Bei ya mahindi yaendelea kushuka Tanzania

January 14, 2022 2:17 pm · Maria
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwezi Novemba 2021 ilikuwa Sh49,683.5 ikiwa imeshuka kutoka Sh58,012.9 iliyorekodiwa Novemba 2020.
  • Sababu ya kushuka kwa bei hiyo ni kuwepo kwa akiba ya kutosha ya chakula na zao hilo kuwepo kwa wingi sokoni.

Dar es Salaam. Huenda wakulima wakasubiri kwa muda mrefu kupata faida katika kilimo cha mahindi baada ya bei ya zao hilo kushuka kwa Sh8,329 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita huku tabasamu likibaki kwa wanunuzi wa zao hilo.

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi December 2021 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  inaeleza kuwa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba 2021 ilikuwa Sh49,683 ikiwa imeshuka kutoka Sh58,012 iliyorekodiwa Novemba 2020.

Hiyo ni sawa kusema bei ya mahindi imeshuka kwa asilimia 14.4 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Kushuka kwa bei ya mahindi huenda kumewasononesha zaidi wakulima ambao wameikosa Sh8,329 ambayo walikuwa wanaipata kwa kila gunia moja katika bei ya Novemba 2020.

Kushuka kwa bei ya mahindi kunatokna na kuwepo kwa akiba ya kutoshwa kwa wakulima na masokoni na hivyo mahitaji ya zao hilo kupungua.

Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano ambayo hutumiwa zaidi na Watanzania.

Mazao mengine ambayo bei yake imeshuka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni maharage kwa asilimia 14.5, na viazi mviringo kwa asilimia 4.9. 


Zinahusiana: 


Wakati bei ya mazao hayo ikishuka, bei ya mchele imepanda hadi Sh154,394 mwezi Novemba 2021 kutoka Sh144,332 iliyorekodiwa Novemba 2020.

Uwele nao bei yake imepanda hadi Sh105,371 kutoka Sh88,438, na ile ya mtama imepanda hadi Sh163,777 kutoka 131,673 iliyorekodiwa Novemba 2020.

Hata hivyo, bei za mazao makuu ya chakula zimekuwa zikipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya uzalishaji pamoja na hali ya hewa.

Mathalan, katika mwezi November 2021 bei za mazao hayo yote zilipanda kwa kiasi kidogo na zingine kama za mchele, maharage, uwele na mtama ziliongezeka kwa kiasi cha wastani ikilinganishwa na mwezi uliotangulia wa Octoba 2021.

Akiba ya chakula yaongezeka

Wakati bei za mazao makuu ya chakula zikipanda na kushuka, akiba ya chakula katika ghala la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeongezeka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. 

Ripoti hiyo ya BoT inaeleza kuwa Novemba 2021 ghala hilo lilikuwa na tani 209,057, huku katika mwezi kama huo kwa mwaka 2020 ghala hilo lilikuwa na tani 110,289.

Mwenendo wa uhifadhi wa chakula katika ghala hilo ambalo huifadhi chakula kwa ajili ya dharura kama njaa umekuwa wa kupanda na kushuka katika miaka mitano iliyopita.

Ripoti ya BoT imeeleza kuwa kuongezeka kwa akiba ya chakula mwezi Novemba 2021 kulichangiwa na NFRA kununua tani 209,057 za mazao ya chakula ambapo ni zaidi ya kiwango cha mwaka kilichopangwa cha tani 165,000.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW