Tahariri: Waliowashambulia wanahabari wa Mwananchi wachukuliwe hatua kali
Julai 22 mwaka huu wanahabari wawili wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) na dereva wao walivamiwa na watu wasiojulikana, kujeruhiwa na kuporwa mali zao wakati wakitelekeleza majukumu yao katika uwanja wa Bulyaga, Temeke jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa uongozi wa MCL, waandishi hao Fortune Francis na Sunday George pamoja na dereva wao Omary Mhando, walishambuliwa Jumamosi, Julai 22, 2023 walipofika kufuatilia maandalizi ya mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama cha Chadema uliofanyika jana Jumapili.
MCL inaeleza kuwa katika tukio hilo wafanyakazi hao walishambuliwa, kujeruhiwa, kuporwa na kuharibu mali ambavyo ni vitendea kazi vya wanahabari hao. Tayari kampuni hiyo ya habari imewasilisha taarifa polisi kwa hatua zaidi.
Habari ya kushambuliwa wanahabari ni ya kushtusha hasa katika kipindi ambacho Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha uhuru wa habari na demokrasia nchini.
Vitendo vya kushambulia wanahabari na hata raia wengine ni uvunjifu wa amani na vinatishia uhuru wa habari na vyombo vya habari nchini. Matukio kama haya yanaweza kupunguza ari kwa wanahabari kuripoti matukio muhimu katika ujenzi wa Taifa letu kwa kuhofia tu usalama wao, jambo ambalo si utamaduni wa Watanzania.
Vitendo viovu kama hivyo si tu vinapingana na katiba na sheria za nchi bali vinataka kutengeneza taifa la watu wa hovyo, waoga na wasiojali utu na maendeleo ya mamilioni ya Watanzania wanaohitaji taarifa sahihi kuhusu masuala mbalimbali ya Taifa hili.
Ni aibu kuona matukio kama haya yanatokea wakati huu kiasi cha kurudisha nyuma jitihada za Serikali na wadau kurejesha uhuru wa habari Tanzania. Tusikubali kurudi tulikotoka. Unawashambulia wanahabari kwa sababu gani? Ili ufanikiwe jambo gani? Hii si sawa katika nchi ya kidemokrasia kama Tanzania.
Tunalaani vikali vitendo hivyo na tunavisihi vyombo vya dola vifanye uchunguzi wake wa kina na kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuhusika katika tukio hilo.
Kama alivyosema Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akilaani tukio hilo Julai 22, si vigumu kuwabaini wahalifu kwa kuwa eneo husika la tukio linajulikana. Kwa minajili hii tunasihi haki itendeke.
Tunaamini kuwa iwapo wahalifu waliowashambulia waandishi wa habari wa MCL watachukuliwa hatua kwa haraka, hali hiyo itasaidia kupunguza hofu miongoni mwa wanahabari na kujenga jamii ya watu wastaarabu.
Watanzania tuna kila sababu ya kukemea vitendo hivyo na kuzuia visitokee tena ili kulinda uhuru wa habari na kuchagiza maendeleo ya nchi.