“Buku” ilivyonihamasisha kufanya biashara ya juisi-2
- Ilinichukua miezi miwili kupata wateja zaidi ya 10 kwa siku.
- Kuacha usingizi wa asubuhi, kubeba mizigo mizito kila siku ni kati ya vitu vilivyonikosesha “kijiamani”
- Corona ndiyo ilikuwa kikwazo kikubwa kuendelea na biashara hii.
Dar es Salaam. Baada ya kukupatia utangulizi wa safari yangu ya kuuza juisi, huenda umebaki na maswali mengi kuhusu biashara yangu na jinsi nilivyonufaika nayo na hata kubadilisha maisha yangu kiaina.
Usiwaze, sasa maswali yako yanaweza kujibiwa.
Nilisahau kukuambia kuwa kwa kipindi hicho chote ambacho nilikuwa nauza juisi nilikuwa najitolea katika kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa huku nikiitegemea familia yangu kuniwezesha kiuchumi.
Hata hivyo, baada ya kuanza biashara hiyo, simu za kuomba pesa zilipungua na hivyo walishangaa pale nilipowapigia kuwajulia hali tu.
Kutokana na mahusiano mazuri na wateja wangu, kila siku nilijipatia wateja wapya ambapo ilifikia wateja 20 kwa siku na hivyo kuuza chupa moja ya juisi kwa Sh1,000.
Kwa sababu gharama za utengenezaji wa juisi hiyo zilikuwa hazizidi Sh10,000 kwa siku nilikuwa na uhakika wa kupata faida ya Sh12,000 kwa siku ambayo ilinisaidia kusuka maisha ikiwemo kupata nauli ya kwenda kazini na kupunguza utegemezi kwa familia yangu.
Mbali na kuniondoa katika kundi la watu tegemezi kwa familia, biashara hiyo iliyoanza kama mzaha ilinifanikisha kufikia mahitaji muhimu lakini zaidi, iliniwezesha kuwa msaada wa kukidhi mahitaji ya shule ya wadogo zangu.
Walau nilikuwa na uwezo wa kukopesha hata rafiki na jamaa pale walipokuwa na uhitaji.
Wateja wangu wengi wanapenda nanasi, embe, karakara, hivyo kwa msimu ambao matunda haya yalipanda bei kwa kuwa nadra, faida ilipungua hadi Sh5000 kwa siku. Picha| Rodgers George
Hakuna safari isiyo na mabonde
Kuna asiyependa usingizi ati? Kuamka saa 10 alfajiri kila siku kutengeneza juisi haikuwa jambo nililolifurahia sana.
Kuna wakati nilijikuta nikiipotezea “Alarm” yangu na kushtuka saa 11 na hivyo kushindwa kufanya kazi yangu kwa ufanisi.
Hapo ndipo juisi ilipozidi maji na niliposhindwa kuweka umakini katika bidhaa hiyo na ni siku kama hizi ambazo ilinilazimu kuomba sahamahani kwa wateja wangu hasa wale wapendao sukari kwani nilisahau kuweka.
Hahaha! inachekesha kiaina lakini ilikuwa safari yenye faraja kwani wateja wangu hawakuwa wepesi wa hasira. Naweza kusema walinivumilia bila ya kujua kuwa ilinilazimu kubeba madumu ya juisi asubuhi na kubeba furushi la matunda jioni.
Mbali na hilo, wateja wangu wengi wanapenda nanasi, embe, karakara, hivyo kwa msimu ambao matunda haya yalipanda bei kwa kuwa nadra, faida ilipungua hadi Sh5000 kwa siku.
“Siyo haba, huwezi kupata faida siku zote” alinitia moyo shangazi yangu pale aliponikuta nimejiinamia nikilalama na mawazo huku akinibariki na maembe mawilli au matatu kutoka kwenye friji yake.
“Yarudi” alisema “Mungu ni mwema” nilijibu nikimtazama nikimaanisha “shangazi hapa imekula kwako,” na tabasamu lake lilionyesha kuwa tumeelewana.
Mbali na hilo, wapo wateja wangu ambao walipoteza mifuniko ya chupa na hivyo ilinilazimu kununua chupa zingine. Nilikuwa nikiudhika lakini niliwapatia juisi yao kesho yake kwa tabasamu.
Huenda iliwafanya kuwa makini siku zilizofuata kwani hakuna aliyewahi kupoteza mfuniko kwa mara ya pili.
Zinazohusiana
- “Buku” ilivyonihamasisha kufanya biashara ya juisi
- Hivi ndivyo ninavyotabasamu kwa kila kazi ninayofanya
- Unawezaje kuishi na kila mtu kwenye makazi mapya?
Nini kiliwafanya wateja wangu kurudi?
Ukweli ni kwamba nilitengeneza juisi ambayo pia niliifurahia. Sijisifii lakini muonekano wa nyuso zao kwa siku ambazo nilishindwa kufika ofisini na juisi ilinionyesha nina mchango katika furaha yao kila siku walau kwa dakika ambazo wanakunya juisi zao walizolipia.
Jambo lingine ni mfumo wa malipo ambao niliweka. Wapo wateja walionilipa kwa siku, walionilipa kwa wiki na wale walionipaSh10,000 na kunywa juisi hadi pesa yao itakapoisha.
Hiyo ilimfanya hata asiye na pesa leo, apate kinywaji chake bila hiana.

Kikomo cha safari yenye tabasamu
Safari yangu ya biashara ilianza kuyumba mara baada ya Tanzania kutangaza mgonjwa wa kwanza wa Corona ambapo kwa namna moja ilinifanya nijiulize juu ya usalama wangu pale ninapoenda sokoni pamoja na usalama wa wateja wangu pale ninapotengeza juisi.
Nilitaka kusitisha lakini niliwaza ni kwa jinsi gani mazowea niliyowajengea wateja wangu ningeweza kuyakatisha. Kwa upande wao, hawakuonekana kuwaza lolote lakini binafsi, jambo hilo lilinifikirisha sana.
Hapana, siyo kwasababu ningekosa pesa, bali kwasababu ningeshindwa kuwa sehemu ya tabasamu lao. Nilipenda iwe hivyo.
Safari hiyo ilifika tamati Machi 20, 2020 ambapo ofisi zetu zilifungwa na shangazi yangu hakuniruhusu kutoka akihofia nitapeleka corona nyumbani.
Hapo ndipo shangazi pamoja na familia kwa ujumla walivyoanza kufurahia juisi ambazo wateja wangu walikuwa wakizifurahia. Niliwakumbuka sana wateja wangu na niliapa kuwapatia juisi za bure mara tu ofisi zitakapofunguliwa.
Hata baada ya ofisi kufunguliwa, bado sijatimiza kiapo nilichoweka kwani bado nipo kwenye sintofahamu ya kama nitaendelea na biashara hiyo licha ya wateja wangu kuniuliza kila mara waonapo sura yangu.
Sijaridhika bado, ila niko njiapanda kama itakuwa salama kwao na kwangu kuendelea.
Natumaini umejifunza kitu, hadi wakati mwingine, wako katika ujenzi wa uchumi wa vijana, Rodgers George.
Latest
