Bei ya mahindi yapanda kwa miezi saba mfululizo
- Bei ya jumla ya zao hilo imefikia Sh101,815 Oktoba mwaka huu.
- Imekuwa akipanda tangu Aprili 2022.
- Upungufu wa mvua, kufunguliwa kwa mipaka kwachangia.
Dar es Salaam. Huenda wakulima na wafanyabiashara wakaendelea kuneemeka baada ya bei ya mahindi kuendelea kupanda kwa miezi saba mfululizo hadi kufikia Sh101,815 Oktoba mwaka huu.
Ripoti ya Tathmini ya Uchumi ya Novemba 2022 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa bei ya mahindi imekuwa ikipanda mfululizo kwa viwango tofauti tangu Aprili mwaka huu.
Mathalan, Septemba 2022, gunia la kilo 100 la mahindi lilikuwa likiuzwa kwa Sh95,931 lakini limeongezeka hadi Sh101,815 Oktoba sawa ongezeko la Sh5,884 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano ambayo hutumiwa zaidi na Watanzania.
BoT imeeleza katika ripoti hiyo kuwa, bei ya mahindi pia imepanda kwa asilimia 111.4 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kutoka Sh48,171 mwaka 2021 unaoishia Oktoba hadi Sh101,815 Oktoba mwaka huu.
Hiyo ni sawa na kusema wakulima na wafanyabiashara wameweka kibindoni Sh53,644 zaidi kwa kila gunia moja au sawa na kusema bei hiyo ya mahindi imeongezeka zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na bei ya mwaka jana.
Kupanda kwa bei kunawaumiza walaji kwa sababu wanalazimika kutoboa mifuko yao zaidi ili kupata zao hilo la chakula.
Kupanda kwa bei ya mahindi kumechangiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya zao hilo hasa nje ya nchi na kutokuwepo kwa mvua za kutosha katika msimu huu, jambo lililosababisha wakulima wapate mazao kidogo.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe katika hotuba zake ameendelea kusisitiza kuwa Serikali haitafunga mipaka na kuzuia mahindi yasiuzwe nje ya nchi ili kuwawezesha wakulima kufaidika na soko la kimataifa.
Pia katika kipindi hicho cha mwaka mmoja uliopita bei za mazao mengine ya chakula zimepanda ikiwemo viazi mviringo na mchele.
Mathalan, mchele umepanda hadi kufikia Sh261,418 kutoka Sh151,867 huku maharage yakipanda hadi Sh266,555 kutoka Sh172,065.
Latest
