Bajeti na Corona: Njia zitakazosaidia kusisimua uchumi wa Tanzania wakati wa Corona

June 23, 2021 5:40 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kwa kutumia sera za kifedha na njia za kibajeti. 
  • Sera za kifedha siyo za moja kwa moja kwa kuwa benki kuu huingiza pesa kwenye uchumi kupitia benki za biashara.

Mapema Machi 17, 2020 Mwanahabari mashuhuri wa masuala ya uchumi Martin Wolf aliandika kwenye gazeti la Financial Times la Uingereza kuwa “Kirusi hiki cha Corona ni dharura ya kiuchumi pia”.

Wakati makala hiyo inaandikwa, Tanzania ilikuwa na siku moja tu tangu itangaze kisa cha kwanza cha ugonjwa wa virusi vya Corona (Uviko-19).

Mwaka 2020 kama taifa hatukukubaliana kuwa Uviko-19 ni dharura ya kiuchumi pia. Kuliibuka makundi makubwa mawili juu ya Uviko-19 na uchumi wetu ambayo ni wale waliokuwa na mtazamo wa kulikadiria janga kwa uzito mdogo (Corona Minimalist) na wale waliolikadiria kwa hofu kubwa (Corona Maximalists).

Mwaka mmoja baadaye, kama taifa na kwa kiwango kikubwa tunakubaliana kuwa Uviko-19 imeathiri uchumi wetu.

Mwaka jana niliandika sana kuhusu Uviko-19 na athari zake kwenye uchumi wa dunia, Afrika na Tanzania. Mwaka 2021, athari za Uviko-19 sasa ni bayana kwenye uchumi wetu.

Wakati huu wa msimu wa bajeti nilitarajia kuwa na mkakati maalum wa kusimumua uchumi ili kuendelea kukabiliana na athari za Uviko-19.

Sababu za kufanya hivi ni kuwa; kama tunavyoshuhudia Uviko-19 imesababisha UVIKO wa kiuchumi (Economic Covid). UVIKO wa kiuchumi ni matokeo ya mshtuko wa kiuchumi kutoka nje na ndani kama yalivyo madhara ya UVIKO-19 duniani kote.

Janga la Corona limeathiri usafirishaji wa bidhaa duniani na hivyo kuongeza bei ya baadhi ya bidhaa katika maeneo mbalimbali. Picha| CNN.

Msingi wa hatua za kuchukua

Kumekuwepo na mjadala kuhusu baadhi ya njia za kusisimua uchumi (stimulus packages) ili kulinda uchumi wetu ambazo siyo nzuri zaidi na stahimilivu.

Njia za kusisimua uchumi (Stimulus measures).

Hizi ni sera za kifedha (monetary policies) na njia za kibajeti (fiscal measures). Sera za kifedha siyo za moja kwa moja kwa kuwa benki kuu huingiza pesa kwenye uchumi kupitia benki za biashara kwa kutumia zana tumizi (Open Market Operations) na wakati huo huo ikipunguza viwango vya riba.

Sera za kibajeti zenyewe hufanya kazi moja kwa moja kwa Serikali kukopa na kutumia. Lengo la njia hizi ni kutaka uchumi uendelee kuchangamka ili shughuli za kiuchumi zisisinyae.

Sera hizi mbili tunaziita zana za kuongoza uchumi kwa kuhakikisha kuna shughuli za kiuchumi (Demand Management Tools). Tunaweza kufikiria njia hizo katika wakati huu kwa tahadhari kwa kuwa Uviko-19 hasa kwa maana ya UVIKO ya kiuchumi siyo wingu linalopita.


Hatua muafaka

Katika mazingira ya kawaida, hatua za kusisimua uchumi za kibajeti huusisha nakisi ya matumizi kwa wigo wa asilimia 1 na asilimia 2 ya pato la taifa (GDP). Kwa mujibu wa Taarifa ya Uchumi ya Wizara ya Fedha na Mipango pato la taifa nchini Tanzania lilifikia Sh148 trilioni mwaka 2020 kwa takwimu hizo kiwango cha kusisimua uchumi ni kati ya Sh1.3 trilioni hadi Sh2.6 trilioni.

Kwa mujibu wa Taarifa ya hali ya uchumi Tanzania mwaka 2020 (Economic Survey 2020) mishahara katika sekta rasmi ni wastani wa Sh800, 000 na kiwango cha chini cha mishahara maeneo ya mijini ni wastani wa Sh352,000. Hata hivyo, si rahisi kukokotoa kiwango cha chini cha mishahara katika sekta isiyo rasmi yenye zaidi ya robo tatu au asilimia 87 ya watu million 21 ya nguvu kazi nje ya kilimo.

Wastani wa viwango hivyo viwili ni kama Sh463,000 na ukihusisha mfumuko wa bei ni Sh513,000.

Asilimia moja ya GDP inaweza kulipa wafanyakazi milioni 4.6 ambao ni moja ya sita ya nguvu kazi yote kwa mwezi mmoja. Lakini hapa tunaweza kuangalia kwa miezi mitatu au sita, ambayo inaweza kucover watu million 1.7 kwa miezi mitatu na watu 700,000 kwa miezi 6.

Kwa Tanzania, ukilinganisha na nchi nyingine nakisi ya bageti bado haijafika kwenye mstari mwekundu yaani kiwango cha asilimia 5 ya GDP jambo linaloacha fursa (fiscal space) ya kukopa. Hata hivyo, kukopa zaidi katika mazingira haya ambayo viashiria (variables) vikubwa vya uchumi vinaweza kuwa arijojo si sahihi sana.

