Benki ya Dunia yatoa Sh10.3 bilioni kusambaza maji vijijini kwa umemejua Tanzania
- Fedha hizo zitawanufaisha Watanzania 500,000 kutoka vijiji 165 kupata maji safi yanayosambazwa na mifumo ya umemejua.
- Unakusudia kupunguza gharama za upatikanaji wa maji vijijini.
- Pia utaboresha maisha ya Watanzania waishio vijijini na kuwaongezea kipato cha familia.
Dar es Salaam. Huenda maisha ya wananchi kutoka vijiji 165 katika mikoa tisa ya Tanzania yataboreshwa, baada ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia kuingia makubaliano ya kuongeza kasi ya usambazaji maji vijijini kwa kutumia mifumo ya umemejua.
Makubaliano hayo yanatokana na kusainiwa kwa mkataba utakaoipatia Tanzania Dola za Marekani 4.5 milioni sawa na Sh10.3 bilioni ili kuwawezesha wananchi kutoka katika mifumo duni ya upatikanaji na usambazaji maji; na kuwaletea mifumo rafiki inayotumia pampu zinazoendeshwa na nishati ya umemejua.
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia iliyotolewa leo (Septemba 24, 2019), mradi huo utakaotekelezwa kwa pamoja na shirika la kimataifa la Global Partnership for Results-Based Approaches (GPRBA) unakusaidia kuwafikia Watanzania 500,000 ambao hawajaunganishwa na gridi ya umeme ya Taifa na kuwapunguzia gharama za kupata maji safi na salama.
Mradi huo utawasaidia kuboresha maisha na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli nyingine za kiuchumi ili kujipatia kipato cha kuendesha familia na kusomesha watoto.
Shirika la kimataifa la GPRBA litachangia asilimia 60 na asilimia iliyobaki itachangiwa na mashirika ya kijamii ya usambazaji maji (CBWSOs) ili kuachana na mashine zao za usambazaji maji zinazotumia mafuta ya dizeri na kuanza kutumia mashine za umemejua.
Zinazohusiana:
- Visima kumaliza tatizo la upatkanaji wa maji safi na salama nchini
- Umejua unavyoweza kuchangia upatikanaji wa maji safi vijijini
Katibu Mkuu wa Wzara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kuletwa kwa mradi huo kunatazamia kupunguza gharama za maji kwa watumiaji katika jamii mbalimbali nchini.
“Kuletwa kwa huduma hii ya kupandisha maji kwa umemejua inatarajiakupunguza gharama za uendeshaji kwa mashirika ya kijamii kwa kuwapatiarasilimali mbalimbali ikiwemo pesa ili kupunguza gharama kwa watumiajiwa maji na kuendeleza huduma hiyo”, amesema Prof. Mkumbo.
Utaratibu wa kidigitali wa malipo utaanzishwa ili kuwezesha ukusanyaji rahisi wa mapato YA mauzo ya maji na malipo ya madeni kutoka kwa wanachama wa CBWSOs na yatapelekwa moja kwa moja kwenye benki za ndani (Local banks).
Naye, Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Bella Bird amesema huduma hiyo itaboresha maisha ya Watanzania kwa kuwapatia maji ya uhakika katika maeneo yao.
“Kwa mradi huu tunatazamia kuanzisha teknolojia mpya ili kuendeleza sekta binafsi kwa huduma za maji zilizo bora na stahimilivu. Ni matumaini yetu kwamba kwa kuunganisha pampu zinazotumia umemejua na teknolojia zingine zitaimarisha mfumo mpya katika sekta hiyo,” amesema Bird.
Latest