Bunge lapitisha muswada wa Sheria ya TBC kuboresha utendaji wake

January 30, 2025 5:36 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuwa na vyanzo vya mapato vya uhakika, vyombo vya kisasa na ulinzi wa miundombinu

Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limepitisha Muswada wa Sheria ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wa mwaka 2024 ili kuliwezesha shirika hilo kukabiliana na changamoto za kifedha, kiutendaji, na kiteknolojia ambazo zimekuwa zikilikabili kwa miaka mingi. 

Muswada huo ambao umejadiliwa na kupitishwa katika kikao cha tatu cha Mkutano wa 18 wa Bunge, iwapo utapitishwa kuwa sheria itaipa TBC msingi thabiti wa kisheria na kuiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia mahitaji ya kisasa na mabadiliko ya teknolojia.

Kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Prof Palamagamba Kabudi, sheria hiyo itatambua TBC kama shirika muhimu la umma linalohusika na utangazaji wa habari, burudani, na elimu. 

Pia itaipa mamlaka ya kusimamia rasilimali zake na kuhakikisha kuwa inaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Changamoto za TBC 

Kwa mujibu wa mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Ali Mlagila, kamati hiyo iliyofanya uchambuzi wa muswada huo imebainisha kuwa kwa miaka mingi, TBC imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo utegemezi wa fedha kutoka serikalini ambazo mara nyingi hazitoshelezi mahitaji.

Mlagila amebainisha kuwa changamoto nyingine ni kukosekana kwa msingi imara wa kisheria unaohakikisha uendelevu wa shirika la TBC kutokana na kuanzishwa kwa amri ya Rais pekee.

Jambo hilo linasababisha waziri mwenye dhamana kutokuwa na mamlaka ya kutengeneza kanuni kwa ajili ya kusimamia na kuendesha masuala yanayohusiana na utendaji bora wa shirika ikiwemo ukusanyaji wa mapato na ulinzi wa miundombinu hivyo pamoja na mambo mengine muswada huo unalenga kutatua changamoto hiyo.

Kwa mujibu wa Mlagila, Sheria iliyopendekezwa itajumuisha masharti yanayotoa ufafanuzi na ufumbuzi wa changamoto mbalimbali ili kuiwezesha TBC kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwemo TBC kujipatia mapato kwa njia mbalimbali kama matangazo, ushirikiano na wawekezaji, na huduma zingine za kibiashara.

Sambamba na hilo, sheria hiyo itatoa nafasi ya kupanua usambazaji wa huduma zake kwa kuanzisha chaneli mpya za televisheni na redio, pamoja na kufikisha matangazo yake kwa watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi. 

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Prof Palamagamba Kabudi akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wa mwaka 2024, bungeni Dodoma. Picha |Bunge la Tanzania

Wabunge waunga mkono 

Innocent Edward, Mbunge wa Morogoro Vijijini (CCM) amesema, Sheria mpya inatarajiwa pia kuwa itachochea uwekezaji katika teknolojia mpya ikiwa ni pamoja na studio za kisasa, vifaa vya ukusanyaji na usambazaji wa habari, na mifumo ya kidigitali ili kuboresha ubora wa vipindi na kuvutia watazamaji zaidi.

“Naamini kwa kutungwa sheria hii tutakwenda kuipa TBC uwezo mkubwa wa kufanya mambo yake kuwa ya kisasa zaidi kama kuwekeza katika teknolojia mpya, ikiwa ni pamoja na mifumo ya digital na mtandao, ili kuboresha ubora wa huduma zake,” amesema Edward.

Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Jumanne (CCM), amesema kuwa sheria hiyo itasaidia TBC kukabiliana na changamoto za kifedha na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa kutumia vyanzo vipya vya mapato, kama vile matangazo na ushirikiano na wawekezaji ili kupunguza utegemezi wake kwa fedha za Serikali na kuipa nafasi ya kufanya maamuzi ya kibiashara.

“TBC imekuwa ikipambana na ukata mkubwa wa fedha. Sheria hii itaipa nafasi ya kujipatia mapato kwa njia mbalimbali,” amesema. 

Jumanne amefafanua kuwa Sheria mpya inayotarajiwa kutokana na muswada huo itaboresha hali ya ushindani wa kibiashara wa shirika hilo kuendana na vyombo vingine ambavyo baadhi yao vimekuwa vikitumia watu wenye mvuto kwa jamii kuvutia hadhira kubwa.

“Leo kuna baadhi ya mambo TBC haiwezi kufanya, mfano kwenye mambo ya ajira, wamebanwa na Sheria ya Utumishi wa Umma ambazo haziwaruhusu kuajiri kulingana na maudhui kwa mtazamaji kama kwenye vyombo vingine ili kuvutia watazamaji, kupitia sheria hii naamini kabisa inakwenda kutatua changamoto,” amesema Jumanne.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks