Bei ya viazi mviringo yapanda Arusha
- Imepanda kutoka Sh90,000 hadi Sh100,000 katika kipindi cha wiki moja.
- Wafanyabiashara mkoani watapata faida ya Sh10,000 kwa kila gunia moja la kilo 100.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa viazi mviringo katika Mkoa wa Arusha leo watalala na tabasamu baada ya bei ya jumla ya zao hilo kupanda kwa Sh10,000 ndani ya kipindi cha wiki moja.
Takwimu za mazao makuu ya chakula zilizotolewa leo (Januari 10, 2022) na Wizara ya Viwanda na Biashara zinaonyesha kuwa bei ya juu ya gunia la kilo 100 la zao hilo linauzwa kwa Sh100,000 mkoani humo.
Bei hiyo imepanda kutoka Sh90,000 iliyorekodiwa Jumatatu Januari 03, 2022, sawa na kusema wafanyabiashara wataweka kipindoni Sh10,000 kwa kila gunia moja watakalouza leo sokoni.
Pia takwimu hizo ambazo hutolewa mara tatu kwa wiki, zinaonyesha kuwa bei ya chini ya viazi mkoani humo imepanda hadi Sh95,000 kutoka Sh80,000 iliyorekodiwa wiki iliyopita.
Kwa bei hizo zinazotumika leo, itakuwa ni maumivu kwa wanunuzi na kicheko kwa wafanyabiashara ambao kupanda kwa bei za mazao ndiyo faida kwao.
Licha ya kuwa bei ya juu na chini ya viazi mviringo katika Mkoa wa Arusha kupanda, bei ya juu kabisa ya zao hilo inayotumika leo kwa upande wa Tanzania Bara imerekodiwa mkoani humo pamoja na Mwanza na Lindi ambayo ni Sh100,000 huku bei ya chini ni Sh50,000 katika Mkoa wa Njombe na Dodoma.

Latest