Bodi ya mikopo leo kutolea ufafanuzi tamko la wanafunzi UDSM

December 16, 2019 10:21 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kutoa saa 72, bodi hiyo iwe imetekeleza maagizo manne likiwamo kuwaingizia fedha wanafunzi ambao hawajapewa.
  • Daruso pia imeitaka Heslb kurejesha makato ya fedha za vitabu, mafunzo kwa vitendo na utafiti. 
  • Heslb yasema inawasiliana na menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) ili kufanyia kazi madai yaliyotolewa. 

Dar es Salaam. Kufuatia Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) kutoa saa 72 kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Heslb) kutekeleza maagizo manne likiwamo kuwaingizia fedha wanafunzi ambao hawajapewa tangu chuo hicho kifunguliwe, bodi hiyo imesema itatoa ufafanuzi wa suala hilo leo Desemba 16, 2019.

Taarifa ya Daruso iliyotolewa jana (Desemba 15, 2019) inaeleza kuwa endapo maagizo hayo hayatatekelezwa katika muda uliotolewa wanafunzi watakusanyika nje za ofisi za Heslb, zilizopo Mwenge jijini Dar es Salaam kupigania hatma yao. 

Imesema wamefikia uamuzi huo baada ya wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza kukosa mikopo tangu chuo kifunguliwe huku baadhi ya wanafunzi wanaoendelea wakikatwa fedha zao. 

Daruso pia imeitaka Heslb kurejesha makato ya fedha za vitabu, mafunzo kwa vitendo na utafiti. 


Zinazohusiana


Hata hivyo, kabla serikali hiyo ya wanafunzi haijatimiza azma yake, Heslb kupitia ukurasa wake wa Twitter imesema inawasiliana na menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) ili kufanyia kazi madai yaliyotolewa. 

“Tumepokea taarifa hii na tutaitolea ufafanuzi wa kina baadae leo. Tunawasiliana na menejimenti ya UDSM kufanyia kazi yaliyotajwa!,” inasomeka sehemu ya taarifa ya bodi hiyo iliyotolewa leo (Desemba 16, 2019). 

Tumepokea taarifa hii na tutaitolea ufafanuzi wa kina baadae leo. Tunawasiliana na menejimenti ya UDSM kufanyia kazi yaliyotajwa! pic.twitter.com/RzJebl1UEd

Mikopo hiyo husaidia wanafunzi kuweza kumudu gharama za masomo na maisha wakati wakiwa kwenye kipindi cha masomo ya elimu hiyo ya juu.

Katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali imetenga Sh450 bilioni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu, ikiwa imeongezeka kutoka Sh427 bilioni zilizotengwa mwaka uliopita. Fedha zilizotengwa mwaka huu zitawanufaisha wanafunzi 123,283 wakiwemo 41,285 wa mwaka wa kwanza.

Septemba 9, 2019, alipotembelea ofisi za bodi hiyo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha , aliitaka bodi hiyo kuhakikisha fedha hizo zinawafikia wanafunzi kwa wakati kwa sababu tayari Serikali imetoa fedha za awamu ya kwanza.

Nayo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia ujumbe wake wa Twitter, imesema imepokea taarifa ya kuwepo kwa changamoto za mikopo ya wanafunzi wa UDSM na imeiagiza bodi ya mikopo na uongozi wa chuo kukutana na serikali ya Daruso leo ili kutatua changamoto hizo.

“Wizara inawataka wanafunzi kuwa watulivu na kuendelea na masomo wakati changamoto hizo zikishughulikiwa,” inasomeka sehemu ya ujumbe wa Twitter wa wizara hiyo.

Enable Notifications OK No thanks