Chadema kukata rufaa hukumu ya Lissu
- Yaeleza kuwa itaomba na dhamana kwa kuwa kesi hiyo ina dhamana hata kama amekutwa na hatia.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa kitakata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kumfunga jela miaka minne mwenyekiti wao Tundu Lissu kwa kosa la uchochezi, hatua itakayoanzisha safari nyingine ya kiongozi huyo kupigania uhuru wake kutoka gerezani.
Leo Novemba 6, 2026 jopo la majaji watatu wakiongozwa na Dunstan Ndunguru wa mahakama hiyo Masjala ndogo ya Dar es Salaam, limesema walikosa ushahidi katika kesi ya uhaini dhidi ya Lissu
Awali Lissu alishtakiwa kwa kosa la uhaini kutokana na maneno aliyatamka April 3, 2025 jijini Dar es Salaam kwa kuazimia kuhamasisha umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2025 na kuonyesha hia hiyo kwa kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lissu alikana mashtaka hayo.
Hata hivyo, katika hukumu iliyotolewa leo majaji hao wamemkuta Lissu na hatia katika kosa la uchochezi likiwa ni kosa dogo mbadala wa uhaini baada ya ushahidi uliowasilishwa kuonyesha uwepo wa jinai ya kuwachochea watu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
“Sisi kama mawakili tunaomsaidia Mwenyekiti Tundu Lissu, tutakaa naye na leo ameonyesha kabisa ana nia ya kukata rufaa,” Rugemeleza Nshala, Mwanasheria Mkuu wa Chadema amewaambia wanahabari na wafuasi wa chama hicho katika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Licha ya yote yaliyotokea, amesema bado wana imani na wataenda mahakamani kwa kuwa wana nafasi ya kukata rufaa na kuandika sababu na kasoro zilizojitokeza.
“Tutaomba vile vile dhamana wakati tunasubiria rufaa kwa sababu ni kosa linalodhaminika hata kama umekutwa na hatia,” amesema.
Katika mkutano huo, Dk Nshala ameonyeshwa kushangazwa na uamuzi wa majaji kuhusu kosa dogo akieleza kuwa kama alivyosema Lissu kuna mazingira bayana kuwa ilikuwa ni kesi ya kisiasa.
“Wewe unasema umeingilia haki za watu za kupiga kura. Ni ushahidi gani unaosema haki yao ya kupiga kura imekiukwa na nani alileta ushahidi aliyesema haki yake ya kupiga kura imekiukwa,” amesema.
Hii ni mara ya kwanza vigogo wa Chadema wanazungumza na wanahabari tangu hukumu hiyo iliyopotolewa mchana wa leo.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema John Heche amesema watakaa vikao vikiwemo vya Sekretarieti, viongozi wakuu na hata ikiwezekana kamati kuu ya chama hicho itaketi na kisha baadaye watatoa muongozo wa kinachofuata.
Hakuna kupiga magoti
Heche ametupilia mbali mwito wa maridhiano katika mazingira ambayo kiongozi wao yupo jela.
“Wale waliotaka kupiga magoti Mwenyekiti wetu amesema hakuna kupiga magoti. Hakuna kupiga magoti kwenye uovu. Nataka kuwaambia tutashinda, ‘very soon’ (siyo muda) tutashinda. Hii ni njia ya Mungu, Mungu ametuchagulia tupite njia hii na ni njia ya ushindi,” amesema Heche.
“Msiogope, muwe imara, tunasonga na tutatoboa…Wanachadema nchi nzima msikubali kugawanyika, msikubali wala msidanywe, tupo katika njia sahihi. Hii ni njia ambayo watu walioandika historia duniani wameipita. Ushindi wowote ‘meaningful’ unapiganiwa,” amesema kiongozi huyo wa juu kwa sasa kutokana na Lissu kuwa jela.
Heche amesema hakuna majadiliano yeyote ya maana yatakayofanyika bila kiongozi wao kuwa nje.
ACT Wazalendo wasema ni siku ya giza
Mbali na Chadema, Chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo nacho kimesema kuwa leo ni siku ya giza baada ya hukumu hiyo kutolewa dhidi ya Lissu, ambayo baadhi ya wadau wa haki za binadamu wanasema inatoa ishara kuwa inazorotesha misingi ya demokrasia.
“Leo ni siku ya giza kwa utawala wa sheria, demokrasia na haki za binadamu nchini Tanzania. Hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania ya kumtia hatiani Mwenyekiti wa CHADEMA, Ndugu Tundu Lissu kwa kosa la uchochezi ni ushahidi mwingine wa namna demokrasia inavyoendelea kukandamizwa nchini,” amesema Dorothy Jonas Semu, Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo.
Amesema tangu Lissu alipokamatwa, chama chao kiliweka bayana msimamo wake kuwa Lissu si mhaini na kwamba kesi iliyokuwa ikimkabili ililenga kumnyamazisha na kumzima kisiasa.
Kutokana na hukumu iliyotolea leo, msimamo wa ACT Wazalendo amesema unabaki pale pale kuwa Lissu ameonewa kwa sababu za kisiasa.