Bunge limepitisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ya Sh36.6 trilioni ambayo itaanza kutekelezwa Julai mosi. Je itasaidia kupunguza athari za Corona?. Picha| Bunge la Tanzania.

Sera za kifedha

Katika njia hii tunaangali namna benki zinavyoweza kulinda ajira. Njia ya moja kwa moja ni kuruhusu benki za biashara kufanya biashara ya dhamana za Serikali (government bonds) kwa muda mfupi na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupata fedha kwa makubaliano ya kununua tena (Repurchase Agreement-REPOs).

Changamoto kuu katika njia hii ni kuwa benki hubadilishana dhamana zenye vihatarishi (risk) vikubwa kwa vihatarishi vidogo. Inahitaji umakini mkubwa na msawazo makini kutekeleza njia hii kwa kuwa uchumi wetu umetoka mikopo chechefu miaka ya hivi karibuni. Ni vema tukaangazia njia nyingine ambayo naona ni muafaka zaidi.

Kuanzisha mfuko wa kulinda ajira kwa muda mrefu (Lifeline fund).

Kwa nini njia ni nzuri zaidi kuliko nyingine za kusisimua uchumi? Hii ni kwa sababu stimulus measure huchochea mwingiliano wa kijamii ambao hurutubisha kuenea kwa kirusi Corona. Yaani njia zile zimejikita kwenye ‘supply response’. Pia, watu katika nyakati kama hizi huwa hawatumii kwa sababu hawaijui kesho yao na kwa upande mwingine hatutahitaji kukopa.

Nchi zilizoendele kama Uingereza, Uholanzi, Denmark zimesema zitawalipa wafanyakazi waliopo kwenye kampuni mbalimbali. Kwa mfano Uingereza itawalipa asilimia 80 ya mishahara. Hata hivyo, Tanzania haiwezi njia kwa sababu mbili hatuna fedha na uchumi wetu kwa upana ni wa sekta isiyo rasmi na fedha nyingi mtaani mahitaji huzidi ugavi.

Mfuko huu kwa kawaida huwa ni kwenye kati ya asilimia 0.5% hadi asilimia moja ya GDP na kwa Tanzania inaweza kuwa kati ya Sh500 bilioi hadi Sh630 bilioni. Kama nilivyoeleza awali kwa sasa si sahihi kukopa fedha hizo lakini njia mbili zinaweza kutumika.

Mosi, kuhamisha baadhi ya matumizi (reallocation) ya bajeti ndani ya wigo wa nakisi iliyopo. Kinachoweza kufanyika ni kusimamisha baadhi ya miradi ya maendeleo au kupunguza rasilimali fedha na kukata matumizi ya bajeti ya matumizi yasiyo ya lazima nje ya mishahara.

Pili, kupitia fedha za nje. Hapa nchi zinaweza kushirikiana kupata muda zaidi wa kulipa deni la nje (Moratorium) na njia kimsingi hii ni kama budget support. Kwa mfano, tunaweza kuchelewesha sehemu ya Sh2.4 trilioni tunayotakiwa kulipa mwaka ujao wa fedha. Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed naye ana pendekezo linalofanana na hili.

Mfuko wa aina hiyo unafanya kazi kwa kuwa na mkopo kwenye masharti mepesi kwa grace period ya miezi sita hadi 12 na muda ambao unaweza kuhuishwa wa miaka mitatu hadi mitano. Ili kufanikisha malengo yake, mfuko unatakiwa kutoa kiwango sawa cha mkopo kila muajiriwa, kutolewa kila mwezi kwa kipindi maalumu na ihusiane na idadi ya wafanyakazi.

Pia, unatakiwa kunufaisha pande mbili ya kuwapatia mikopo wafanyakazi (check off loans) na waajiri (kama business loans).

Kwa mfano, ikiwa mgahawa una wafanyakazi 10, ukasema kila mfanyakazi atapata Sh50,000 kwa kipindi cha miezi mitano basi mgahawa huo unahitaji Sh2.5 milioni kwa kipindi hicho.

Mipango ya kuwawezesha wananchi kiuchumi pia iwafikie wafanyabiashara wadogo hasa wanawake kupata mitaji kuinua biashara na kujipatia kipato cha kuendesha familia. Picha| K15 Photos.

Iwapo zitotelewa sawa kwa wafanyakazi na mwenye biashara na bila riba kwa miaka mitano, biashara italipa Sh10,000 na mfanyakazi nusu ya hiyo kila mwezi mpaka hali itakapotengemaa.

Benki za biashara zinapaswa kushughulikia usimamizi na suala la aina ya biashara na wafanyakazi wanaostahili huduma hiyo.  

Njia hizi lengo kuu ni kupunguza madhara ya tatizo kwa kuweka sakafu katika uchumi.

Mbali na njia hizo ni muhimu kwa Afrika kuendelea kuimarisha ushirikiano na jumuiya ya kimataifa ili ziziongeze nchi zetu muda wa kulipa madeni au kuyafuta yanayowezekana. Jambo hilo muhimu kwa sababu kutota kwa uchumi wa Afrika kunaathiri pia uchumi wa dunia. Ni vyema vikwazo visivyo vya lazima vikaondoshwa. Corona imeleta dhahama Afrika kwa kuleta “umbali kijamii” na umbali wa kifedha (distancing).

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dk Akinwumi Adesina hivi karibuni aliandika kuwa “kutokukaribiana kijamii ni lazima kwa sasa lakini si wakati wa kutokukaribiana kwenye sera za kifedha.”

Dk Bravious Kahyoza ni Mchumi, Mchambuzi wa sera na Mwandishi wa habari wa biashara.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW