Kutana na mtengeneza misumari ya majahazi, majeneza anayefanyia shughuli zake makaburini

June 17, 2022 1:08 pm · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Ally Kisukari, mhunzi anayeendesha shughuli zake pembezoni mwa makaburi ya Mwananyamala kwa Kopa.
  • Amejipatia umaarufu kwa sababu anauza misumari hadi Mombasa, Kenya.
  • Teknolojia duni, ukosefu wa taarifa yamkosesha mafanikio.

Dar es Salaam. Ni saa tano asubuhi, sauti ya vyuma vinavyogongwa inasikika kutoka katika makaburi yaliyopo Mwananyamala kwa Kopa jijini Dar es Salaam.

Sauti hiyo ni bidhaa za vyuma zinazotengenezwa na mhunzi anayefanyia kazi zake pembezoni mwa makaburi hayo yaliyopo Kata ya Mwananyamala, Wilaya ya Kinondoni. 

Akiwa katika kibanda kidogo kilichozungushiwa mabati yaliyochakaa, Ally Kisukari anaendelea kukoleza moto ili kuyeyusha vyuma vinavyotumika kutengenezea misumari ya kuunganishia majeneza na majahazi (mitumbwi) yanayotumika katika shughuli za uvuvi hasa Bahari ya Hindi. 

Ally aliyeanza kufanya shughuli hiyo ya uhunzi katika eneo hilo miaka 18 iliyopita hutengeneza vifaa (patasi) vya kuchongea vinyago na bidhaa nyingine za mbao ambazo hutumika katika shughuli za utamaduni, sanaa na utalii. 

Ally aliyerithi kazi hiyo kutoka baba yake ni miongoni mwa vijana wa Tanzania waliojiajiri katika shughuli ndogo ndogo ili kujipatia kipato kwa ajili ya familia. 

Licha ya bidii na ubunifu alionao bado hajafaidika kikamilifu katika shughuli hiyo ya uhunzi kwa sababu ya kukosa taarifa muhimu, matumizi ya teknolojia duni na ukosefu wa mitaji kuboresha mazingira ya biashara yake. 

Kilichomsukuma kufungua banda hilo kando ya makaburi ni kutokana na eneo walilokuwa wanafanyia kazi awali kuchukuliwa na mwekezaji. 

“Mahali hapa tuliamia baada ya kupisha ujenzi wa eneo ambalo tulikuwa tukifanya biashara awali ndio tukasogea karibu na makaburi haya,” anasema Ally.

Ally Kisukari akiendelea na shughuli  ya uhunzi katika banda lake jijini Dar es Salaam. Picha| Daudi Mbapani.

Teknolojia bado kikwazo

Licha ya kijana huyo mwenye familia ya watoto watatu kujibidiisha katika kazi yake, bado hajafanikiwa kuifanya biashara yake kuwa ya kisasa kutokana na kutumia teknolojia duni ya kutengeneza vifaa hivyo.

Amebuni teknolojia isiyo rasmi ya kuyeyusha vyuma ili kupata maumbo anayoyataka kwa kuchukua mfumo wa kiyoyozi cha gari (AC) ambao umeunganishwa na umeme wa kawaida.

Mashine hiyo ambayo imeunganishwa na bomba maalum la chuma huzalisha upepo kwa ajili ya kuwasha moto wa mkaa kuwaka wakati wote anapokuwa analainisha vyuma mbalimbali anavyotengeneza. 

Teknolojia anayotumia Ally humfanya kutumia nguvu nyingi za mwili na muda mrefu kukamilisha majukumu yake.

Licha ya changamoto hizo, mhunzi huyo ana uwezo wa kutengeneza  wastani wa misumari 100 hadi 200 ya ukubwa tofauti kwa siku moja ikiwemo ya nchi tano ambapo msumari mmoja anauzwa kwa Sh350.  

“Hii mashine inanisaidia sana kutengeneza misumari kwa sababu moto wa mkaa unawaka wakati wote,” anasema Ally huku akiendele kutengeneza misumari katika banda lake lenye upana wa mita tatu.


Soma zaidi: 


Soko la bidhaa zake

Misumari anayotengeneza Ally huwauzia wavuvi kwa ajili ya kuunganisha kuunda majahazi ya kuvulia samaki na dagaa katika mwambao wa Bahari ya Hindi ikiwemo Dar es Salaam na Mombasa nchini Kenya.

Kutokana na ufanisi wa misumari hiyo, wateja wake hutoka pande mbalimbali kuifuata katika ofisi yake na mingine hutengeneza kwa oda na kuwapelekea katika maeneo yao.

