Lissu ahukumiwa miaka minne jela kwa kosa la uchochezi

November 6, 2026 1:22 pm · Waandishi Wetu
Share
Tweet
Copy Link
  • Mahakama Kuu ya Tanzania yasema hakuna ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kwenye kesi ya uhaini.
  • Ni baada ya kusota siku zaidi ya 575 mahabusu akisubiri hukumu ya kesi ya uhaini.
  • Yamhukumu kwa kosa dogo mbadala linalofanana na uhaini baada ya ushahidi kubainisha kuwa kulikuwa na jinai katika matamshi yake yaliyowachochea watu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani ikiwemo kuzuia uchaguzi.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imemhukumu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu kifungo cha miaka minne jela baada ya kukutwa na hatia ya kosa la uchochezi, uamuzi unaomwingiza kiongozi huyo katika historia ya kukutwa na jinai. 

Awali Lissu alishtakiwa kwa kosa la uhaini kutokana na maneno aliyatamka April 3, 2025 jijini Dar es Salaam kwa kuazimia kuhamasisha umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2025 na kuonyesha hia hiyo kwa kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lissu alikana mashtaka hayo.

Lakini katika hukumu iliyotolewa leo Novemba 6, 2026 na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Dunstan Ndunguru, mahakama hiyo Masjala ndogo ya Dar es Salaam, limesema hakuna ushahidi wowote usioacha shaka uliobanisha kuwa aliyoyasema Lissu ni uhaini. 

“Treason per se haikuthibitishwa bila kuacha shaka,” amesema Jaji Ndunguru. 

Hata hivyo, amesema mahakama ina jukumu kisheria kutathmini kama kuna kosa dogo linaloweza kuwa ni mbadala wa kosa kubwa lenye jamii ya hilo la uhaini kutokana na ushahidi uliokuwepo. 

Jaji Ndunguru amebainisha kuwa  baada ya kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo hapana shaka kuwa maneno hayo yalitamkwa na mshtakiwa hakuyakana na hayakubishaniwa. 

Baadhi ya mashahidi, Jaji Ndunguru amesema waliieleza mahakama kuwa walihamasika na kauli ya kufanya uasi kiasi cha kuanza kupanga kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani ikiwemo kuzuia uchaguzi. 

Kutokana na ushahidi huo, mahakama imemtia hatiani Lissu kwa uchochezi kama kosa dogo mbadala linalohusiana na kosa kubwa la uhaini kwa kuwa kuzuia uchaguzi ni kukiuka katiba ya nchi inayompa mtu “haki ya kupiga kura, kuchagua na kuchaguliwa”. 

Kabla ya kusomwa hukumu, Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa Lissu kwa kile alichoeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la watu kutenda makosa ya uchochezi nchini kwa maslahi yao binafsi yanayoleta athari za kisiasa, kiuchumi na kijamii ikiwemo kupoteza uhai wa watu. 

Lissu akataa kuomba msamaha

Katika utetezi wake, Lissu amesema hawezi kuomba msamaha kwa sababu wasiokuwa na hatia huwa hawaombi msamaha.

“You don’t seek forgiveness if you are innocent (Huombi msamaha kama huna hatia.

“Kwa hiyo waheshimiwa majaji nataka niwe ‘very clear’ (nataka niseme bayana) kwamba haya nitakayosema yasichukuliwe kama naomba msamaha kwa sababu I’m completely innocent,” amesema Lissu aliyekuwa amevalia shati jeusi lenye mikono mifupi huku akiwa nywele zilizosokotwa kuwa rasta fupi. 

Lissu, aliyekuwa akijitetea mwenyewe, ameendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo aliyokuwa ameshtakiwa nayo ni ya kisiasa.  

“Kuna kitu hamjakisema majaji na mimi nitakisema ‘for the record’ (kwa kumbukumbu) kuwa mmekubaliana na nami kuwa hii ilikuwa ni kesi ya kisiasa kugeuza mahakama kuwa ni uwanja wa kisiasa, ni ‘political persecution’ (mateso ya kisiasa),” amesema Lissu. 

“Inabidi itengenezwe kesi ya kumfunga huyu mgomvi wetu wa kisiasa. Ni kutafuta excuses za kumfunga huyu mpinzani wa kisiasa kwa uchochezi kosa ambalo sikushtakiwa nalo,” ameongeza.

Lissu aliyekamatwa Aprili 9 mwaka jana hadi wakati hukumu inasomwa jijini Dar es Salaam alikuwa ameshakaa rumande kwa zaidi ya siku 575. 

Jela miaka minne

Wakati akisoma hukumu hiyo, Jaji Ndunguru amesema licha ya kuwa katiba inampa mtu uhuru na haki, Ibara ya 30 (1) inaeleza kwamba “pale mtu utakapokuwa unadai haki zako utahakikisha ya kuwa huingilii haki za mtu mwingine…haitatumika na mtu mwingine kuingilia haki au kukatiza haki ya mtu mwingine au watu wengine au maslahi ya umma.”

“Hivyo, tunasema katika mazingira hayo tunaona kuhamasisha kuzuia uchaguzi, kuhamasisha kuvuruga uchaguzi ni kuzuia pia haki ya kikatiba ya watu wengine,” Jaji Ndunguru amesema hayo ndani ya chumba cha mahakama kilichokuwa kimejaa watu waliotaka kushuhudia uamuzi huo. 

“Hivyo katika mazingira haya, mahakama inaona kwamba ‘option’ (chaguo) ya kwanza itakuwa ni kifungo badala ya faini na hivyo mahakama inakupa adhabu ya kifungo kwa muda wa miaka minne badala ya mitano ambayo ni maximum sentence (adhabu ya juu),” amesema Jaji Ndunguru kabla ya kuhitimisha hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa nne.

Jaji huyo amesema Lissu ana fursa ya kukata rufaa ya hukumu hiyo. 

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Itikadi wa Chadema, Brenda Rupia amemweleza mwandishi wetu kuwa watakata rufaa hukumu hiyo na kwamba kwa sasa chama hicho kitakuwa na vikao kujadili yaliyojiri mahakamani hapo. 

Baada ya hukumu hiyo Lissu alipelekwa gerezani akiwa chini ya ulinzi mkali wa maofisa magereza na polisi. 

Habari hii imeongezwa muktadha na Nuzulack Dausen

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
27 Nov, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
26 Nov, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
26 Nov, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
DC Mpogolo: Marufuku kufanya biashara za mapishi, moto Buguruni Darajani.

DC Mpogolo: Marufuku kufanya biashara za mapishi, moto Buguruni Darajani.

Nukta TV

CHADEMA: Hakuna mazungumzo tutakayofanya hadi Tundu Lissu aachiwe huru

CHADEMA: Hakuna mazungumzo tutakayofanya hadi Tundu Lissu aachiwe huru

Nukta TV

Je, maridhiano ni sharti la lazima, kabla ya mchakato wa Katiba mpya?

Je, maridhiano ni sharti la lazima, kabla ya mchakato wa Katiba mpya?

Nukta TV