Uchimbaji madini ya kinywe, adimu utakavyoipa tabasamu Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan akishuhudia Waziri wa Madini Doto Biteko pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Eliezer Mbuki Feleshi wakisaini Mkataba wa Makubaliano ya Msingi (Framework Agreement) baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Evolution Energy Minerals ya Australia iliyowakilishwa na Mtendaji Mkuu wake Phillip Hoskins, pamoja na viongozi wengine Michael Bourgnoin pamoja na Heavenlight Kavishe kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma, Aprili 172023. Mkataba huo ni wa Chilalo, Ruangwa Mkoani Lindi
- Unatarajia kuvutia uwekezaji wa Sh1.5 trilioni.
- Utafungua milango ya ajira, biashara na kuongeza pato la Taifa.
- Madini hayo yamegunduliwa katika mikoa ya Songwe, Morogoro na Lindi.
Dar es Salaam. Serikali inatarajia kuvutia uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 667 sawa na Sh1.5 trilioni baada ya kuanza kuchimba na kuchakata madini ya kinywe na adimu ambayo yatasaidia kuongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia huku ikiboresha maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan akirejea utafiti wa madini ya kinywe na madini adimu ulioanza mwaka 2000 kupitia kampuni mbalimbaili, hadi sasa kuna mashapu tani milioni 67 yenye wastani wa asilimia 5.4 ya madini ya kinywe yaliyogundulika katika Kijiji cha Chilalo mkoani Lindi ambayo yatachimbwa kwa muda wa miaka 18.
Tani milioni 63 zenye 7.6 ya madini ya Kinywe yamegundulika katika Kijii cha Ipanko, mkoani Morogoro ambayo nayo yatachimbwa kwa miaka 18 huku tani milioni 18.5 zenye asilimia 4.8 ya madini adimu yamegundulika katika Kijiji cha Ngualla mkoani Songwe ambayo uchimbaji wake ni wa miaka 20.
Madini haya ya kinywe na adimu yanajulikana kama madini muhimu ya kimkakati duniani kutokana na uwezo wake wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Yanahitajika sana katika teknolojia mpya za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo hutumika kutengeneza betri za magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki na mitambo mbalimbali,” amesema Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Aprili 17, 2023 Ikulu mkoani Dodoma wakati wa utiaji saini mikataba ya makubaliano kati ya Serikali na kampuni tatu za madini kutoka nchini Australia.
Amesema kutokana na Tanzania kuwa na madini haya, imekuwa nchi ya kutamaniwa na wawekezaji duniani.
“Katika siku zijazo nchi yetu itakuwa kitovu cha uzalishaji na usafishaji wa madini haya na hivyo kuweza kuvutia uwekezaji mahiri,” amesisitiza kiongozi huyo mkuu wa nchi.
Amesema utekelezaji wa mikataba hiyo utafungua fursa mbalimbali ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua madini hayo hivyo kufaidika na fedha zitakazolipwa na nchi nane jirani zinazoizunguka Tanzania zenye madini hayo.
Serikali itapata kodi, tozo, itafungua fursa za ajira na biashara hasa kwa wananchi walio karibu na migodi ya madini hayo, itasaidia kukuza uwezo wa kitaaluma na kurudisha hisani kwa jamii.
“Kwa mwenendo huu ambao tunajitahidi kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini sekta ya madini itazidi kukua na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.
Ni matarajio yangu kuwa kwamba ifikapo 2025 sekta hii itatimiza lile lengo tulilowekewa kwenye Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025 sekta hii ichangie katika pato la Taifa kwa asilimia 10,” amesema Rais.
MHE. RAIS SAMIA AKISHUHUDIA UTIAJI SAINI WA MIKATABA YA MAKUBALIANO KATI YA SERIKALI NA KAMPUNI 3 ZA MADINI ZA AUSTRALIA https://t.co/9cRmDvRdgZ
— ikulu_Tanzania (@ikulumawasliano) April 17, 2023
Nini kifanyike?
“Miradi hii ni mikubwa ni lazima ilete manufaa kwa Taifa, kwa hiyo Watanzania tujipange katika sera yetu ya uwekezaji wa ndani kwenda kutoa kufanya kazi, huduma kwenye miradi hii,” amesema Rais akiwataka Watanzania kuchangamkia fursa.
Amewataka viongozi na wananchi katika maeneo husika kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na kuhahakisha miundombinu ya migodi ya madini hayo inalindwa ili iwafaidishe huku akiagiza kurahisishwa kwa utekelezaji wa mikataba hiyo kama ilivyopangwa.
“Ni matumaini yetu Watanzania kuwa utekelezaji wa miradi hii utafanyika kwa haraka ili miradi hii ianze kuchangia pato la Taifa,” amesema Rais akimalizia hotuba yake.
Kuinua pato la Taifa
Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema madini hayo yatasaidia kuongeza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa pato la Taifa kutokana na uwekezaji utakaofanyika.
“Miradi hii yote ambayo umeshuhudia (Rais Samia) ikisainiwa italeta mtaji wa uwekezaji kutoka nje ya nchi jumla ya Dola za Marekani 667 (Sh1.5 trilioni),” amesema Biteko.
Amesema uwekezaji huo utaharakisha sekta anayoiongoza kuchangia asilimia 10 ya pato la Taifa kabla ya mwaka 2025 huku akibainisha kuwa kutokana na maboresho ya shughuli za madini hilo limewezekana hata kabla ya uwekezaji huo kufanyika.
“Kati ya Julai hadi Septemba 2022, sekta ya madini imeshachangia asilimia 9.7 katika pato la Taifa,” amesema Biteko mbele ya Rais Samia ambaye alikuwa akishuhudia utiaji saini huo.
Biteko amesema watasimamia vizuri utekelezaji wa mikakaba hiyo itakapoanza kutekelezwa nchini ili kuifaidisha nchi na wananchi wake.
Soma zaidi:
- Rais Magufuli awaweka kitanzini wakuu wa mikoa wasiojenga vituo vya kuuzia madini
-
Huyu ndiye bilionea mpya wa madini Tanzania
Undani wa mikataba
Kiongozi wa timu ya majadiliano na wawekezaji wa madini hayo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema mikataba iliyosainiwa iko katika maeneo makuu matatu ya uwekezaji.
Mkataba wa kwanza umehusisha kampuni ya Peak Rare Earth Limited ya Australia ili kuendesha mradi wa uchimbaji wa madini adimu mkoani Songwe kupitia kampuni mbili za ubia.
Kampuni hizo ni ya Mamba Minerals Corporation itakayojihusisha na uchimbaji wa madini na kampuni ya Mamba Refinery Corporation itakayojihusisha na uchenjuaji madini huku gharama za awali za uwekezaji katika mradi huu ni Dola za Marekani milioni 439 (Sh1 trilioni)
Mkataba wa pili unahusisha kampuni ya Evolution Energy Minerals Ltd ya Australia kuhusu mradi wa madini ya kinywe mkoani Lindi kupitia kampuni ya ubia ya Kudu Graphate ambapo gharama za awali za uwekezaji za mradi huo ni Dola za Marekani milioni 100 sawa na Sh234.6 bilioni
Kampuni ya EcoGraf ya Australia imeingia mkataba na Serikali ya uendelezaji wa uchimbaji wa madini ya kinywe ulioko mkoani Morogoro kupitia kampuni ya ubia ya Duma. Uwekezaji wa awali ni Dola za Marekani milioni 127.7 sawa na Sh299.6 bilioni.
Serikali inamiliki asilimia 16 ya hisa kwa kila kampuni za ubia zilizoanzishwa huku ikitarajia kujipatia faidia ya asilimia 51 kwa kila uwekezaji, kwa mujibu wa Prof Kabudi ambaye ni Mbunge wa Kilosa.
Mikataba iliyosaidiniwa leo mbele ya Rais ni ya aina tatu; makubaliano ya msingi kuhusu mgawanyiko wa faida za kiuchumi, mkataba wa wanahisa wa kampuni za ubia tatu, na katiba za kampuni za ubia.
Prof Kabudi amesema pia Watanzania watashirikishwa katika ngazi za juu ya kampuni hizo zikiwemo bodi za wakurugenzi ili kulinda maslahi ya nchi.