Rais Samia abainisha sababu za kutilia mkazo mifumo ya Serikali kusomana
- Ni pamoja na kurahisisha utoaji wa huduma na kudhibiti uzembe.
- Asisitiza mifumo kusomana ifikapo Desemba 2024.
- Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali kusimamia uboreshaji na kuunganishwa kwa mifumo hiyo.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha inatekeleza agizo lake la kuiunganisha mifumo ya Serikali na kuhakikisha inasomana ifikapo Desemba, 2024 ili kurahisisha utendaji kazi wa Serikali, kupunguza gharama na kudhibiti mianya ya rushwa.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa 15 wa Baraza la Biashara Tanzania (TNBC) Ikulu jijini Dar es Salaam leo Julai 29, 2024 amebainisha kuwa wizara hiyo si tu ihakikishe mifumo inasomana bali ifuatilie na kuunganisha mifumo mipya iliyoanzishwa.
“Kwa kuangalia manufaa ya mifumo kusomana naweza kusema tumechelewa sana kufanya kuiunganisha mifumo hii, hivyo nitumie jukwaa hili kuikumbusha wizara kuhakikisha kwamba lile agizo langu la kuhakikisha mifumo inasomana ifikapo Disemba 2024, liendelee kufanyiwa kazi
…Vilevile mfanye ufuatiliaji kuhakikisha mifumo yote mipya iliyotengenezwa nayo inasomana na mifumo iliyopo, mifumo yetu ikisomana inapunguza gharama zisizo za lazima lakini pia inapunguza uzembe na kuziba mianya ya rushwa,” amebainisha Rais Samia.
Soma zaidi: Rais Samia awafuta kazi Nape Nnauye, January Makamba
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kutoa agizo hilo, aliwahi kufanya hivyo Juni 9, 2023 akiwa kwenye mkutano kama huo wa TNBC akitaka kuharakishwa kwa maboresho yatakayofanya mifumo ya taasisi za umma isomane.
Agizo kama hilo alilitoa tena Agosti 11, 2023 kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kuhakikisha mifumo yote ya Tehama inayotumika ndani ya Serikali inasomana.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiongoza mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC)PichaI Ikulu Mawasiliano
Aidha, Aprili 3, 2024 wakati akizindua Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) alimuagiza Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa kuhakikisha anasimamia zoezi la kuunganisha mifumo ya Serikali ifikapo Disemba 2024, akiwataka makatibu wakuu wa wizara kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wake.
“Mifumo yote ya Tehama isomane, si yule anaenda kushoto, kulia, Mashariki, Magharibi hakuna kusomana, hakuna mawasiliano ndani ya Serikali,” alisema Rais Samia.
Rais Samia ametumia jukwaa hilo pia kuutambulisha Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Tanzania wa mwaka 2024- 2034 ambapo kupitia mkakati huo Serikali itahakikisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) inaboreshwa, inaunganishwa na kusomana ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa sekta binafsi na wadau wengine kupitia mifumo ya kielekitroniki.
Latest