Ganinus Mussa, mfanyabiashara katika soko la vinyago Mwenge jijini Dar es Salaam ni miongoni anakiri patasi anazotengeneza Ally zimekuwa zina ufanisi mkubwa katika kazi yake ya uchongaji bidhaa hizo zinazotokana na miti ambazo hutumiwa na watalii au shughuli za utamaduni. 

“Mimi huwa sipendi kwenda dukani, napendelea kuja hapa (kibanda cha Ally) kwa sababu vifaa hivi anavyotengeneza Ally ni imara na bei rahisi,” anasema Ganinus wakati akitoka kununua patasi kwa mhunzi huyo. 

Wateja hao ndiyo wanamuweka mjini Ally, licha ya kuwa soko lake siyo kubwa kumuwezesha kuzalisha bidhaa nyingi kwa wakati mmoja. 


Mafanikio aliyopata mpaka sasa

Katika eneo analofanyia kazi amezungukwa na vijana wengine ambao hujishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo kutengeneza majiko ya mkaa na kurekebisha ndoo za plastiki zilizotoboka.

Ally anasema akilinganisha na wenzake anaofanya nao kazi, yeye amepiga hatua kidogo katika maisha kwa sababu kipato anachopata humsaidia kutunza familia na kusomesha watoto. 

“Kwa kweli biashara hii ndiyo inanisaidia kusomesha watoto wangu, pia nimenunua kiwanja na kujenga nyumba kupitia biashara hii hivyo najivunia,” anasema Ally huku akitabasamu na kubainisha kuwa hayo ni mafanikio makubwa kwake. 

“Pia kodi nayolipia eneo langu la kazi hutokana na kipato cha biashara yangu hii.”

Mashine anayotumia Ally kukoleza moto kwa ajili ya kulainishia vyuma. Picha| Daud Mbapani.

Changamoto zinazomvuta nyuma 

Ili mhunzi huyo afanikiwe zaidi katika shughuli hiyo ikiwemo kuongeza uzalishaji na masoko anatakiwa kupanua wigo wa kupata taarifa kuhusu ujasiriamali na kuboresha teknolojia anayotumia. 

“Changamoto zipo kwa sababu saa nyingine unaweza hata kuungua na moto nifanyapo kazi zangu hizi, lakini mbali na hiyo malighafi nazotumia (nondo) muda mwingine bei inakuwa juu hivyo biashara inakuwa ngumu,” anasema.

Pia hulazimika kuacha kwa muda kutengeneza bidhaa ili kupisha shughuli za mazishi katika eneo la makaburi, jambo ambalo humfanya kukosa mapato kwa sababu wanaozika wakati mwingine huja kwa mfululizo. 

Hata hivyo, hajakata tamaa kwa sababu anaamini safari ya kuboresha maisha ina vikwazo vingi, hivyo anakusudia kufanya ubunifu mkubwa katika teknolojia anayotumia na kutafuta eneo zuri litakalomwezesha kuajiri watu watakaomsaidia katika uzalishaji. 


Wito kwa vijana wengine

Ally anasema wito wake kwa vijana ni kupenda kujifunza ili kupata ujuzi ambao utawasaidia kujiajiri kwenye vitu mbalimbali wanavyovipenda.

“Ujuzi huu niliupata kwa baba yangu hivyo vijana wenzangu nawasihi nao  kujifunza ujuzi mbalimbali ili nao waweze kufanya kujiajiri.” Ally anasema.


Tangazo:


Mambo muhimu ya kuzingatia

Wataalam wa masuala ya ujasiriamali wanawashauri wafanyabiashara ndogo ndogo kama Ally kuwa na malengo endelevu ya kukuza biashara zao ili kuwawezesha kukua kila siku.

Mtaalamu wa masuala ya biashara na uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) Damas Mushi anasema wajasiriamali wanatakiwa kuwa na malengo ya biashara kwa kuweka rekodi ya mapato na matumizi ili kulinganisha kwa kipindi kilichopo na kijacho kwani kufanya hivyo kutaweza kumsaidia kujua iwapo anaendelea au anakwama katika biashara.

“Baadhi ya wafanyabiashara wanafanya kazi kwa mazoea bila malengo yoyote, hivyo ni muhimu kuweka malengo ya unachofanya kwani hii itamsaidia kujisimamia kwa umakini,” aanasema Mushi, ambaye ni mhadhiri wa SAUT. 

Hata hivyo, Mushi anashauri endapo mjasiriamali anaona kazi anayoifanya kwa muda mrefu haikui kama matarajio yake ni vyema kujaribu kazi nyingine.

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV