Mitandao ya kijamii fursa kukuza ujasiriamali
- Husaidia kuwafikia wateja wengi kwa muda mfupi.
- Ni njia mojawapo ya kutangaza bidhaa na huduma.
- Kufaidika na mitandao ya kijamii inahitaji umakini na uvumilivu.
Dar es Salaam. Wewe ni mjasiriamali na umekuwa ukipata changamoto ya kuwafikia watu wengi ili uuze bidhaa au huduma? Kama jibu ni ndio, suluhu imepatikana. Ni matumizi ya mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa au huduma unazotoa.
Mitandao ya kijamii haitumiki kuwasiliana pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuboresha maisha ya wajasiriamali kwa kuongeza kasi ya kuwafikia watu wengi.
Ni muhimu kufahamu kuwa dunia imehamia mtandaoni. Shughuli mbalimbali za kibiashara hufanyika mtandaoni. Kwako wewe mjasiriamali unayeanza au ambaye uko sokoni kwa muda mrefu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii yanaweza kuboresha biashara yako.

Zipo faida nyingi kwa wajasiriamali kutumia mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, Twitter na hata TikTok.
Hupunguza gharama za kufungua duka
Ponsiana Chikawe (23) mkazi wa Gogoni jijini Dar es salaam, mjasiriamali anayejihusisha na uuzaji wa nguo za ndani za wanawake na wanaume, ni mfano hai wa jinsi mitandao ya kijamii inavyobadilisha biashara.
Ponsiana hana duka lakini huuza bidhaa zake WhatsApp, Instagram, na Snapchat na kuwafikia wateja wengi kwa muda mfupi.
“Mitandao ya kijamii inanipa nafasi ya kuwafikia watu wengi kutoka sehemu tofauti, hata walioko mikoani…Sihitaji kuwa na duka, lakini bado nauza vizuri kwa sababu naweza kutangaza bidhaa zangu kwa urahisi na kuwatumia wateja mizigo yao kwa uaminifu,” anasema Ponsiana.
Mjasiriamali huyu anaeleza kuwa hata wenye maduka wanaweza kutumia mitandao ya kijamii kuongeza wigo wa wateja.
“Hata ukiwa na duka, bado unahitaji mtandao kwa sababu inakusaidia kuwafikia wateja wengi zaidi,” anasisitiza Ponsiana.
Cletus Mboya (20), kijana anayejihusisha na uuzaji wa simu na vifaa vyake, anaweka wazi kuwa licha ya kuwa na duka lililopo Kariakoo, bado anapata wateja wengi zaidi kupitia mitandao ya kijamii.
“Kwa siku, wateja ninaopata kupitia WhatsApp, Instagram na Snapchat ni wengi zaidi kuliko wale wanaoniona kwa macho wakipita dukani. Hii inanifanya nitumie muda mwingi mtandaoni kujibu wateja na kuwashawishi zaidi,” anasema Mboya.

Hukuza biashara kwa haraka
Baadhi ya wajasiriamali ambao nukta.co.tz imeongea nao, wanaeleza kuwa baada ya kufahamu nguvu ya mitandao ya kijamii kusaka wateja, biashara zao zimekua na wao wameboresha maisha.
“Nilipoanza kuweka video fupi za kutengeneza juisi na keki zangu TikTok na Instagram, wateja wakaanza kumiminika…watu wanapenda kuona bidhaa kabla ya kununua, na mitandao ndio sehemu pekee naweza kufanikisha hilo… wengi wanafika mgahawani kwangu baada ya kuona posti zangu,” amesema Janeth John (23), mjasiriamali anayemiliki mgahawa mdogo wa juisi na keki uliopo Kimara Baruti, Dar es Salaam.
Siyo rahisi kihivyo…
Licha ya faida kubwa zinazotokana na kutumia mitandao ya kijamii katika biashara, wajasiriamali wana kibarua cha ziada. Ushindani wa soko umeongezeka, utapeli wa mtandaoni na ugumu wa kujenga uaminifu wa wateja.
Ponsiana anasema kwa sababu hana duka, baadhi ya wateja wanapata mashaka ya kulipia bidhaa bila uhakika wa kuzipokea.
“Wanaogopa kuibiwa fedha zao, hasa kwa sababu kuna matapeli wengi mitandaoni. Wakati mwingine, mteja anaomba kuja dukani kujiridhisha, lakini ninapomwambia kuwa nafanya biashara mtandaoni pekee, wengi hupotea na hawanunui tena,” anaeleza kwa masikitiko.
Mawasiliano yasiyo na lengo la kibiashara ni changamoto kubwa nayokumbana nayo Cletus Mboya. Kutokana na kuweka mawasiliano yake wazi kwa ajili ya biashara, anakutana na watu wanaoleta mijadala isiyohusiana kabisa na biashara, hasa kuhusu masuala ya mapenzi.

“Unakuta mtu anaomba bei ya simu, lakini baada ya muda mazungumzo yanabadilika na anauliza maswali yasiyo na uhusiano na biashara. Hii inapoteza muda na wakati mwingine inakatisha tamaa,” anasema Mboya.
Naye Janeth anasema baadhi ya wateja wanaweka oda mtandaoni lakini hawaendi dukani kuchukua bidhaa. Hii huleta hasara baada ya mteja kuingia mitini.
“Nilikuwa natengeneza bidhaa kabla ya mteja kulipia, lakini mara nyingi nilipata hasara. Sasa nimejifunza, siandai kitu chochote hadi mteja alipie kwanza,” anasema kwa msisitizo Janeth.
Mbali na hilo, changamoto nyingine ni kucheleweshwa kwenye mihadi ya kuchukua bidhaa, jambo linalomsababishia kupoteza muda na kuathiri ratiba yake ya kazi.
“Wateja wengine huomba niwapelekee bidhaa sehemu fulani kwa muda waliopanga, lakini wakifika huko, wanachelewa au hawatokei kabisa. Inakuwa usumbufu na upotevu wa muda,” anaeleza Janeth huku akisisitiza umuhimu wa wateja kuwa waaminifu.
Licha ya changamoto hizi, wajasiriamali wanaendelea kutumia mitandao ya kijamii kwa sababu ya manufaa yake makubwa. Uaminifu wa wateja unajengwa kwa muda, na kwa kutumia njia sahihi za mawasiliano, wafanyabiashara wanaweza kuondoa vikwazo hivi na kufanikisha biashara zao kwa ufanisi zaidi.
Mitandao ya kijamii si tu nyenzo ya matangazo, bali ni uwanja mpana wa biashara unaotoa fursa ya kufikia wateja wengi zaidi, kuongeza mauzo, na kukuza chapa (brand) bila gharama kubwa. Changamkia fursa ya matumizi ya mitandao ya kijamii.
Latest



