Balozi James: Hakuna Mtanzania aliyeshambuliwa Afrika kusini
- Asema picha mjongeo zinazosambazwa mtandaoni ni upotoshaji.
- Afrika Kusini imeahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wa mashambulizi hayo ya chuki dhidi ya wageni.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa kuna Watanzania wanashambuliwa nchini Afrika Kusini, ikieleza kuwa picha na video zinazooneshwa si za matukio ya sasa bali ni za zamani zilizohaririwa upya kwa lengo la kupotosha umma.
Taarifa ya Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini iliyotolewa leo Aprili 28, 2026 inafafanua kuwa video hiyo ni ya miaka ya nyuma na imehaririwa upya ili kueneza taharuki na kupotosha kuhusu hali ya usalama wa Watanzania nchini humo.
“Picha mjongeo (Video clips) zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii zikionesha raia wa Tanzania akishambuliwa nchini Afrika Kusini ni upotoshaji unaofanywa na watu wenye nia ovu…ni za mwaka 2023 na zimehaririwa upya na watu wenye nia ovu na kuzihusanisha na matukio ya sasa yanayoendelea nchini humo,” amesema Balozi Bwana kupitia taarifa hiyo.
Kwa wiki kadhaa sasa, kumekuwa na mjadala mkali mtandaoni kufuatia kusambaa kwa video zinazoonesha watu wanaodaiwa kuwa raia wa Afrika kusini wakiwashambulia raia wa kigeni jambo lililozua hofu na taharuki.
Suala hilo limegonga vichwa mbalimbali mtandaoni kutokana na matukio yanayojirudia mara kwa mara ya kwa nchi hiyo kushambulia wageni kutokana na kile wanachodai ni kuongezeka kwa ukosefu wa ajira, uhalifu, pamoja na ushindani wa fursa za kiuchumi unaohusishwa na wahamiaji kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Kutokana na sintofahamau hiyo Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini umefanya mawasiliano ya moja kwa moja na viongozi wa jumuiya za Watanzania waliopo katika majimbo yote tisa ya nchi hiyo, kupitia mazungumzo hayo, imebainika kuwa hakuna Mtanzania aliyeshambuliwa au kudhurika kutokana na vurugu zinazoendelea dhidi ya wahamiaji.
Balozi Bwana ameongeza kuwa juhudi zinaendelea kufanywa kwa kushirikiana na mamlaka za Afrika Kusini ili kuhakikisha usalama wa Watanzania unaimarishwa na kulindwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za kimataifa.
Katika wito wake kwa umma, wizara hiyo imewataka wananchi na hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii kuwa makini kabla ya kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa.
“Wizara inatoa rai kwa waandaa maudhui mitandaoni kuhakikisha kuwa wanakuwa na taarifa sahihi kabla ya kusambaza katika mitandao, ili kuepuka kuzusha taharuki zisizo za lazima kwa jamii,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa ikiwemo Shirika la Habari la DW, limeeleza kuwa Serikali ya Afrika Kusini imeahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wa mashambulizi hayo ya chuki dhidi ya wageni.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo imesisitiza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha amani na utulivu pamoja na kudhoofisha misingi ya utawala wa sheria.
Latest