Umemejua unavyoweza kuchangia upatikanaji wa maji safi vijijini

June 3, 2019 3:27 am · Charles
Share
Tweet
Copy Link
  • Mifumo ya nishati ya jua ina gharama nafuu za uendeshaji vituo vya maji ukilinganisha na mifumo inayotumia dizeli na petroli.
  • Itasaidia kufanikisha lengo la Serikali la kuwafikishia maji safi na salama wananchi wa vijijini kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2020.

Lengo la sita la Malengo Endelevu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (Sustainable Development Goals) ambao Tanzania ni mwanachama  ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa maji safi na Salama kwa watu wote ifikapo mwaka 2030. 

Lakini Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wake, hasa maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya wizara ya Maji na Umwagiliaji ya mwaka 2018/19 , kulikuwa na vituo vya maji safi 123,888 maeneo ya vijijini ambavyo vingeweza kuhudumia asilimia 85.2  ya wananchi wanaoishi katika maeneo hayo. 

Hata hivyo, ni vituo 85,286 tu ndivyo vilithibitishwa kufanya kazi na hivyo kuhudumia asilimia 58.7 tu ya wananchi wa vijijini.

Moja ya changamoto kubwa inayovikabili vituo hivi ni gharama kubwa za uendeshaji, ikizingatiwa vituo vingi kati ya hivi vinaendeshwa kwa mafuta ya dizeli na petroli. 

Pia, mitambo ya dizeli na petroli inahitaji matengenezo ya mara kwa mara, ikiwemo matengenezo madogo ya kila mwezi na matengenezo makubwa ya walau mara mbili kila mwaka. 

Gharama hizi za uendeshaji zimefanya vituo vingi kushindwa kujiendesha na hivyo kushindwa kutoa huduma kwa wananchi.


Zinazohusiana: 


Na ndiyo maana serikali, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imekusudia kubadilisha mitambo yote ya kupampu maji vijijini, inayoendeshwa kwa dizeli na petroli na kuweka mitambo inayotumia nishati ya jua (Solar water pumps).

Kabla ya kufikia uamuzi huu, Benki ya Dunia iliendesha zoezi la kuwajengea uwezo, uelewa na ufahamu wataalamu wa maji pamoja na wadau wa sekta ya maji kutoka katika ngazi ya Wizara ya Maji, Serikali Kuu na Halmashauri nchini. 

Zoezi hili pamoja na mambo mengine, wataalam wa maji walisaidiwa kuelewa teknolojia zilizopo za mifumo ya kupampu maji kwa kutumia nishati ya jua, uwezo na gharama za mifumo husika. 

Pia Benki ya Dunia ilisaidia kushauri na kuandaa mfumo ambao sekta binafsi ingeweza kuongeza ushiriki wake katika miradi ya maji, kwa kuwa hadi sasa, ushiriki wa sekta binafsi ni wa kiwango cha chini.

Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali inakusudia kutumia nishati ya jua kwa ajili ya miradi yote ya kupampu maji (non-gravity water schemes) maeneo ya vijijini katika kipindi cha miaka mitano ijayo. 

Hatua hii inatokana na manufaa yatokanayo na teknolojia ya nishati ya jua, hasa kutokuhitaji matengenezo ya mara kwa mara baada ya kufungwa. 

Pia, tumeshuhudia gharama za mifumo ya nishati ya jua zikipungua kwa kasi, kwa zaidi ya asilimia 80 katika soko la dunia, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na hivyo kufanya mifumo ya nishati ya jua kuwa na gharama nafuu za uendeshaji ukilinganisha na mitambo ya dizeli na petroli.Mitambo ya kupumpu maji inayoendeshwa kwa nishati ya jua ina gharama nafuu na endelevu. Picha|Mtandao.

Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002 inaelekeza kuwapatia maji safi na salama wananchi wa vijijini katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao. 

Sambamba na hilo, Serikali imejiwekea malengo ya kuhakikisha kuwa asilimia 85 wananchi wa vijijini wanafikiwa na huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2020. 

Pamoja na kusisitiza sekta ya Umma na Binafsi kushirikiana kwa ukaribu kuhakikisha lengo hili linafikiwa, ninaamini matumizi ya teknolojia ya nishati ya jua, yatatoa mchango mkubwa katika kufikia lengo hilo endapo wadau wote katika sekta ya nishati na maji watayapa msukumo unaostahili.

Prosper Magali ni Mtaalamu wa Nishati Jadidifu mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 17, ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Nishati Jadidifu (Tanzania Renewable Energy Association) na mmoja wa wakurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa ya Alliance for Rural Electrification yenye Makao yake Makuu Brussels, Ubelgiji na pia Mkurugenzi wa Miradi na Ubunifu wa Kampuni ya Ensol Tanzania Ltd, waendelezaji miradi ya nishati jadidifu wa hapa Tanzania. Makala hii ni maoni yake binafsi.

Enable Notifications OK No thanks