioni zinazomilikiwa na watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya.

Taarifa iliyotolewa leo Desemba 3, 2025 na Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo inaeleza kuwa uamuzi huo umefikia baada ya kuridhiwa na Mahakama kuu divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Lyimo amesema maombi ya kutaifishwa kwa mali hizo yaliwasilishwa mahakamani hapo baada ya kufanyika kwa uchunguzi na kubaini watuhumiwa hao wanamiliki mali zilizopatikana kwa njia za uhalifu wa biashara ya dawa za kulevya.

MDMA ni dawa iliyotengenezwa kiufundi katika kundi la amphetamines. Inapangiwa kama dawa ya empathogenic. Picha/ Magenta drug test.

“Utaifishaji wa mali hizo umefanyika chini ya Sheria ya Mazao ya Uhalifu Sura ya 256 ikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura ya 200 na Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015,” amesema Lyimo.

Lyimo amesema miongoni mwa mali zilizotaifishwa ni pamoja na nyumba, viwanja na magari zinazomilikiwa na watuhumiwa Saleh Khamis Basleman na Gawar Bachi Fakir.

Aidha, Lyimo ameeleza utaifishaji wa mazalia ya uhalifu umewekwa kisheria ili kuifundisha jamii kuwa uhalifu hauna faida na adhabu za kifungo hazitoshelezi kutokomeza uhalifu hasa katika makosa ya kupangwa ikiwemo makosa ya dawa za kulevya. 

Hata hivyo, katika operationi nyingine Jijini Dar es Salaam DCEA, katika eneo la Sinza D, iliwakamata Cuthbert Kalokola (34) na Murath Abdallah (19) wakiwa na dawa mpya za kulevya aina ya 3,4 – Methylenedioxymethamphetamine (MDMA) vidonge 738 vyenye uzito wa gramu 177.78 na dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Rohypnol (flunitrazepam) vidonge 24 vyenye uzito wa gramu 10.03.
Kulingana na ufafanuzi uliotolewa na DCEA, katika operesheni zilizofanyika mikoa mingine nchini, zilikamatwa kilogramu 2,041.45 za bangi, kilogramu 1,423.28 za mirungi na ekari 18 za mashamba ya bangi ziliteketezwa huku magari manne na pikipiki 12 pamoja na watuhumiwa 84.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks