Ubunifu unavyowabeba waliojiajiri kuuza juisi Dar
- Ushindani wa biashara hiyo waongezeka.
- Wanatumia nakshi na urembo kuongeza thamani za juisi.
- Vifungashio vyenye ubora vyawatofautisha na wengine sokoni.
Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji yanayokua kwa kasi duniani, jambo linalofungua fursa kwa vijana kujiajiri katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Miongoni mwa biashara iliyojipatia umaarufu katika mitaa mbalimbali ya jiji hili lililopo mashariki mwa Tanzania ni utengenezaji na uuzaji wa juisi za matunda.
Juisi hizo (shurabati) hutengenezwa kwa matunda mbalimbali kama embe, karoti, stafeli, tende, nanasi, ukwaju, machungwa na mapapai. Huongezwa viungo na ladha tofauti tofauti ikiwemo tangawizi ili kumuongezea mnywaji hamu ya kunywa kwa kiwango kinachohitajika.
Kutokana na umaarufu wake imevutia idadi kubwa ya vijana jijini hapa ambao wanatumia kama fursa ya kujiajiri na kuingiza kipato kwa ajili ya kuboresha maisha.
Juisi hizo huuzwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo sokoni, vituo vya daladala na mafuta na hata kwenye migahawa.
Kadiri ushindani wa biashara hiyo unavyokuwa mkubwa, wauzaji wa bidhaa hiyo hufanya kila linalowezekana kuwafikia wateja wao kwa kuongeza ubunifu katika bidhaa zao ikiwemo kuboresha vifungashio na muonekano wake.
Noti Hemedi, mfanyabiashara wa juisi Tabata Jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa vijana ambao kila siku anaongeza ubunifu katika biashara yake ili asiwapoteze wateja wake.
“Wiki moja tu mara baada ya kuanza kuuza juisi hizi nilianza kufikiria namna ninavyoweza kuboresha ndiyo nikaja na wazo la ubunifu huu wa kuongeza muonekano na ladha ya juisi zangu,” anasema Noti ambaye ni mmiliki wa Notty Fresh Juice.
Juisi anazotengeneza, kijana huyo ni pamoja na za matunda ya embe, karakaa, stafeli na tende.
Ubunifu wa kuongeza mvuto ni moja kati ya mbinu zinzzotumika kuvuta wateja wa juisi. .Picha | Noti Hemedi.
Tofauti na wafanyabiashara wengine, vifungashio anavyotumia Noti ni vya kisasa vilivyotengenezwa kwa plastiki vikiwa na mifuniko kwa juu na mrija ambao, mteja anatumia kunywea juisi.
Mbali na kutumia vifungashio hivyo, juisi yake ni ya kuvutia kwa sababu anaiongezea urembo na nakshi kwa kutumia kimiminika cha ladha ya chokoleti ambacho humvuta mtu kwa haraka kununua.
“Sasa hivi tuna juisi ya peanut banana (ndizi na karanga),” anasema Noti kuwa juisi hiyo siyo rahisi kuikuta katika maeneo yanayouza juisi na ameamua kuwaletea wateja wake bidhaa mpya ili kukidhi mahitaji yao.
Kila aamkapo, Noti hufikiri namna ya kuboresha biashara yake kwa kusoma mtandaoni na kuwauliza wateja nini cha kufanya ili kukidhi mahitaji yao ili aendelee kuwepo katika ushindani wa soko.
“Kila siku najifunza ili kuhakikisha natengeneza kitu kipya, ndiyo maana hata nikaja na wazo la juisi ya ndizi na karanga ambayo wengi hawakudhani kama kuna juisi aina hiyo,” anasema Noti.
Kijana huyo ambaye ni msomi kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) alikosomea masoko na mahusiano kwa umma anasema tangu aanze kuongeza ubunifu kwenye biashara yake amekuwa akipata wateja wengi kulinganisha na wakati anaanza mishe hiyo.
“Ubunifu huu umeniongezea wateja sana mfano mtu anakuwa hataki kununua juisi ila akiona umemleta mteja mwingine unakuta anapenda muonekano wa juisi zetu hivyo na yeye ananunua,” anasema kijana.
Soma zaidi
-
Biashara ya juisi inavyowatoa kimaisha wasomi waliokataa kuajiriwa
-
“Buku” ilivyonihamasisha kufanya biashara ya juisi
Usalama nao ni ubunifu
Tofauti na wauzaji wengine wa juisi ambao wanaweza kuwa hawazingatii usafi, Noti anasema yeye usafi ni wa muhimu kwenye biashara yake na unaanza wakati wa kununua na kuchagua matunda anayotumia kwenye utengenezaji wa juisi.
“Mimi nazingatia sana usafi hata matunda ninayotumia nahakikisha kuwa yako salama ili hata mteja akinikuta natengeneza basi asishtuke,” ameongeza mfanyabiashara huyo.
Biashara hiyo ndiyo inamuweka mjini kijana huyo na kumuwezesha kutunza familia ya watu watatu akiwemo mama yake.
Alikotoka na anakoenda
Ukosefu wa ajira baada ya kuhitimu masomo ya chuo mwaka 2020, ilikuwa changamoto iliyobadilika kuwa fursa kwa kijana huyu kuanzisha biashara ya juisi.
“Nilianzisha biashara hii ili kuweza kujiingizia kipato cha ziada kwa sababu kazi niliyopata nilikuwa nalipwa kwa commission (mpaka nipeleke wateja),” anasema Noti.
Licha ya kuwa alianzisha biashara hiyo kama hatua ya kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira baada ya kumaliza chuo lakini imekuwa ni kazi yake ambayo amepanga kuikuza na kutua ajira kwa vijana wenzake.
Noti Hemedi akiwa katika kibanda chake anachotumia kuuzia juisi. Picha| Noti Hemedi.
Changamoto anazozipitia
Kama ilivyo kwa vijana wengine kuanza biashara changamoto kubwa huwa ni mtaji, hata kwa Noti ilikuwa hivyo lakini angalau yeye alipata pa kuanzia kwa kutumia vifaa vya nyumbani kutengeneza juisi hizo.
“Nilianza zero nikiwa sina mtaji kabisa ikanibidi kutumia vifaa vya nyumbani kama blenda na fridge (jokofu) ya nyumbani, haikuwa ngumu sana kwangu kuanza,” anasema Noti.
Kwa vijana wanaokabiliwa na changamoto za ajira, Noti anawashauri kuangazia shughuli ndogo ndogo katika maeneo yao wanazoweza kufanya ili kujiingizia kipato.
Latest